Geita. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi amewataka wazazi na walezi nchini kuiga mfano wa malezi bora ya marehemu Sussana Ngolo kwa kuhakikisha wanalea watoto wenye maadili na uwezo wa kulitumikia taifa.
Dk Nchimbi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Mei 29, 2026 alipomwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Mama Sussana, mama mzazi wa Hayati Dk John Magufuli, yaliyofanyika nyumbani kwa marehemu wilayani Chato mkoani Geita.
Amesema Mama Sussana, licha ya kutokuwa katika familia ya kisiasa, alitimiza wajibu wake wa malezi na hivyo kusaidia taifa kupata kiongozi mahiri na mchapakazi.
“Wazazi wana wajibu wa kulea watoto kwa kuwaandaa kulitumikia taifa. Kufanya mema kwa binadamu mwenzako siyo lazima yalipwe kwako,” amesema.
Dk Nchimbi amesema kutokana na malezi hayo, Hayati Rais Magufuli aliendeleza fikra za kulea na kuandaa viongozi wengine, akitolea mfano msaada wake wakati wa mabadiliko yake ya kisiasa akiwa Jimbo la Njombe Mjini.
Amesema pia kuwa baada ya kutangaza kusitisha siasa kwa muda, alipokea simu kutoka kwa viongozi mbalimbali akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira na baadaye Hayati Dk Magufuli, waliomshauri kubadili uamuzi huo na kuendelea kulitumikia taifa.
Katika maelezo yake, Dk Nchimbi amesema Magufuli alimpa moyo na kumtaka asiharakishe kujiondoa kwenye siasa, akimweleza kuwa bado ana nafasi kubwa ya kulitumikia taifa, hatua iliyofuata baadaye kwa kuteuliwa kwake kuwa Balozi nchini Brazil.
Amesema kiongozi huyo alikuwa akipenda mijadala yenye hoja na si uhasama, akibainisha kuwa tofauti za mawazo kati yao hazikuwa uadui bali sehemu ya ujenzi wa fikra.
Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda, Mhashamu Simon Masondole, amesema jamii inapaswa kuenzi maisha ya Mama Sussana kwa kuendeleza malezi bora na kudumisha umoja wa kitaifa.
Akitoa shukrani kwa niaba ya familia, Simon Michael ameishukuru Serikali, wahudumu wa afya na wananchi kwa kuwa pamoja na familia katika kipindi chote cha ugonjwa na msiba.
Mama Sussana Mussa alifariki Mei 25, 2026 kutokana na matatizo ya moyo, kisukari na shinikizo la damu

















