Na Jackline Minja, Dodoma
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewahimiza wazazi na walezi kuimarisha malezi ya watoto wao na kutoa taarifa mapema kwa maafisa ustawi wa jamii pale wanapobaini changamoto zinazoweza kuhatarisha ustawi wa mtoto.
Mhe. Mahundi ametoa wito huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Martha Festo Mariki leo Juni 19, 2026 bungeni Dodoma, ambapo amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani nchini, ikiwemo kutoa elimu kwa wazazi na walezi, kuimarisha uchumi wa kaya na kuboresha huduma za ustawi wa jamii.
Amesema Serikali imeweka mkazo katika kuelimisha wazazi na walezi kuhusu wajibu wao wa kuwalea na kuwatunza watoto ili kuwazuia kukimbilia maisha ya mitaani.
“Serikali inaendelea kutoa elimu kwa walimu na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola mara mtoto anapopotea nyumbani au shuleni, hatua ambayo imekuwa ikisaidia kuzuia watoto wengi kuingia katika mazingira ya kuishi mitaani.” Amesema Mahundi
Katika hatua nyingine, Mhe. Mahundi amesema Serikali imeanzisha Madawati ya Huduma za Ustawi wa Jamii katika vituo vya usafirishaji nchini kwa lengo la kuwabaini na kuwasaidia watoto wanaotoroka majumbani kuelekea mitaani ambapo Madawati hayo yanasaidia kubaini watoto walio katika hatari na kuwaunganisha na familia zao kabla hawajaingia katika maisha mtaani aidha kuimarisha uchumi wa kaya ni sehemu muhimu ya suluhisho la changamoto hiyo, kwani umasikini ni miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya watoto kuondoka nyumbani.
Takwimu zinaonesha kuwa kati ya Julai 2025 na Februari 2026, jumla ya watoto 6,182 waliokolewa kutoka mitaani, huku watoto 5,663 kati yao wakiunganishwa tena na familia zao na wengine kupatiwa huduma mbalimbali kulingana na mahitaji yao.
Hata hivyo Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha tatizo la watoto wa mtaani linapungua na hatimaye kutokomezwa kabisa nchini.
















