Vita dhidi ya shisha, sigara yaendelea

Dar es Salaam. Wakati matumizi ya shisha na sigara za kielektroniki yakizidi kuenea kwa baadhi ya vijana nchini, wataalamu wa afya wameeleza tabia hiyo itaongeza mzigo wa saratani na magonjwa mengine yasiyoambukiza ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa. Ili kudhibiti hilo, wanaandaa mpango wa Taifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku na bidhaa zake ili kulinda afya…

admin Avatar

by

5 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Wakati matumizi ya shisha na sigara za kielektroniki yakizidi kuenea kwa baadhi ya vijana nchini, wataalamu wa afya wameeleza tabia hiyo itaongeza mzigo wa saratani na magonjwa mengine yasiyoambukiza ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.

Ili kudhibiti hilo, wanaandaa mpango wa Taifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku na bidhaa zake ili kulinda afya ya vijana na kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza nchini.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana Jumamosi, Mei 30, 2026 na Shirika la Shirika la Afya Duniani (WHO) takribani vijana milioni 15 wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 15 ulimwenguni wanatumia sigara za kielektroniki (e-cigarettes), huku vijana milioni 40 wa kundi hilo la umri wakitumia bidhaa za tumbaku.

Takwimu hizo zimetolewa kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Dunia ya Kutotumia Tumbaku yanayofanyika leo Mei 31, mwaka huu, yenye kaulimbiu ya: “Kufichua Ushawishi wa Bidhaa za Nikotini na Tumbaku.”

Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dk Harrison Chuwa amesema nchini Tanzania vijana wengi wadogo wanaanza kuwa na uraibu na shisha na sigara za kielektroniki bila kujua madhara yake kiafya.

Amesema matumizi ya tumbaku yanaendelea kuwa miongoni mwa visababishi vikuu vya saratani duniani, huku takribani asilimia 30 ya visa vya saratani vikihusishwa moja kwa moja na matumizi ya bidhaa za tumbaku.

Amesema saratani ya mapafu ndiyo inayojulikana zaidi kuhusishwa na tumbaku, lakini madhara yake hayaishii hapo kwa kuwa, saratani za kichwa na shingo, pamoja na baadhi ya saratani za mfumo wa chakula, pia zimehusishwa na uvutaji wa sigara.

“Karibu saratani zote zina uhusiano kwa namna moja au nyingine na matumizi ya tumbaku, lakini saratani za kichwa na shingo ndizo zinazoonekana zaidi kuhusishwa na uvutaji sigara,” amesema.

Dk Chuwa amesema changamoto kubwa kwa sasa ni mtazamo wa baadhi ya vijana wanaoona matumizi ya shisha na sigara za kielektroniki kama sehemu ya maisha ya kisasa na burudani, bila kufahamu athari zake za muda mrefu kiafya.

Amesema kipindi kimoja cha kuvuta shisha kwa takribani saa moja kinaweza kuwa sawa na kuvuta pakiti tano za sigara za kawaida.

“Mtu anaweza kukaa kwa saa moja akivuta shisha, jambo ambalo ni sawa na kuvuta pakiti tano za sigara. Wengine huendelea kufanya hivyo kwa saa kadhaa usiku mzima, hivyo kujiweka katika hatari kubwa ya kupata saratani pamoja na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu,” amesema.

Amesema kutokana na hali hiyo, kuna umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti matumizi ya tumbaku na bidhaa zake ili kulinda afya ya vijana na kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza nchini.

Dk Chuwa amesema wataalamu wa afya wamekuwa sehemu ya maandalizi ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Saratani; na awamu ya kwanza imekamilika na maandalizi ya awamu ya pili yanaendelea.

Amesema katika mapendekezo yaliyowasilishwa, wataalamu wameelekeza nguvu katika kuimarisha elimu ya afya kwa umma na kudhibiti matumizi ya tumbaku kupitia sera na hatua za kiuchumi.

“Tumependekeza kuimarisha kampeni za utoaji elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya tumbaku na kuangalia uwezekano wa kuongeza kodi kwa bidhaa za tumbaku ili kupunguza matumizi yake, hasa kwa vijana,” amesema.

Amesema ingawa sigara tayari zinatozwa kodi kubwa nchini, wataalamu wanaamini bado kuna nafasi ya kuimarisha zaidi hatua hizo ili kufikia viwango vinavyoshauriwa kimataifa.

Hata hivyo, amesema jukumu la kutafsiri mapendekezo hayo kuwa sera na hatua za utekelezaji, liko mikononi mwa Serikali kupitia Wizara ya Afya na mamlaka nyingine husika.

Akizungumzia hali ya saratani zinazohusishwa na uvutaji sigara nchini, Dk Chuwa amesema Tanzania bado ina viwango vya chini vya saratani ya mapafu ikilinganishwa na baadhi ya mataifa mengine duniani.

Amesema saratani za kichwa na shingo zinazohusishwa na matumizi ya tumbaku,  zinakadiriwa kushika nafasi ya tano au sita miongoni mwa saratani zinazoongoza nchini.

Kwa upande wa saratani ya mapafu, amesema bado haijajumuishwa miongoni mwa saratani 10 zinazoongoza nchini, ingawa baadhi ya wataalamu wanaamini uwezo mdogo wa kutambua ugonjwa huo mapema unaweza kufanya baadhi ya visa kutoripotiwa ipasavyo.

“Kuna wagonjwa wanaotibiwa kwa muda mrefu wakidhaniwa kuwa na kifua kikuu, lakini baadaye hubainika kuwa walikuwa na saratani ya mapafu. Hivyo ni muhimu kuendelea kuimarisha uchunguzi na utambuzi wa mapema,” amesema.

Wakati Serikali ikiandaa awamu ya pili ya Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Saratani, wataalamu wanaamini vita dhidi ya saratani haviwezi kufanikiwa bila kudhibiti matumizi ya tumbaku na kuongeza uelewa wa umma kuhusu hatari za shisha, sigara za kawaida na sigara za kielektroniki.

WHO imeeleza katika nchi zenye takwimu zinazopatikana, vijana wana uwezekano mkubwa mara tisa zaidi wa kutumia sigara za kielektroniki kuliko watu wazima.

Kwa mujibu wa shirika hilo, zaidi ya watu milioni saba duniani hufariki dunia kila mwaka kutokana na matumizi ya tumbaku, huku bidhaa hizo zikisababisha vifo vya hadi nusu ya watumiaji ambao hawaachi matumizi yake.

WHO imezituhumu kampuni za tumbaku na nikotini kwa kubuni bidhaa zinazolenga kuwavuta vijana kupitia ladha mbalimbali, vifungashio vinavyovutia, matangazo ya kidijitali, mitandao ya kijamii na ushawishi wa watu maarufu.

Shirika hilo limesisitiza kuwa uraibu wa nikotini unaweza kushindwa iwapo mtumiaji ataamua kuacha. Kwa mujibu wa WHO, ndani ya dakika 20 baada ya kuacha matumizi ya tumbaku mapigo ya moyo hupungua, ndani ya wiki mbili hadi 12 uwezo wa mapafu huanza kuimarika, na baada ya mwaka mmoja hatari ya ugonjwa wa moyo hupungua kwa nusu.

WHO imezitaka Serikali, mashirika ya kiraia na vijana kushirikiana kudhibiti matumizi ya bidhaa za nikotini ili kulinda afya ya kizazi cha sasa na kijacho.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports