Dodoma. Tanzania inaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kuziba pengo la ufadhili wa miradi ya miundombinu linalokadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 2.5 (Sh6.5 trilioni) kwa mwaka.
Serikali imekiri kuwa haiwezi kuziba pengo hilo kwa kutegemea bajeti pekee, hivyo imeelekeza nguvu katika kuimarisha mfumo wa PPP kama njia ya kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, wakati wa mhadhara maalumu uliofanyika jana Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Alikuwa akiwasilisha ramani ya kimkakati ya kubadilisha sekta ya miundombinu na huduma za umma, katika mkutano uliowakutanisha wasomi, viongozi wa serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wananchi wa kawaida.
Mada kuu katika mhadhara huo ilikuwa: “Kubadilisha Miundombinu na Huduma za Umma Tanzania: Nafasi ya Kimkakati ya PPP katika Kufanikisha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) kuelekea Dira 2050.”
Akizungumza katika mhadhara huo, Kafulila amesema utegemezi wa mapato ya kodi na ongezeko la deni la taifa vimeifanya serikali kutafuta vyanzo mbadala vya kugharimia miradi mikubwa kama SGR, nishati na miundombinu ya kidijitali.
“Ubia unawezesha utekelezaji wa miradi hiyo bila kuongeza mzigo wa moja kwa moja kwa serikali, jambo linalotoa nafasi zaidi ya kifedha ya utekelezaji wa miradi ya kijamii katika sekta za afya, elimu na nyinginezo,” amesema Kafulila.
Amefafanua kuwa katika FYDP IV (2026/27–2030/31), mahitaji ya uwekezaji yamekadiriwa kufikia Sh477 trilioni.
Kwa mujibu Kafulila, sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya fedha hizo, sawa na Sh334 trilioni, huku asilimia 51 ya kiasi hicho, sawa na Sh170 trilioni, ikitarajiwa kupatikana kupitia mpango wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).
“Sekta muhimu zitakazohitaji ushiriki wa sekta binafsi ni pamoja na nishati inayokusudia kuzalisha megawati 5,000 katika kipindi cha miaka mitano ijayo, usafirishaji ikiwemo uboreshaji wa bandari na barabara za tozo, huduma za maji safi na salama pamoja na miundombinu ya kijamii kama makazi ya wanafunzi,” amesema.
Kafulila alisema mageuzi ya mashirika ya umma (SOEs) yanalenga kuongeza tija badala ya ugawaji wa rasilimali pekee, kwa kutumia ipasavyo ardhi, bandari na rasilimali nyingine.
Ameongeza kuwa bila mageuzi, mashirika hayo yanaweza kuigharimu serikali hadi kufikia Sh12 trilioni kufikia mwaka 2030, na kubainisha kuwa PPP inaweza kupunguza mzigo huo kwa asilimia 70.8.
Kafulila amefafanua kuwa tofauti na watu wengi wanavyofikiri, PPP si ubinafsishaji.
“Katika ubinafsishaji, sekta binafsi humiliki mali husika, lakini katika ubia, serikali huendelea kumiliki mali na kubaki na jukumu la jumla la usimamizi,” amesema.
Amesema PPP ni mfumo wa kugawana hatari za uwekezaji ambapo sekta binafsi hutoa huduma kwa muda wa mkataba kabla ya kurejesha jukumu kwa serikali.
Ili kuvutia wawekezaji, Kafulila alibainisha kuwa serikali imeweka vivutio kama ruzuku ya kuziba pengo la uhimilivu wa miradi, dhamana za serikali na kurahisisha ununuzi, hasa baada ya marekebisho ya sheria yaliyofanywa mwaka 2023.
Akizungumza katika mdahalo huo wa wazi kwa umma, Mhadhiri wa UDOM na mtaalamu wa PPP aliyeidhinishwa na Benki ya Dunia, Dk Abiud Bongole, amesema Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) kinahitaji kuimarishwa ili kuongeza ufanisi.
“Ili kuongeza kasi ya maendeleo tunahitaji kuimarisha na kuboresha Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) ili kiwe na mamlaka makubwa zaidi ya kiutendaji,” amesema.
Amependekeza kibadilishwe na kupewa hadhi ya mamlaka kamili kama ilivyo Uingereza na kwamba taasisi zote za serikali zinapaswa kuwa na wataalamu wa PPP.
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho mwenye ithibati ya Benki ya Dunia katika masuala ya ubia, Dk Anastasia Njiku, amesema hivi sasa UDOM ina miradi 11 ya PPP, miwili ikiwa hatua za mwisho za mazungumzo na wawekezaji.
“Miradi miwili imefikia hatua za mwisho za mazungumzo na wawekezaji na kwamba inatarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni,” alisema, na kupongeza PPPC kwa kushirikisha wahadhiri katika mafunzo ya Benki ya Dunia hivyo kuongeza utaalamu wa ndani.
Mchumi na mtaalamu mwingine wa PPP aliyeidhinishwa na Benki ya Dunia, Dk Bravious Kahyoza, alisema bado kuna mkanganyiko kuhusu mchango wa sekta binafsi kufikia asilimia 70 katika utekelezaji wa FYDP IV.
“Kabla ya utekelezaji wa FYDP IV kuanza, kunapaswa kuwepo mkakati wa wazi utakaobainisha namna mpango huo utakavyogharimiwa,” amesema.
Aliongeza kuwa si kila uwekezaji wa kawaida wa sekta binafsi unapaswa kuhesabiwa katika lengo hilo la kuchangia asilimia 70.
“Asilimia 70 inayozungumziwa hapa inaangazia mifumo mbadala ya ufadhili na mikakati ya uhamasishaji wa rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo,” amefafanua.
Kihistoria, Tanzania imekumbwa na changamoto za kugharimia utekelezaji wa miradi ya miundombinu kutokana na utegemezi wa bajeti, huku mahitaji yakiongezeka.
Hata hivyo, kufikia Aprili 2026, Serikali imetambua miradi 113 inayoweza kutekelezwa kupitia PPP, na asilimia 32 ya bajeti ya miradi inaweza kuhamishiwa PPP ili kupunguza shinikizo la hazina na kuongeza kasi ya maendeleo.
Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof Razack Lokina, alisema PPP ni muhimu kwa vyuo vikuu hasa kwenye tafiti na kubainisha kuwa kwa UDOM inafungua zaidi umuhimu wa mijadala kwenye utekelezaji wa Dira 2050.
“PPP ni muhimu kwani serikali haina rasilimali za kutosha kwendana na mahitaji. Mijadala hii ni muelekeo sahihi katika kufikia malengo yetu,” amesema.
“Kwenye utekelezaji wa PPP, lengo liwe kujibu changamoto halisi za watu na kupambana umaskini,” ameongeza Profesa Lokina.

















