Mbarali yatarajia kuvuna tani 430,452 za mpunga, masoko yatajwa

Mbarali. Kufuatia uwekezaji wa Serikali katika kuboresha miundombinu ya sekta ya kilimo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, inatarajia kuzalisha tani 430,452 za mpunga katika msimu wa kilimo wa 2025/2026. Takwimu hizo zinaonyesha ongezeko la uzalishaji wa tani 111,168 ikilinganishwa na tani 319,284 zilizozalishwa msimu wa kilimo wa 2024/2025. Katika msimu uliopita, halmashauri hiyo…

admin Avatar

by

3 minutes

Read Time

Mbarali. Kufuatia uwekezaji wa Serikali katika kuboresha miundombinu ya sekta ya kilimo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, inatarajia kuzalisha tani 430,452 za mpunga katika msimu wa kilimo wa 2025/2026.

Takwimu hizo zinaonyesha ongezeko la uzalishaji wa tani 111,168 ikilinganishwa na tani 319,284 zilizozalishwa msimu wa kilimo wa 2024/2025.

Katika msimu uliopita, halmashauri hiyo ilikusanya zaidi ya Sh11 bilioni, mapato ya ndani kutokana na zao hilo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Mei 27, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli, alipokuwa akizungumza na Mwananchi ofisini kwake kuhusu mchango wa zao la mpunga katika mapato ya Serikali.

Mweli amesema zao la mpunga linachangia takribani asilimia 78 ya mapato ya halmashauri, fedha ambazo hutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.

“Sababu zinazochangia kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la mpunga ni mikakati ya halmashauri kutoa mikopo ya asilimia 10, kuwajengea uwezo wakulima kutumia teknolojia za kisasa na kuimarisha huduma za ugani,” amesema.

Amesema sababu nyingine ni uwekezaji wa Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika ujenzi wa zaidi ya skimu 100 za umwagiliaji kwenye maeneo yanayozalisha zao hilo jambo  ambalo  limepelekea wakulima kulima kwa uhakika mwaka mzima.

“Lakini ili kufikia malengo tuliyojiwekea, tunaendelea kugharamia mafunzo kwa wakulima kuhusu teknolojia za kilimo bora kupitia mashamba darasa, pamoja na kuwawezesha kupata mikopo ya pembejeo kwa masharti nafuu,” amesema Mweli.

Mchango wa kilimo cha mpunga.

Mweli amesema katika msimu uliopita halmashauri ilikusanya zaidi ya Sh11 bilioni kutokana na zao la mpunga, sawa na asilimia 78 ya mapato ya ndani yaliyotumika kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Mikakati yetu ni kuendelea kuwekeza katika zao hilo ili kuongeza mchango wake kwenye mapato ya halmashauri, sambamba na kuhakikisha wakulima wanatumia mbegu bora na kupata masoko ya uhakika,” amesema.

Ameongeza kuwa halmashauri inaendelea kusajili wakulima ili wanufaike na mbolea za ruzuku pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa mawakala wa pembejeo vijijini.

Mweli amesema katika kuongeza tija ya uzalishaji halmashauri inashirikiana na taasisi za utafiti kuwafundisha wakulima mbinu za kukabiliana na magonjwa ya mimea na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Wataalamu wanaendelea kutoa elimu kuhusu mbinu za kilimo zinazotumia maji kidogo, mbegu chache, lakini zenye tija kubwa, maarufu kama kilimo shadidi. Pia tunaimarisha usimamizi wa skimu za umwagiliaji kupitia sheria ndogo na katiba za watumiaji wa maji,” amesema.

Amesema lengo ni kuwawezesha wakulima kutumia mbinu bora za uzalishaji na mbegu zinazostahimili magonjwa pamoja na mabadiliko ya tabianchi.

Mweli amesema dira ya halmashauri kuhakikisha wakulima wanapata fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kuvutia uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa zao la mpunga.

“Mbarali ni miongoni mwa halmashauri zinazofanya vizuri katika uzalishaji wa mpunga nchini. Kupitia mikakati hii, tutahakikisha tunazalisha mpunga wenye ubora na ushindani katika soko la kimataifa,” amesema.

Ameongeza kuwa wakulima wataendelea kuunganishwa na wanunuzi wakubwa na taasisi mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa vibali na taratibu za kuuza mazao katika masoko ya nje ya nchi.

Mkulima wa mpunga kutoka Kijiji cha Madibira, Amos Thomas, amesema maboresho ya miundombinu ya umwagiliaji yameongeza hamasa ya wakulima kuzalisha kwa tija.

“Kilimo cha umwagiliaji kimekuwa mkombozi mkubwa. Sasa tunatumia teknolojia za kisasa kuanzia maandalizi ya mashamba hadi uvunaji,lakini pia halmashauri  inatusaidia kupata mikopo na kutuunganisha na taasisi za kifedha,” amesema.

Naye Anna Sanga amesema uwekezaji wa Serikali katika sekta ya kilimo umewapa matumaini makubwa wakulima, hasa kupitia upatikanaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakati.

“Miaka ya nyuma Mbarali ilikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji, hali iliyochochea migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Baada ya uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji, changamoto hiyo imepungua kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Pia,  ameomba Serikali kupitia Wakala wa Vipimo (WMA),kufanya ufuatiliaji wakati wa mavuno ili kudhibiti wanunuzi wanao tumia  mizani zisizo na ubora na kuibia wakulima.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports