Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezindua rasmi awamu ya pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, ijulikanayo kama “Mama Samia Legal Aid Campaign” katika Viwanja vya Dole Kizimbani, Zanzibar tarehe 20 Juni, 2026.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Dkt. Mwinyi amesema kuwa kufanyika kwa kampeni hiyo ni mojawapo ya jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za sheria na upatikanaji wa haki kwa wananchi.
*“Kampeni hii imekuwa ni chachu kubwa katika kuhakikisha wananchi hususan wasiokuwa na uwezo wanaifikia haki kwa wakati na kwa ufanisi.* Amesema Mhe. Dkt. Mwinyi .
Aidha, amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mifumo mbalimbali ya kisheria ikiwemo kutungwa kwa Sheria ya Msaada wa Kisheria Sura ya 21 ya Tanzania na Sheria ya Msaada wa Kisheria ya Mwaka 2018 ya Zanzibar kwa lengo la kuboresha huduma mbalimbali za Sheria.
*“Kupitia Sheria hizi Serikali inaendelea kuweka na kutekeleza mikakati na mipango madhubuti ya kuhakikisha wananchi wanaifikia haki kwa wakati na kwa usawa.”* Amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera amesema kuwa Serikali itendelea kuboresha miundombinu ya upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi, kupitia ujenzi wa majengo ya Taasisi mbalimbali za kisheria ikiwemo ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali unaoendelea Mtumba, Jijini Dodoma.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari ameshiriki katika Uzinduzi wa awamu ya pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, ambapo pia alipata fursa ya kutembelea mabanda ya Taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za Kisheria katika Kampeni hiyo, ikiwemo Banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inashiriki katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, na itaendelea kutoa huduma za elimu na ushauri wa kisheria pamoja na utatuzi wa migogoro mbalimbali kwa Wananchi wa Zanzibar kuanzia tarehe 20 Juni hadi tarehe 5 Julai, 2026.












