Watu wengi wanapofikiria uwekezaji, mara nyingi huangalia biashara, viwanja au nyumba za kupangisha. Hata hivyo, kuna njia nyingine inayoweza kusaidia kujenga mali za muda mrefu na kuandaa maisha bora ya baadaye.
Bondi ni chombo cha uwekezaji, mwekezaji huikopesha Serikali au kampuni fedha kwa muda maalumu na kwa malipo ya riba ya mara kwa mara inayojulikana kama coupon.
Mwishoni mwa muda wa bondi, mwekezaji hurudishiwa mtaji wake wote. Hii ndiyo sababu bondi huonekana kuwa moja ya uwekezaji wenye utulivu kwa watu wanaopanga maisha ya muda mrefu.
Kwa mfano, mtu anaweza kuanza kwa kununua bondi ya Serikali au ya kampuni yenye thamani ya Sh50 milioni na yenye muda mrefu wa miaka 20 au 25. Bondi hiyo huanza kumlipa kuponi kila mwaka kulingana na masharti yake. Kilicho muhimu zaidi ni kwamba benki nyingi hukubali bondi kama dhamana ya mkopo. Mara nyingi benki zinaweza kutoa mkopo wa takribani asilimia 70 ya thamani ya bondi husika.
Hii ina maana kwamba, bondi ya Sh50 milioni inaweza kumwezesha mwekezaji kupata mkopo wa karibu Sh35 milioni.
Badala ya kutumia fedha hizo kwa matumizi ya kawaida kama kununua gari la kifahari au kufanya matumizi ya anasa, anaweza kutumia mkopo huo kununua bondi nyingine.
Bondi hiyo mpya nayo inaweza kutumika kama dhamana ya kupata mkopo mwingine wa kununua bondi nyingine tena. Kadiri mchakato huu unavyoendelea kwa nidhamu na umakini, thamani ya kitabu cha bondi kinaweza kukua kutoka Sh50 milioni za mwanzo na kufikia zaidi ya Sh150 milioni za uwekezaji.
Faida kubwa ya mkakati huu ni kwamba kuponi zinazotolewa na bondi hizo huendelea kuingia kila mwaka. Sehemu ya mapato hayo inaweza kutumika kusaidia kulipa mikopo iliyotumika kujenga kitabu hicho. Kadiri muda unavyopita, deni hupungua huku idadi ya bondi zinazomilikiwa ikiendelea kuongezeka.
Baada ya miaka kadhaa, kwa mfano miaka saba au minane, mwekezaji anaweza kujikuta amemaliza kulipa sehemu kubwa ya mikopo iliyotumika kujenga kitabu chake. Wakati huo, bondi nyingi hubaki kuwa mali zake na zinaendelea kumlipa kuponi kila mwaka.
Hii ni muhimu sana kwa mtu anayefikiria maisha ya baadaye. Tunapokuwa vijana tuna nguvu za kufanya kazi, kufanya biashara na kutafuta kipato. Lakini kadiri umri unavyoongezeka, uwezo wa kufanya kazi hupungua. Watu wengi huingia katika kipindi cha uzee bila kuwa na vyanzo vya mapato vinavyoendelea kufanya kazi kwa niaba yao.
Kwa kujenga kitabu cha bondi mapema, mtu anaweza kuwa amejiwekea msingi wa uhuru wa kifedha. Wakati nguvu za kufanya kazi zinapopungua, kuponi zinazotokana na bondi zinaendelea kuingia. Zaidi ya hapo, bondi hizo bado zina thamani kubwa ya mtaji ambayo inaweza kuuzwa au kutumika kama dhamana kwa mahitaji mengine muhimu.
Wengine wanaweza kusema hawana milioni 50 za kuanzia. Hata hivyo, jambo muhimu si kiasi unachoanza nacho bali kuanza mapema. Mtu anaweza kuanza na kiwango kidogo anachoweza kumudu na kuendelea kuongeza uwekezaji wake hatua kwa hatua.
Kinachojenga utajiri si ukubwa wa hatua ya kwanza, bali nidhamu ya kuendelea kujenga mali kwa muda mrefu.
Kwa hiyo, badala ya kufikiria tu jinsi ya kupata fedha za matumizi ya leo, fikiria jinsi ya kujenga mali zitakazolinda maisha yako ya kesho. Bondi inaweza kuwa mwanzo wa safari hiyo. Ukiwa na nidhamu na mtazamo wa muda mrefu, unaweza kujenga kitabu kikubwa cha uwekezaji itakayokupa amani ya kifedha hata wakati nguvu za kufanya kazi zitakapokuwa zimepungua.

















