Samia ataja kinachoichelewesha Afrika kukabili changamoto zake

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Afrika inayo nafasi ya kutatua changamoto zinazoikabili, iwapo mataifa yake yatashirikiana kama ilivyokuwa katika kipindi cha harakati za kudai uhuru. Aidha, Rais Samia amesisitiza kukuzwa kwa ushirikiano wa maeneo ya kimkakati kati ya Tanzania na Namibia, ikiwemo sekta ya mafuta na gesi, ili kujikinga na kujilinda na…

admin Avatar

by

4 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Afrika inayo nafasi ya kutatua changamoto zinazoikabili, iwapo mataifa yake yatashirikiana kama ilivyokuwa katika kipindi cha harakati za kudai uhuru.

Aidha, Rais Samia amesisitiza kukuzwa kwa ushirikiano wa maeneo ya kimkakati kati ya Tanzania na Namibia, ikiwemo sekta ya mafuta na gesi, ili kujikinga na kujilinda na changamoto zinazotokana na mwenendo wa mabadiliko ya uchumi wa dunia.

Mataifa hayo, yamesaini hati nne za makubaliano ya ushirikiano katika sekta za biashara ulinzi na ukuzaji wa miji ya Zanzibar kwa upande wa Tanzania na Swakopmund nchini Namibia.

Rais Samia ameyasema hayo leo, Jumamosi Juni 20, 2026 alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kikao chake na Rais wa Namibia, Netumbo Ndaitwah aliyepo nchini kwa ziara ya kiserikali.

“Licha ya changamoto zilizopo, Bara la Afrika lina utajiri na fursa nyingi ikiwemo nguvukazi kubwa ya vijana, utajiri wa rasilimali za maliasili pamoja na ardhi yenye rutuba.

“Endapo nchi za Afrika zitashirikiana ipasavyo, kama tulivyofanya katika harakati za ukombozi, tutaweza kutatua changamoto nyingi zinazotukabili na kuleta maendeleo yetu bila woga, bila vikwazo, bila hofu,” amesema.

Amewataka watendaji wa nchi zote kuhakikisha masuala waliyojadili na kukubaliana yatekelezwe kwa wakati ili kuchagiza ustawi wa nchi zote.

Sambamba na hayo, Rais Samia amesema Tanzania imedhamiria kuuenzi uhusiano wake na Namibia, ulioanza tangu enzi za harakati za ukombozi.

Amesema Rais Ndaitwah ana historia ndefu na Tanzania kwa kuwa aliishi Magomeni jijini Dar es Salaam, wakati wa harakati za kupambania uhuru wa Taifa lake.

Licha ya uhusiano mzuri wa Tanzania na Namibia, Rais Samia amesema bado kuna ushirikiano mdogo wa kiuchumi baina ya mataifa hayo.

Mwaka 2024, amesema biashara kati ya mataifa hayo ilikuwa na thamani ya Sh20 bilioni, ndiyo maana katika mazungumzo yao wamekubaliana kukuza ushirikiano wa kiuchumi na maeneo mengine ya kimkakati.

“Tumekubaliana kukuza ushirikiano wa maeneo mengine ya kimkakati kama vile usalama wa chakula, uchumi wa buluu na upande wa madini, mafuta na gesi,” amesema.

Ameeleza matumaini yake ni kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo hasa baada ya ziara ya Rais Ndaitwah nchini.

Ametaja eneo la uchumi wa buluu kuwa miongoni mwa waliyozungumza, hasa ukizingatia nchi zote zina bahari ambazo zikitumika ipasavyo zitayanufaisha mataifa hayo.

Katika mafuta na gesi, amesema wamekubaliana kushirikiana kwani mataifa yote yana utajiri wa rasilimali hizo na zikitumika vema zitasaidia kubadili uchumi wa nchi hizo.

“Kwa kuzingatia mwenendo wa mabadiliko ya kiuchumi duniani, tumeona kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina yetu ili kujikinga kujilinda na kuhimili changamoto hizo, pia kunufaika na rasilimali hizo tulizobarikiwa kuwa nazo,” amesema.

Katika eneo la ufugaji na mifugo, amesema wamekubaliana kukamilisha hati za makubaliano zitakazoweka msingi wa uhusiano kwenye maeneo hayo.

Pia, amesema wamekubaliana kushirikiana katika sekta ya anga kwa kuanzisha safari za ndege kutoka Tanzania hadi Namibia, kuwezesha usafiri na kukluza utalii.

Rais Samia, amesema wamekubaliana lugha ya Kiswahili kufundishwa katika taasisi za elimu ya juu za nchini Namibia.

Katika mazungumzo yao, amesema amemwomba Rais huyo wa Namibia, kuiunga mkono Tanzania katika harakati za kugombea nafasi za ujumbe wa muda katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029/30.

Pia, amesema ameomba kuungwa mkono kwa wagombea wa Tanzania katika nafasi mbalimbali za kimataiga na kikanda.

Kwa upande wake Rais Ndaitwa, amesema Tanzania inapaswa kujivunia kwa juhudi ilizozifanya katika uhuru wa Namibia.

Rais wa Namibia, DkNetumbo Nandi-Ndaitwah wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Juni 20, 2026 Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

Amesema ni muhimu kwa mataifa hayo mawili, kuendeleza ushirikiano wa kisiasa kuwa wa kiuchumi na kujenga ustawi wa wananchi wa pande zote.

“Dhamira ya ziara yangu ni kubadili uhusiano wa muda mrefu wa kisiasa, kuwa wa kiuchumi na ulimwengu tuliopo sasa unataka hilo,” amesema.

Ili kutimiza hayo, amesema makubaliano yaliyofikiwa ni muhimu yakafanyiwa kazi, hasa kuondoa vikwazo vya biashara kati ya nchi zote.

Katika hafla hiyo, mikataba minne ilisainiwa, ikiwemo hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Namibia.

Pia, imesainiwa hati ya makubaliano ya ushirikiano katika maendeleo ya biashara ndogo na za kati kati ya Serikali ya Tanzania na Namibia.

Hati nyingine ya makubaliano iliyosainiwa ni kuhusu ushirikiano katika sekta ya ulinzi kati ya Tanzania na Namibia na mkataba wa ushirikiano wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar na Manispaa ya Swakopmund nchini Namibia.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports