Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amewataka viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla kushirikiana katika kuendeleza miradi yenye manufaa kwa jamii akisisitiza kuwa maendeleo hayachagui chama cha siasa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mahafali ya wahitimu wa mafunzo ya ufundi chuo cha VETA Furahika yaliyofadhiliwa na Mbunge wa Ukonga, Bakari Shingo (ACT) Ameir alisema juhudi zinazolenga kuwapatia vijana elimu na stadi za kazi zinapaswa kuungwa mkono na wadau wote bila kuangalia tofauti za kisiasa.
Alimpongeza Mbunge huyo kwa kufadhili mafunzo ya ufundi kwa vijana wa Ukonga na kueleza kuwa hatua hiyo inatekeleza dhamira ya Serikali ya kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Ameir alisema Serikali kupitia Wizara ya Elimu inaendelea kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya stadi ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, huku akizitaka taasisi za mafunzo kushirikiana na sekta binafsi ili wahitimu wapate uzoefu wa kazi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Aidha, alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Utambuzi na Urasimishaji wa Ujuzi inayosimamiwa na VETA, inayowezesha vijana waliopata ujuzi kupitia uzoefu wa kazi au mafunzo yasiyo rasmi kutambuliwa na kupata vyeti vinavyotambulika rasmi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ukonga, Bakari Shingo, alisema mpango wa kufadhili mafunzo ya ufundi kwa vijana unalenga kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira na kuwawezesha wananchi kujitegemea kupitia ujuzi wa kazi mbalimbali.
Naye Mbunge wa Segerea,(CHAUMA) Agnesta kaiza, alimpongeza Naibu Waziri kwa kuonesha mfano wa ushirikiano wa kisiasa katika kuwatumikia wananchi na kuahidi kuhamasisha vijana wa jimbo lake kutumia fursa za mafunzo ya ufundi zinazotolewa katika eneo hilo.
Awali, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala Charangwa Selemani alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kupitia ujenzi wa shule, madarasa na utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo, hatua ambazo zimeongeza fursa za elimu kwa wananchi wengi zaidi.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi wa serikali, vyama vya siasa, taasisi za elimu, wazazi na mamia ya wahitimu waliomaliza mafunzo ya ufundi katika fani mbalimbali kwa lengo la kujiajiri na kuchangia maendeleo ya taifa.
Pia kupitia mahafali hayo, Charangwa alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Ilala ikiwemo ya elimu na ujenzi wa majengo ya ghorofa Kwa Sekondari 12 na mawili kwa Shule za Msingi.
Naye Mkuu wa Chuo hicho,Dk David Msuya alisema mchakato wa Mbunge Shingo, kupeleka wanafunzi 200 katika Chuoni hapo ni wa kupongeza na kugwa na viongozi wengine
Pia aliongeza wataendelea kupokea wanafunzi kwaajili ya muhula mpya na kutoa wito kwa wazazi na walezi kupeleka vijana wao ili wapate ujuzi utakaowafaa maishani.














