DAR ES SALAAM: WANAWAKE wajasiriamali wameendelea kupatiwa nyenzo muhimu za kuwawezesha kukuza biashara zao na kuimarisha ustawi wao kupitia mafunzo mbalimbali nchini.
Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa kushirikiana na Benki ya ABSA wametoa mafunzo maalumu kwa wanawake hao yatakayowapa mustakabali bora wa biashara zao.
Mafunzo hayo yamewaleta pamoja wanawake kutoka sekta mbalimbali ikiwemo biashara, viwanda vidogo, madini, utalii, sekta za ubunifu na wakandarasi, wakiwakilisha wanachama wa TPSF.

Katika mafunzo hayo, wataalamu wa ABSA walitoa elimu kuhusu usimamizi wa fedha ikijumuisha masuala ya bajeti, akiba na uwekezaji kwa ajili ya kukuza biashara za wajasiriamali, hatua inayowasaidia wanawake kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kiuchumi.
Pia wataalamu kutoka TRA walitoa elimu kuhusu utii wa kodi (tax compliance) kwa SMEs, wakisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za kodi katika uendeshaji wa biashara ili kujenga biashara imara na endelevu.
Kwa upande wa uwekezaji, Global Alpha Capital walitoa mada kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji na namna wajasiriamali wanavyoweza kunufaika na masoko ya mitaji, jambo linalofungua nafasi zaidi za ukuaji wa biashara zinazomilikiwa na wanawake.
Mwisho, sekta ya bima ilihusika ambapo Jubilee Insurance walieleza kuhusu bima ya maisha, huku Britam Insurance wakifundisha kuhusu bima ya afya kama nguzo muhimu ya usalama wa biashara na familia.
TPSF imesisitiza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia maarifa, mitandao na fursa za kifedha, hatua inayotarajiwa kuongeza mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii na uchumi wa taifa kwa ujumla.















