Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikitoa tathimini ya uhabirifu wa mali kipindi walichofungiwa kujishughulisha na siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imetonesha kidonda kwa kukilima barua nyingine.
Mbali na hayo, chama hicho kimeeleza utaratibu utakaofuatwa kwa waliokuwa wanachama wanaotaka kurejea, na hasa wale waliotishia uhai wa chama.
Juni 10, 2025 Mahakama Kuu ilitoa uamuzi wa kuzuia Chadema kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali zake kutokana na kesi ya mgawanyo wa mali iliyokuwa imefunguliwa na makada wake watatu wa upande wa Zanzibar.
Kesi hiyo ilifunguliwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake Zanzibar, Said Issa Mohamed, Anna Maulida Komu (marehemu) na Ahmed Rashid Khamis, wakilalamikia mgawanyo usio sawa wa mali za chama hicho kati ya Zanzibar na Bara.
Aprili 15, mwaka huu chama hicho kilishinda rufaa na kuruhusiwa ya kuendelea kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali zake baada ya siku 309 na baadaye Mei 28, kesi hiyo ikafutwa kabisa.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche amesema hali ya mali za chama hicho zilizokuwa hazitumiki kwa muda huo walizikuta katika hali mbaya.
Amesema wamekuta uharibifu mkubwa na sasa wanafanya tathmini kujua kiwango cha hasara ambazo watakiweka hadharani.
“Kuna uharibifu mkubwa. Usipotumia kitu kwa muda mrefu, kwa mfano nyumba inapata shida kubwa sana. Ofisini makao makuu pale kumekuwa na shida ya mifumo ya majitaka imeharibika,” amesema.
Amesema hata magari yameharibika hasa wilayani na ndiyo maana kwa sasa wanakusanya taarifa kujua kiwango cha athari na ripoti itatolewa rasmi.
Mbali na hasara hizo zinazolipika, Heche amesema zipo ambazo hazilipiki ikiwemo kuwanyima wanachama haki za kufanya siasa kwa kwa kipindi chote walichozuiwa kwa amri ya mahakama.
“Chama kinafanya kazi za kushawishi watu kujiunga nacho, sasa kwa siku zote hizo tumezuiwa kushawishi kuongeza wanachama wapya, unailipaje hiyo,” amehoji.
Heche amesema kwa yote hayo wanaelekeza lawama zao kwa jaji aliyewanyima nafasi ya kusilikizwa na kwamba “inaonyesha kulikuwa na makusudi katika hilo.”
“Siku ambayo mwenyekiti wetu (Tundu Lissu) alikamatwa ni siku hiyo hiyo ndio kesi ilifunguliwa. Lakini, mapema baada ya kesi kufunguliwa, Ofisi ya Msajili ilisema haiwatambui viongozi wetu waliopitishwa na baraza kuu,” amedai Heche.
“Kwa hiyo inaonyesha kila kitu kilipangwa na havikuwa vitu vya bahati mbaya, vilipangwa kukishambulia chama chetu,” amesema Heche.
Hata hivyo, ameeleza kufurahishwa na molari ya wananchi kwa chama hicho hasa baada ya kufunguliwa, kwani mikutano yake imepata uungwaji mkono.
Katikati ya hali hiyo, juzi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetonesha kidonda baada ya kukiandikia barua ya pili ndani ya mwezi mmoja akikitaka kijieleze kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria, ikiwemo kusimamishwa usajili wake au kutozwa faini kwa madai ya ukiukaji wa masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa.
Hatua hiyo, imekuja ikiwa ni wiki chache tu tangu Mei 7, 2026, Msajili akikitaka Chadema kujieleza kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria, ikiwemo kusimamishwa au kutozwa faini kwa madai ya ukiukaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Chadema ikiwa tayari imejibu barua ya kwanza ya Msajili, Mei 26, 2026 ililimwa nyingine Chadema ikitakiwa kujieleza kwa nini isichukuliwe hatua kwa kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa kwa kauli mbalimbali zilizotolewa na viongozi na makada wake.
Licha ya kujibu barua ya kwanza, Chadema ilifungua shauri na kupata zuio la Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Babati mkoani Manyara dhidi ya ofisi ya Msajili, ikitakiwa isichukua hatua zozote dhidi ya chama hicho hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.
Pamoja na zuio hilo, ofisi hiyo imekilima barua nyingine, ambayo Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza haijakiuka amri ya mahakama kwa kuwa hilo ni tukio jipya.
Kwa mujibu wa barua hiyo, ambayo kama ilivyokuwa ile ya kwanza imesainiwa na Nyahoza, Ofisi ya Msajili inaitaka Chadema kuwasilisha maelezo kuhusu utekelezaji wa masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 (Toleo la urekebu la mwaka 2023).
Msajili katika barua hiyo ameeleza kuwa katika mitandao ya kijamii zipo video zikiaonyesha Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi akiongea lugha/maneo ya matusi, kashfa na dhihaka dhidi ya wanasiasa wenzake katika mkutano wa hadhara wa chama hicho.
Kitendo hicho Msajili amekitaja kama ukiukwaji wa kifungu cha 9(2) na 19(2)(f) vya Sheria ya Vyama vya Siasa. Maneno hayo pia yanakiuka Kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Kuratibu mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa za mwaka 2023 (TSN. 209).
Nyahoza amenukuu maneno yaliyotamkwa na Mbilinyi kwenye mkutano huo wa hadhara kuwa”…wamekuja na slogan saizi wanazunguka, never, never, never! matako yenu…”
Amekitaka chama hicho kuwasilisha maelezo kwa nini usajili wake usisimamishwe au kutozwa faini kwa kukiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa ikiwemo masharti ya usajili au kupewa adhabu kwa mujibu wa kanuni ya 11 ya Kanuni za Kuratibu Mikutano ya Hadhara ya Vyama vya Siasa za Mwaka 2023.
“Maelezo yenu yawasilishwe Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa siyo zaidi ya tarehe 08 Juni 2026 saa tisa na nusu alasiri. Nimekutumia video hizo kwa njia ya baruapepe ya chama na yako binafsi na WhatsApp,” ameandika Msajili.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema wataishughulia kwa mujibu wa taratibu, kanuni, katiba na maadili na itafaki ya chama hicho.
Sambamba na hilo, Mnyika amesema watachukua hatua zinazostahiki dhidi ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, akidai inakiumiza chama hicho.
Masharti wanaoataka kurejea
Wakati huohuo, Heche amesema haitakuwa rahisi kwa baadhi ya makada wake za zamani kurejea, akiweka wazi wapo watakaoshughulikiwa kwa namna tofauti, hasa waliowahi kushiriki vitendo vilivyotishia uhai wa chama hicho.
Amesema hata wale waliowahi kukishtaki chama hicho mahakamani uanachama wao uko mashakani, kwa kuwa vitendo hivyo viliiweka Chadema katika wakati mgumu wa kutekeleza shughuli za kujijenga.
Chadema inakuja na msimamo huo, wakati ambao waliokuwa makada wake waandamizi watatu waliokihama chama hicho kwa nyakati tofauti, wamejea na kukabidhiwa kadi za uanachama katika matawi wanayotokea.
Makada hao ni Mchungaji Peter Msigwa aliyekuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) amerejea Mei 23, 2026, Patrick Assenga aliyekuwa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na Joseph Selasini aliyekuwa NCCR Mageuzi.
Hata hivyo, zipo tetesi za makundi mengine ya makada wake wa zamani kuwa mbioni kurejea ndani ya chama hicho, ingawa hazijathibitishwa rasmi.
Heche amesema anaamini watu wengi watatoka vyama mbalimbali kikiwemo tawala na kujiunga na Chadema, lakini haitakuwa rahisi kwa wageni hao kujiunga nao.
“Nataka nikuhakikishie, kuna watu ambao kwa makosa makubwa waliyokifanyia chama hiki, hao tutaangalia namna nyingine ya kushughulika nao,” amesema.
Amesisitiza hata kama mtu huyo alikuwa mwanachama wao, lakini alijaribu kukiua chama hicho kwa makusudi, kinyume cha utaratibu wa katiba yake, watashughulika naye kwa njia tofauti.
“Kama kuna watu walijaribu kwa makusudi na wakafanya matukio ya kuhatarisha kuwepo kwa chama chetu, wasitarajie itakuwa rahisi sana, kwa sababu hata wanachama wetu hawatakubali hao watu wapate nafasi tena kwenye chama chetu,” amesema Heche.
Walioishtaki Chadema shakani
Heche, amesema watatumia njia za kikatiba kuwakabili watu hao, kwani inaeleza wazi kuwa ukikishtaki chama ni kujiondoa moja kwa moja.
“Sisi hatukuchukua hatua kwa mtu yeyote kwa sababu wangesema oooh… mnachukua hatua wakati ambao labda kesi inaendelea, hakuna kitu tutaacha kwa sababu sisi ni chama ambacho tunataka kujenga nidhamu, kufuata sheria na utaratibu.
“Nakuhakikishia kwamba lazima kuna hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa katiba kwa baadhi ya watu,” amesema.
Kwa upande mwingine, mmoja wa waliofungua kesi ya mgawanyo wa mali iliyofutwa, Said Issa Mohamed ameliambia Mwananchi kuwa, hajakata tamaa licha ya uamuzi wa mahakama kuifuta kesi hiyo.
Amesema kesi kufutwa ni jambo la kawaida ila anachokipigania ni uwiano sawa wa mali za Chadema kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Nitashauriana na wanasheria wangu, lakini pili nitaangalia utekelezaji wa makubaliano tuliyokubaliana pembeni na uongozi wa sasa. Tulikubaliana kuna vitu wanavyopaswa kuvifanya kwa Zanzibar,” amesema.
Hata hivyo, Said amedai kuwa kuna mazungumzo yanaendelea baina yao na uongozi wa sasa wa Chadema, kuhusu mambo wanayoyalalamikia.
“Kuna mazungumzo tumeyafanya na wahusika, kuna mambo ambayo tumezungumza binafsi kwa sababu na sitaki yaende kwenye vyombo vya habari kwa hatua ya sasa. Mimi bado mwanachama halali wa Chadema, tunachokipigani ni haki,” amesema.
Hata hivyo, Heche amesema Said hana nafasi yoyote ndani ya Chadema kwa sasa, hivyo si rahisi kujua kinachoendelea ndani ya chama hicho.
Katika maelezo yake, Issa amesema angependa kuona kama Kanda za Chadema Tanzania bara zina magari, basi upande wa Zanzibar iwe hivyo hivyo, hata kwa upande wa ruzuku pia.
“Hiki ndicho ninachokipigania na haya yapo kwenye karatasi za vikao vya kamati maalumu ya Zanzibar. Tulikuwa tunapata ruzuku Sh300 milioni lakini Zanzibar tulipata Sh2 milioni, sasa tunataka iwekwe wazi kwamba ruzuku ikitoka Zanzibar itakuwa inapata asilimia 3 au 5,” amesema.
Kuhusu kesi ya mgawanyo wa mali, kupoteza muda, Said amesema, “wao (Chadema) ndio wametaka kwa sababu siku ya kwanza wangekubali kulifanyia kazi jambo hilo lingekuwa limeshaisha, ila walibisha wakisema si kweli.
“Nasubiri utekelezaji yale tunayoyataka, hatutakuwa na kesi, wasipotekeleza tutafuata miongozo mingine ya kisheria kufunga kesi. Shida hapa si kukomoana, bali kuona yale yaliyojadiliwa kwenye vikao yanatendeka,” amedai.
















