WASICHANA WA SHULE 11 MAFIA WANUFAIKA NA SETI 2,408 ZA PEDI KUTOKA TEEMO – Habari Mpya

Na Mwamvua Mwinyi, Mafia Jumla ya seti 2,408 za taulo mbadala za kike (Reusable Pads) zimetolewa kwa wanafunzi wa kike katika shule 11 za sekondari Wilaya ya Mafia kupitia awamu ya pili ya mradi wa “Wezesha Wasichana – Tabasamu Mpaka Mwisho” unaotekelezwa na Shirika la Harakati na Uwezeshaji wa Mazingira Tanzania (TEEMO). Mradi huo unaofadhiliwa…

admin Avatar

by

2 minutes

Read Time

Na Mwamvua Mwinyi, Mafia

Jumla ya seti 2,408 za taulo mbadala za kike (Reusable Pads) zimetolewa kwa wanafunzi wa kike katika shule 11 za sekondari Wilaya ya Mafia kupitia awamu ya pili ya mradi wa “Wezesha Wasichana – Tabasamu Mpaka Mwisho” unaotekelezwa na Shirika la Harakati na Uwezeshaji wa Mazingira Tanzania (TEEMO).

Mradi huo unaofadhiliwa na C-Weed Mwani, CEAMSA na Cargill unalenga kuboresha usimamizi wa afya ya hedhi kwa wasichana, kupunguza utoro unaotokana na changamoto za hedhi, kuimarisha usafi binafsi, kuongeza ufaulu wa masomo, kujenga kujiamini na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Akizindua awamu ya pili ya mradi huo, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Taifa Costantino, aliwashukuru wadau waliofanikisha utekelezaji wake na kueleza kuwa umefungua fursa kwa wasichana kupata mazingira bora ya kujifunzia na kutimiza ndoto zao.

Aliwasisitiza wanafunzi kuendeleza utamaduni wa usafi binafsi na utunzaji wa mazingira, huku akiwataka kutumia walimu wa malezi kama sehemu salama ya kupata ushauri na msaada wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali wawapo shuleni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TEEMO, Winfrida Shonde, alieleza uwekezaji kwa mtoto wa kike ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya jamii.

“Tunaamini kuwa msichana mwenye afya bora, elimu bora, kujiamini na mazingira salama ana nafasi kubwa zaidi ya kufikia ndoto zake na kuchangia maendeleo endelevu ya Tanzania,” alisema Shonde.

Alieleza kuwa mradi huo umejengwa katika nguzo sita ambazo ni upatikanaji wa taulo mbadala za kike, elimu ya afya ya hedhi na usafi binafsi, kujenga kujiamini na kukuza uongozi kwa wasichana, kuboresha mahudhurio na ufaulu wa masomo, kuimarisha mazingira salama ya shule yasiyo na unyanyasaji na kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya plastiki.

Shule zilizofikiwa na mradi huo ni Kilindoni, Raphta, Micheni, Baleni, Kidawendui, Kirongwe, Bweni, Jibondo, Jojibaki, Omari Kipanga na Kitomondo Sekondari.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi walionufaika na mradi huo, mwanafunzi wa Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Kitomondo, Ummulkheir Wabu, alisema taulo hizo zitasaidia kuongeza mahudhurio darasani na kuboresha ufaulu wa masomo.

Mradi huo unaotekelezwa na TEEMO kwa ufadhili wa Cargill, C-Weed Mwani na CEAMSA unatarajiwa kuendelea kuboresha afya, elimu na ustawi wa wasichana, huku ukichangia utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu katika jamii.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports