IRINGA: Katika kuenzi mchango wa walipakodi ambao wamekuwa uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa kwa miongo mitatu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa itahadhimisha wiki ya mlipa kodi kwa kutoa elimu na shukrani kwa walipakodi.
Wiki hiyo itafanyika kati ya Juni 22 na 27, 2026, sambamba na maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo kwa kuhusisha shughuli mbalimbali za kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Maigloria Saria amesema shughuli hizo ni pamoja na utoaji wa elimu ya kodi, mikutano ya wadau, ziara za kuwashukuru walipakodi na kampeni za kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari.
Amesema shughuli zote hizo ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Mlipakodi kwa mwaka wa kodi 2024/2025.
Maadhimisho hayo yamebeba ujumbe wa kutambua mchango wa walipakodi katika kuijenga Tanzania kupitia mapato ya ndani yanayowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii.
Amesema katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa TRA mwaka 1996, mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato, kuongeza wigo wa walipakodi na kuboresha huduma kwa kutumia teknolojia, hatua ambazo zimechangia kuongezeka kwa mapato ya serikali na kuimarika kwa uchumi wa taifa.
“Tunapotimiza miaka 30 ya TRA, tunatambua kuwa mafanikio yote yaliyopatikana yametokana na ushirikiano mkubwa wa walipakodi. Wiki hii itakuwa fursa ya kuwashukuru, kuwasikiliza na kuendelea kuwajengea uelewa kuhusu wajibu wao wa kikodi,” alisema Saria.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, maadhimisho yataanza Juni 22 kwa zoezi la upandaji miti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, litakaloongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta.
Shughuli hiyo inalenga kuonesha mshikamano wa TRA na jamii katika kulinda mazingira na kuunga mkono juhudi za taifa za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Juni 23, TRA itaandaa jukwaa maalumu la wadau litakalowakutanisha wafanyabiashara, washauri wa kodi, viongozi wa dini, machifu na makundi mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kujadili masuala ya kodi, kupokea maoni ya wananchi na kuibua mapendekezo yatakayosaidia kuboresha huduma za mamlaka hiyo.
Saria amesema jukwaa hilo litatoa nafasi kwa wadau kueleza changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu ya kikodi na kujadiliana namna bora ya kuimarisha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari.
Katika hatua nyingine, Juni 24 na 26 maofisa wa TRA watafanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa kwa lengo la kuwashukuru walipakodi mmoja mmoja na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara kwa mchango wao katika maendeleo ya taifa kupitia kodi wanazolipa.
“Tunataka walipakodi wajione kuwa ni sehemu muhimu ya maendeleo ya nchi. Ndiyo maana tutawafuata walipo ili kuwashukuru na kuendelea kuwapatia elimu ya kodi,” alisema.
Mbali na shughuli za elimu na uhamasishaji, TRA pia itatekeleza jukumu lake la kijamii kwa kutembelea wodi za wanawake na watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa Juni 25, ambapo itatoa msaada na faraja kwa wagonjwa pamoja na wahudumu wa afya.
Siku hiyo pia anatarajiwa kushiriki kipindi maalumu cha redio kitakacholenga kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kodi katika maendeleo ya taifa na kutoa shukrani kwa walipakodi.
Maadhimisho hayo yanayotarajiwa kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Fedha wa TRA yatahitimishwa Juni 27 kwa matembezi ya hisani (Fun Walk) na msafara wa uelimishaji kwa umma (Roadshow) utakaozunguka maeneo mbalimbali ya mji wa Iringa ukihusisha watumishi wa TRA, wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele hicho cha maadhimisho ya mkoa.















