Dar es Salaam. Ndoa ni aina ya uhusiano wenye uzito mkubwa zaidi katika maisha ya mwanadamu.
Ni ahadi ya kushirikiana maisha, hisia, mipango na changamoto.
Hata hivyo, wataalamu wengi wa masuala ya ndoa wanakubaliana kwamba ndoa haipaswi kumfanya mtu apoteze utambulisho au maendeleo binafsi ikiwamo umiliki wa mali.
Mtaalamu mashuhuri wa masuala ya ndoa, Dk John Gottman, ambaye amefanya kazi za kitafiti kwa miongo kadhaa kuhusu ndoa, anasisitiza mara nyingi kwamba ndoa imara hujengwa na watu wawili waliokomaa kihisia na kiakili.
Anaonyesha kuwa ndoa haifanikiwi pale mmoja anapojitoa kupita kiasi cha kupoteza sauti, mipaka na malengo yake binafsi ya kimaisha.
Hapa ndipo ujumbe wa: “Endeleza ndoa, lakini usisahau nawe kujiendeleza” unapopata maana.
Maendeleo ya ndoa hayapaswi kuathiri ndoto zako, kugharimu usalama wako wa kifedha, au maisha yako ya baadaye. Ndoa ni safari, lakini bado kila mmoja ana miguu yake miwili ya kutembelea.
Mwandishi wa masuala ya mapenzi na jamii, Bell Hooks, aliwahi kuandika kwa dhana kwamba upendo wa kweli hauwezi kuwepo pale ambapo mmoja analazimika kujikana ili mwingine awe salama.
Kwa mantiki hiyo, ndoa yenye afya inahitaji watu wawili wanaojipenda, wanaojithamini na wanaojijenga, si wanaojitoa mpaka kujipoteza.
Moja ya maeneo nyeti zaidi katika ndoa ni suala la mali. Waandishi wengi wameandika kuwa migogoro mingi ya ndoa haianzi kwa ukosefu wa mapenzi, bali kwa fedha, umiliki na nguvu ya uamuzi.
Ndani ya mazingira ya mapenzi, watu wengi hufanya uamuzi wa haraka wakiamini kuwa “tuko pamoja milele”.
Mwandishi na mshauri wa masuala ya fedha na ndoa, Dave Ramsey, amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba fedha huongeza kile kilichopo tayari kwenye ndoa; kama kuna upendo huongezeka, kama kuna migogoro huongezeka pia.
Kwa maneno mengine, mali hairekebishi ndoa, bali hufichua hali halisi ya uhusiano.
Historia ya watu mashuhuri imeshuhudia mifano mingi ya watu waliowekeza mali zao kwa majina ya wenza wao kisa mapenzi, kisha wakajikuta katika migogoro mikubwa baada ya talaka.
Bila kutaja majina kwa undani, visa hivi vimeandikwa sana kwenye vitabu na tafiti za kisheria, vikionesha kuwa kumiliki mali pamoja hakujawahi kuwa kinga ya usaliti au kuvunjika kwa ndoa.
Mtaalamu wa uhusiano, Esther Perel ameandika kwa mtazamo wa kisaikolojia kwamba mapenzi hayafi kwa sababu ya kukosa kujitolea, bali mara nyingi hufa kwa sababu ya kupotea kwa mipaka na heshima binafsi.
Hili linaakisi ukweli kwamba pale mmoja anapojitoa sana kifedha bila usalama au mipango, heshima na usawa vinaweza kuyumba.
Ndiyo maana kumiliki mali kwa jina lako mwenyewe si ishara ya kukosa mapenzi, bali ni ishara ya busara. Kumsaidia mwenza wako ni jambo la heshima, lakini kufanya hivyo kunapaswa kuwa ni sadaka ya moyo, si dhamana ya mustakabali wako.
Upendo ni mzuri, unatia moyo na unajenga matumaini. Lakini wanazuoni wengi wa uhusiano wanakubaliana kuwa upendo pekee hauwezi kubeba ndoa bila akili.
Ndoa si shindano la nani amejitoa zaidi, bali ni mkataba wa watu wawili wanaoelewana na kuheshimiana.
Hooks aliwahi kuandika kwa msisitizo kwamba upendo wa kweli unapaswa kwenda sambamba na haki na usalama wa wahusika wote.
Hii ina maana kuwa kumpenda mtu hakumaanishi kujinyima haki zako za msingi, ikiwemo haki ya kumiliki, kupanga na kulinda maisha yako ya baadaye.
Kusaidia ndoa yako ikue ni jambo la baraka. Lakini hilo lisikuzuie wewe kukua. Kuwa na mali yako, kuwa na kipato chako na kuwa na sauti katika uamuzi wa kifedha, hakupunguzi mapenzi, bali huongeza usawa na heshima.
Katika Uislamu, haki ya mwanamke kumiliki mali binafsi ni jambo lililo wazi na lisilopingika.
Mwanazuoni mkubwa, Imam Al-Ghazali aliandika kuhusu ndoa akisisitiza kuwa mwanamke ana haki kamili juu ya mali yake, na kwamba heshima ya ndoa inalindwa pale haki za pande zote zinapotambuliwa.
Kwa tafsiri ya maandiko yake, ndoa haimaanishi kuhamisha umiliki wa mali ya mwanamke kwenda kwa mwanaume.
Uislamu unatambua wazi kuwa mume ana wajibu wa kugharamia familia, lakini haukatazi mwanamke kufanya kazi, kuwekeza au kuwa na mali yake.
Hii inaonesha kuwa kujiendeleza kiuchumi kwa mwanamke si kinyume cha ndoa, bali ni sehemu ya heshima yake kama mwanadamu kamili.
Kwa upande wa Ukristo, waandishi wengi wa Kikristo wa masuala ya ndoa wamehimiza uwiano kati ya umoja na uwajibikaji binafsi.
Gary Chapman, mwandishi wa The Five Love Languages, anasisitiza: ” Upendo wa kweli unahusisha kumpa mwenza wako nafasi ya kukua, si kumfunga.” Ukuaji huo unajumuisha pia ukuaji wa kiuchumi na uwezo wa kujisimamia.
Biblia inahimiza hekima, mipango na uwajibikaji. Hakuna mafundisho yanayosema kuwa mke au mume lazima wapoteze mali zao binafsi ili ndoa iwe halali.
Kinyume chake, wanandoa wanahimizwa kusaidiana bila kupoteza wajibu wa mtu binafsi mbele ya Mungu.
Kwa mtazamo wa dini zote mbili, basi, ndoa ni ushirika wa heshima, si kufutwa kwa mipaka ya mtu binafsi.

















