IRINGA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wanasiasa wanaohamia kwenye chama hicho kutoka upinzani kutolalamika wanapokosa vyeo.
Kimesisitiza kuwa nafasi za uongozi ndani ya chama hupatikana kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sifa zilizowekwa, kwani chama hicho ni cha kila Mtanzania.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi alisema hayo Juni 20,2026 alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa mkoani Iringa.

Akizungumza na hadhara hiyo Kihongosi alisema kujiunga na CCM ni uamuzi wa kisiasa unaopaswa kuongozwa na imani ya kutumikia wananchi na chama, badala ya matarajio ya kupata natasi za uongozi mara moja.
Aidha, aliwahimiza wanachama wapya kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama na kuheshimu utaratibu uliopo wa kupata viongozi na si kutaka uongozi kwa lazima na kwa kuwekea chama masharti.
“Chama hiki ni kikubwa kinachukua watu wa kila aina wenye elimu na wasio na elimu ni chama cha kila Mtanzania ukija CCM ukataka cheo ukakosa usinung’unike na unakuja na masharti magumu kwamba msiponipa narudi kule sisi hatutishwi,”aliongeza Kihongosi.

Aliongeza: “Wewe ukitaka kwenda nenda tutakuwepo na tukutane demokrasia iamue, na watu wa Iringa wanaakili na hawadanganyiki sio kichwa cha mwendawazimu kwamba kufanyia mchezo”.













