Waziri Mkuu, mawaziri SMZ washusha presha ya ubaguzi

Dodoma/Zanzibar. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba na baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wametuliza presha kuhusu kauli za ubaguzi dhidi ya Wazanzibari na Watanganyika. Mjadala wa kurushiana vijembe vya tuhuma za ubaguzi uliibuka kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la…

admin Avatar

by

7 minutes

Read Time

Dodoma/Zanzibar. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba na baadhi ya mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wametuliza presha kuhusu kauli za ubaguzi dhidi ya Wazanzibari na Watanganyika.

Mjadala wa kurushiana vijembe vya tuhuma za ubaguzi uliibuka kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar baina ya wabunge na wawakilishi, hali iliyokemewa na baadhi yao kuwa inaweza kuhatarisha Muungano na mshikamano wa kitaifa.

Juni 6, 2026, akizungumza kwenye Baraza la Wawakilishi, Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum, alinukuliwa akihoji mwenendo wa watu wasiokuwa Wazanzibari kwenda kutibiwa visiwani humo kupitia Matibabu Kadi, ambayo ni maalumu kwa Wazanzibari pekee.

Alisisitiza kuwa bajeti ya Zanzibar ni Sh8 trilioni pekee, hivyo haiwezi kubeba gharama za matibabu kwa watu milioni 60.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil akizungumza wakato akihitimisha mjadala wa bajeti kuu ya Serikali barazani Chukwani Unguja Zanzibar.

Kauli hiyo iliibua mjadala mpana, hasa kwa wananchi wa Tanzania Bara walioipokea kama ya kibaguzi.

Vilevile, Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Hassan Hamis Hafidh maarufu kama Diaspora, wakati akichangia hotuba ya bajeti ya wizara yake, alisema Zanzibar ina hoteli 1,184 zilizosajiliwa, lakini wafanyakazi wengi katika hoteli hizo si wazawa.

Akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni jana, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu ni kama amezima moto wa wabunge kuhusu mivutano ya matibabu kwa pande mbili za Muungano, ambapo ametaka kuwepo na utulivu kwani hakuna jambo baya linaloweza kuwagawa.

Dk Mwigulu amekiri yapo mambo ya Muungano na yasiyokuwa ya Muungano, ikiwemo suala la afya, lakini akafafanua kuwa wizara mbili za afya zimekubaliana kupokea kadi za bima ya afya za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wa Tanzania Bara na Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) wa Zanzibar.

Alikuwa akijibu swali la mbunge wa Segerea (Chaumma), Agnesta Kaiza, aliyeuliza kuwa Tanzania ni Jamhuri ya Muungano, lakini yapo masuala yasiyo ya Muungano, ikiwemo afya, lakini hivi karibuni kumekuwepo na mijadala mikubwa kuhusu matibabu. “je, ni upi utaratibu wa kisera na kisheria unaotumika kuwahudumia Watanzania wa pande zote mbili kwenye maswala yasiyo ya Muungano?” amehoji mbunge huyo.

Katika majibu yake, Dk Mwigulu amesema: “Ni kweli nami nimesikia mjadala huu, na mbunge umelileta kwa wakati. Mpango uliopo ni kuwa kama utakuwa na kadi ya bima unaweza kutibiwa upande wowote wa Muungano, na kama huna, basi utatakiwa kulipa kwa fedha taslimu.”

Hata hivyo, amekiri wapo wageni kutoka nje ya Tanzania ambao wamekuwa wakijipenyeza na kupata vibali vya ukazi, wanaotumia fursa hiyo, na hao ndiyo wanasababisha kelele hizo. Amewataka Watanzania wazipuuze.

Dk Mwigulu amesema suala hilo lisitumike kuwagawa wananchi, bali kutangaza fursa na mema yaliyopo, kwani hata kero nyingi za Muungano zimefanyiwa kazi.

Wakati Dk Mwigulu akitoa ufafanuzi huo bungeni, ndani ya Baraza la Wawakilishi huko Zanzibar, baadhi ya wajumbe wa baraza hilo wamewataka wenzao kuacha kupotosha umma, wakisema Zanzibar ndiyo inanufaika zaidi katika Muungano ikilinganishwa na Tanganyika.

Hayo yameelezwa leo, Juni 18, 2026, wakati wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiendelea kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali huko Chukwani, Unguja, Zanzibar.

Akichangia mjadala huo, Mwakilishi wa Kwahani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mohammed Sijamini Mohammed, ameonya kuhusu kauli za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wawakilishi ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

“Kama kuna watu wanaonufaika ndani ya Muungano ni sisi Wazanzibari. Ifike hatua tuseme ukweli. Sisi sasa tunalalamika nini? Sisi tunyamaze, badala yake tutumie fursa hii kuwaelimisha watu wetu badala ya kupotosha,” amesema Sijamini.

Akitolea mfano namna Zanzibar inavyonufaika, amesema mashindano ya Soka ya Mataifa ya Afrika (AFCON) yanaandaliwa na mataifa matatu; Kenya, Uganda na Tanzania, lakini kwa kutaka kuweka usawa na Zanzibar, baadhi ya mechi zitachezwa visiwani humo.

Pia ametolea mfano wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ambaye kwa sasa yupo nchini Kenya kumwakilisha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akisema anayenufaika zaidi katika uwakilishi huo ni Zanzibar.

“Tumuogope Mungu, tuache kupotosha mambo tofauti na yalivyo,” amesema.

Mwakilishi wa Konde (CCM), ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Zawadi Amour Nassor, amesema hakuna ukweli kwamba ajira za Zanzibar zinatolewa kwa ubaguzi, isipokuwa hutolewa kulingana na vigezo na sifa.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza bungeni leo Alhamis Juni 18, 2026 wakati akijibu maswali ya wabunge.

“Hii kasumba kwamba watu wanachaguliwa au wanabaguliwa si kweli. Tuache kupotosha umma. Kinachozingatiwa ni sifa za watu na elimu zao. Kueleza hapa kwamba kuna ubaguzi katika ajira za Zanzibar si kweli, na tuwaeleze watu usahihi,” amesema.

Naye Mwakilishi nafasi za Rais ambaye pia ni Waziri wa Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Idrissa Kitwana Mustafa, amesema kama kuna watu wanafitinisha Muungano kwamba utavunjika, basi hauwezi kuvunjika, kwani Muungano sio wa kisiasa tu bali ni maisha ya watu.

Kuhusu upatikanaji wa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi ambavyo vinasimamiwa na wizara yake, Kitwana amesema suala hilo lipo wazi kikatiba.

“Katiba imeweka wazi kumtambua Mzanzibari ni nani, na iwapo mtu akiishi miaka 10 akiwa Zanzibar anaruhusiwa kupewa kitambulisho cha Zan ID, na ili awe Mzanzibari tayari anakuwa ni Mtanzania,” amesema.

Akihitimisha mjadala wa bajeti hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil, amesema kauli za Zanzibar kutonufaika ndani ya Muungano ni za kifitina, akitaka wanaosema hivyo kuacha.

Amesema Zanzibar ina kinga ya hadhi ya Tanzania katika kukopa, jambo ambalo linatokana na uimara wa Muungano.

“Tuna hadhi ya kinga ya mikopo chini ya Tanzania, amani na utulivu tulivyonavyo haipatikani kirahisi nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tuna uingiliano mkubwa kiuchumi, tunazaliana, na wasiwe wanatoa maneno ambayo yanaweza kuleta chuki ndani ya Jamhuri, tuyaache,” amesema.

Kuhusu Zanzibar kutojitegemea kibajeti, amesema jambo hilo si kweli, na ndio maana hata bajeti yake inaendelea kupunguza utegemezi kila mwaka hadi kufikia asilimia 2.8.

Amesema mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) asilimia 100 yanabaki Zanzibar, tofauti na ilivyozungumzwa kwamba fedha hizo zinachukuliwa.

“Kwa hiyo fitina hizi si nzuri, hasa tunapofanya kwa kuheshimiana. Ni vyema tukaacha kauli hizi,” amesema.

Naye Mwakilishi wa Amani, Masoud Amour Masoud (CCM), amesema kuna mafanikio makubwa ya Muungano kwani kuna ushirikiano na muingiliano mkubwa kati ya Zanzibar na Tanganyika, hivyo wanaoubeza wanataka kuleta chokochoko.

“Mimi nimekaa Kahama (Shinyanga), kule ukienda kwenye majaruba unakuta Wazanzibari watupu ndio wanauza mpunga, na ukiwaambia waje Zanzibar hawakubali, na wala hawabaguliwi. Kwa hiyo hizi kauli za kibaguzi hazifai, na sisi tutaendelea kuwa kitu kimoja,” amesema Masoud.

Amesema wataendelea kuulinda Muungano na hakuna atakayethubutu kuuvunja, na wanatakiwa waseme ukweli kuhusu manufaa ya Muungano badala ya kupotosha wananchi.

Akizungumza kuhusu kubaguliwa kwenye ajira na kupewa watu wengine, mwakilishi huyo amewataka wanaosema hivyo pia kuwa wa kweli.

Amesema changamoto ya Wazanzibari kutopata ajira kwenye sekta binafsi, hususan hotelini, inatokana na vijana wengi kubagua kazi hizo ambazo zinahitaji mabadiliko ya mitazamo na maadili ya kazi.

“Si kwamba watu wanabaguliwa, ajira zipo lakini hazichukuliwi na wenyewe. Badala yake tunakimbilia ajira za serikali.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiwa wamenyoosha mikono wakato wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali baada ya kuulizwa na Spika wa Baraza, Zuberi Maulid wanaounga mkono hoja kupitisha bajeti hiyo

“Hata mimi kwangu, mtu akisema binti yangu anavaa sketi fupi, ukimwambia aende hotelini anaona sio kazi inayofaa. Kwa hiyo watu wengine wanakuja kufanya kazi hizo. Niwaombe wajumbe wenzangu, tubadilike na kuwasaidia watu wetu, ajira zipo na watu hawabaguliwi,” amesema.

Hoja ya ajira pia imezungumziwa na Sijamini, ambaye amesema ajira si za vikosi vya SMZ tu, bali zipo nyingi mtaani ila watu hawazitaki.

“Tuwaelimishe vijana wetu, tutumie fursa hii kuwapa elimu na kubadilisha mitazamo yao kuhusu ajira. Zanzibar ina fursa nyingi za ajira, lakini watu wetu hawazitaki. Wajumbe tubadilike na kuwasaidia watu wetu katika hili,” amesema Sijamini.

Mwakilishi wa nafasi za Wanawake, Jabu Kame Juma (ACT Wazalendo), amesema licha ya Muungano kila nchi inatakiwa kuheshimu nyingine, lakini Zanzibar imekuwa ikinyanyaswa ndani ya Muungano.

“Zanzibar imekuwa koloni kwa muda mrefu ndani ya Muungano,” amesema na kuhoji kwa nini Zanzibar isiwe mjumbe katika mashirikisho ya mpira CAF na FIFA, akidai haki hizo zinabebwa na Tanganyika.

“Michezo sio Muungano, lakini kwa nini Zanzibar haijaingia FIFA na CAF, badala yake nafasi hizo zinatolewa…” amesema.

Kuhusu ajira, Jabu amesema: “Wanakuja watu wasiokuwa Wazanzibari wanachukua ajira za vijana wa Kizanzibari. Lazima tuwape kipaumbele na sio kuwapa watu ambao hawahusiki.”

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports