Morogoro. Serikali imeendelea kuweka mipango na mikakati ya kuwawezesha vijana kiuchumi ikiwa pamoja na kuwapa ujuzi wa kujiajiri na mitaji kwa ajili ya kuendeleza biashara kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka wakati akizindua Jukwaa la Vijana (Platform Campus Connect) katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) kampasi ya Mazimbu mkoani Morogoro.
Waziri Nanauka amesema baada ya Rais kutoa fedha kwa ajili ya mikopo kwa vijana, moja ya maagizo aliyopewa kama waziri mwenye dhamana na maendeleo ya vijana, ni kuboresha mazingira ya namna mikopo hiyo itakavyotokewa ili vijana wengi waweze kupata na kunufaika.
“Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi ndani ya siku 100 za kwanza baada ya kuingia madarakani atatoa Sh200 bilioni kwa ajili ya kuhakikisha vijana na wanawake wanawezeshwa kiuchumi kwa kuwapa mitaji hasa kwenye biashara changa na zile zinazokua,” amesema Nanauka.
Ameongeza: “Februari 2, 2026, Rais Samia alitekeleza ahadi yake hiyo na fedha hizo zilipelekwa kwenye sekta mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kunakuwa na uendelezaji wa uwezeshaji katika maeneo hayo.”
Amesema maboresho yaliyofanywa na wizara yamewezesha vijana kutoka katika makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, mtu mmoja mmoja, vikundi vya kijamii kupatiwa mikopo kwa masharti na riba nafuu
“Uzuri wa mikopo hii unaweza kuomba hata ukiwa bado mwanafunzi, ndiyo maana katika awamu ya kwanza wapo waliokuja na wazo la biashara na watapatiwa mkopo kuhakikisha wanaanza biashara hii ni kwa sababu Rais ametuagiza wizara turahisishe mchakato badala ya kupitia milolongo mingi, vijana wanaweza kuomba mkopo kwenye wizara moja kwa moja,” amesema Nanauka.
Hivyo, amewataka vijana kupitia majukwaa hayo yaliyoanzishwa kwenye mikoa mbalimbali nchini kuendelea kutafuta taarifa za msingi kuhusu fursa zinazopatikana ndani ya Serikali na pia kuchukua nafasi ya kufanya mambo yatakayowakwamua kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Japhar Kubecha amesisitiza umuhimu wa kutumia mikopo hiyo ili kujenga jamii na wao kupata ajira na maendeleo endelevu badala ya kukesha kwenye mitandao kwa kufuatilia vitu visivyokuwa na manufaa kwao wala Taifa.
Aidha, amewataka vijana kulitumia vema jukwaa hilo kwa kujifunza, kubadilishana uzoefu na kutambua fursa mbalimbali zinazoweza kuwa chachu ya maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla na kuwahimiza kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, ujasiriamali na ubunifu.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Sua anayeshughulikia Utawala, Fedha na Mipango, Profesa Amendus Mhairwa amesema vijana wanapaswa kupewa maarifa, ujuzi na mwelekeo sahihi wa kujiajiri.
“Lazima vijana wapewe maarifa ili wajitegemee badala ya kuishia kuhamasishwa kwa maneno pekee,” amesema Profesa Mhairwa.
Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Morogoro, Josephine Kapoma amesema bado kuna haja kwa Serikali kuendelea kuimarisha mifumo ya uwezeshaji kwa vijana ili wengi zaidi wapate mitaji na kunufaika na fursa zilizopo nchini.

















