Moshi. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amewataka wanachama wanaotamani kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho kujipima kwanza uwezo wao kabla ya kuingia kwenye kinyang’anyiro.
Wasira ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Juni 6, 2026, alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, wakiwemo viongozi wa mabaraza ya jumuiya na wazee wa chama hicho.
Amesema CCM inahitaji viongozi wenye uwezo, msimamo thabiti na wanaoweza kulinda maslahi ya chama bila kuyumbishwa na mazingira ya kisiasa.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, akizungumza na wanachama wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini pamoja na viongozi wa mabaraza ya jumuiya na wazee wa chama hicho, katika ofisi za CCM Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo alisisitiza mshikamano, uhai wa chama na utekelezaji wa majukumu ya kisiasa kwa kuzingatia maadili na taratibu za chama.
“Mwaka ujao tutafanya uchaguzi. Kila anayetamani kugombea nafasi ya uongozi anapaswa kujiuliza kwanza kama ana uwezo wa kuongoza nafasi hiyo,” amesema Wasira.
Ameongeza kuwa kiongozi wa CCM anapaswa kuwa mwaminifu, mwenye msimamo na asiyeweza kuhamisha siri za chama kwa vyama vingine.
“Hatuhitaji viongozi wanaokwenda chama kingine kufichua siri za chama. Kiongozi wa aina hiyo hatufai,” amesisitiza.
Wasira pia amewataka wanachama kuacha makundi na badala yake kushirikiana katika kuimarisha chama na utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Amesema ushindani wa uongozi unapaswa kuzingatia uwezo wa mtu na mahitaji ya chama, si maslahi binafsi.
“Tunahitaji viongozi wanaoweza kujibu hoja za upinzani kwa hoja na sera, si kwa matusi. Kiongozi bora hushinda kwa hoja na uelewa,” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa CCM ni chama cha wanachama na si cha viongozi pekee, hivyo kila mwanachama anapaswa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, amesema chama hicho kimeendelea kufanya vizuri katika mkoa huo, akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano serikali imetoa Sh1.57 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

















