Dar es Salaam. Katika uhusiano, si kila jambo la kweli linapaswa kusemwa kwa namna yoyote au wakati wowote.
Wataalamu wa uhusiano wanaeleza kuwa mafanikio ya uhusiano hayategemei tu ukweli unaosemwa, bali pia namna ukweli huo unavyowasilishwa.
Mara nyingi wanaume hujikuta wakiharibu hali ya uhusiano wao bila kukusudia kutokana na kauli wanazoziona za kawaida, lakini zikawa na athari kubwa kwa wenza wao.
Wanawake wengi huweka uzito mkubwa katika mawasiliano na maneno wanayoyasikia kutoka kwa wapenzi wao. Kauli moja inaweza kujenga kujiamini, kuimarisha upendo na kuongeza ukaribu, lakini pia kauli nyingine inaweza kuibua mashaka, huzuni, hasira au kupunguza imani ndani ya uhusiano.
Kutokana na hali hiyo, kuna baadhi ya maneno ambayo mwanaume anapaswa kuyatumia kwa umakini mkubwa ili kulinda afya ya uhusiano wake.
Miongoni mwa kauli zinazoweza kuleta taharuki ni zile zinazomhusisha rafiki wa karibu wa mpenzi wako. Kwa mfano, kumwambia mpenzi wako kuwa rafiki yake ni mzuri sana, anavutia au ana umbo zuri kunaweza kumfanya aanze kujenga mashaka ambayo awali hayakuwepo. Hata kama unalizungumza jambo hilo kwa nia ya kawaida, mpenzi wako anaweza kutafsiri kuwa unavutiwa na rafiki yake.
Matokeo yake ni kuibuka kwa hali ya kutokuwa na amani kila anapokuona ukiwa karibu na mtu huyo au hata kuanza kuhoji uaminifu wako.
Kauli nyingine inayoweza kuibua hisia hasi ni ile inayohusu mwonekano wa mwili wake. Kumwambia mwanamke kwamba anatakiwa kupunguza uzito au aanze kula chakula kidogo kunaweza kuonekana kama ushauri wa kawaida, lakini mara nyingi huumiza zaidi kuliko kusaidia.
Wanawake wengi tayari huwa wanajitathmini kuhusu miili yao na wakati mwingine hujihisi kutoridhika na baadhi ya maeneo ya mwonekano wao. Kauli kali kuhusu mwili wake inaweza kuathiri kujiamini kwake na hata kumfanya ahisi kuwa humkubali alivyo.
Kadhalika, kauli zinazohusu kutopenda ndoa huwa na uzito mkubwa kwa wanawake wengi walio katika uhusiano wa muda mrefu. Mwanamke anayejenga matumaini ya maisha ya baadaye na mpenzi wake anapomsikia mwanaume akisema hapendi kuoa au hafikirii kuingia kwenye ndoa, anaweza kuanza kujiuliza nafasi yake ndani ya uhusiano huo.
Wakati mwingine hujiuliza kama anapotezewa muda au kama mpenzi wake hana mipango ya baadaye pamoja naye. Hali hii inaweza kusababisha sintofahamu na kuanza kudhoofisha msingi wa uhusiano.
Vilevile, hakuna mwanamke anayependa kulinganishwa na mpenzi wa zamani wa mwanaume wake. Kauli kama “mpenzi wangu wa zamani alikuwa anafanya hivi” au “alikuwa tofauti na wewe” mara nyingi huibua hisia za kutotosha.
Hata kama lengo si kumdhalilisha, mwanamke anaweza kuhisi kuwa bado unamkumbuka au unaendelea kumthamini mtu huyo kuliko yeye. Kadri marejeo hayo yanavyoongezeka, ndivyo wivu na mashaka yanavyoweza kuongezeka ndani ya uhusiano.
Katika maisha ya kila siku, wanawake wengi hupenda kutumia muda na wenza wao. Hivyo, kauli ya kumwambia “nadhani tusiende pamoja” au “sina haja ya kwenda na wewe” bila maelezo ya kutosha inaweza kutafsiriwa vibaya. Anaweza kuhisi hujivunii kuwa naye hadharani, unamficha au unaona uwepo wake ni mzigo. Hata kama sababu zako ni za msingi, namna ya kuwasilisha ujumbe huo ndiyo inayofanya tofauti kubwa.
Pia kuna mambo ya kawaida ya kibinadamu ambayo yanahitaji busara kuyazungumzia. Kumcheka au kumkejeli mpenzi wako kutokana na harufu mbaya iliyotokea kwa bahati mbaya kunaweza kumuacha na aibu kubwa.
Ingawa huenda jambo hilo likaonekana la kawaida kwako, kwake linaweza kuwa chanzo cha fedheha na kumfanya ajisikie vibaya kwa muda mrefu.
Wanaume wengi pia hupenda kulalamika kwamba wanawake wanaongea sana. Kauli kama “wewe mbona unapenda kuongea kila mara?” inaweza kuonekana nyepesi, lakini mara nyingi huumiza.
Kwa wanawake wengi, mazungumzo ni njia ya kuonyesha ukaribu, kueleza hisia na kujenga uhusiano. Badala ya kukatisha mazungumzo kwa maneno makali, ni bora kueleza kwa utulivu kuwa kwa wakati huo huwezi kuzungumza na ungependa kufanya hivyo baadaye.
Sababu nyingine inayochangia migogoro ni matumizi ya neno “niko bize sana” kila wakati. Ni kweli kwamba kazi ni muhimu, lakini kutumia shughuli kama kisingizio cha kukwepa mawasiliano kunatuma ujumbe kwamba uhusiano hauna kipaumbele.
Mwanamke anayekupenda anatarajia kuona jitihada za kutenga muda kwa ajili yake, hata kama ni dakika chache za mawasiliano kwa siku.
Aidha, wanaume wengi hufanya kosa la kulinganisha mapishi ya wapenzi wao na yale ya mama zao. Kauli kama “nakikumbuka sana chakula cha mama yangu” au “mama yangu anajua kupika sana” inaweza kuonekana ya kawaida, lakini kwa mwanamke anayejitahidi kukuhudumia inaweza kuibua hisia za kushindwa au kutothaminiwa. Wakati mwingine kauli hizo hujenga ushindani usio wa lazima kati ya mpenzi na mama wa mwanaume.
Kwa ujumla, mafanikio ya uhusiano hayajengwi na zawadi pekee au matumizi makubwa ya fedha, bali pia na namna wenzi wanavyowasiliana kila siku. Maneno yana uwezo wa kujenga au kubomoa. Kabla ya kusema jambo lolote, ni muhimu kufikiria namna litakavyopokelewa na mtu unayempenda.

















