Dodoma. Mkutano wa tatu wa Bunge utaendelea tena wiki ijayo, kuanzia kesho Mei 25, 2026, wizara tatu zitawasilisha bajeti zao kwa maombi ya fedha ya mwaka wa bajeti 2026/27.
Wizara zinazotarajia kuwasilisha bajeti zao ni Mambo ya Ndani ya Nchi, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itakayojadiliwa kwa siku mbili.
Wizara ya Ardhi ndiyo inatarajiwa kukabiliwa na mjadala mzito kutokana na kinachoendelea kwenye jamii hususani migogoro ya ardhi yenye sura tofauti.
Malalamiko ya wananchi yameonesha kuwepo kwa migogoro mingi inayosababishwa ama na viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia au mtu na mtu huku mchakato wa usuluhishi nao ukiwa na changamoto zake.
Jiji la Dodoma, mara nyingi limetajwa kuwa kinara wa migogoro hiyo ambayo kwa sehemu kubwa ilizaliwa wakati wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), ikakuzwa na Manispaa ya Dodoma na sasa inamwagiliwa na Jiji la Dodoma.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu aliweka kambi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kusikiliza kero za ardhi lakini hakuzimaliza kwani kadri muda ulivyokwenda ndivyo ambavyo hoja zilizidi kuongezeka na watu wengine wamekuwa wakifunga safari kutoka wilayani kumfuta ili kuwasilisha kero za wenzao.
Miongoni mwa kero hizo ni ugawaji wa viwanja kwa mtu zaidi ya mmoja, kuhamishwa kwa mipaka ya viwanja, ucheleweshaji wa hati kwa mtu aliyetimiza vigezo na wakati mwingine namba za malipo kucheleweshwa kwa makusudi.
Foleni ndefu na kauli za njoo kesho nazo zinatajwa kuwa usumbufu kwa wananchi hivyo wizara itatakiwa kuyatolea majibu maswali hayo.
Mtihani mwingine utakaomkabili Waziri wa Ardhi, Dk Leonard Akwilapo ni uwekaji wa mikapa halisi kati ya makazi ya watu na maeneo yenye hifadhi ya wanyama kwani malalamiko ya wabunge yamekuwa ni makubwa hasa mikoa ya Mbeya na Katavi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi ambaye anafungua pazia la hotuba za wiki hii, huenda naye akakutana na maswali kutoka kwa wabunge ikiwamo kambi ya walio wachache ambayo itajielekeza kwenye ukamataji, kuteswa na utekaji.
Wizara hiyo haitakuwa na mambo mengine katika kipindi hiki ambacho wabunge wengi wakiamua jambo lao hakuna mbunge anayeweza kuwahamisha kwenye msimamo.
Kwenye Wizara ya Mambo ya Nje, bado yanayotarajiwa ni ujenzi na ukarabati wa ofisi za ubalozi, lakini pia uimarishaji wa diplomasia na mataifa mengine ili kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo hasa kwenye eneo la amani na uchumi.
Vilevile, suala la uraia pacha kwa diaspora linatarajiwa kurudi tena kwani limekuwa likijadiliwa kila msimu wa bajeti huku Serikali ikieleza mikakati yake ya kuwatengenezea mazingira bora ikiwamo kuwapatia hadhi maalumu.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) katika Idara ya Uhandisi, Joshua Mkalimoto amesema wizara pekee ambayo inagusa maisha ya watu moja kwa moja ni ardhi ambayo kwake angependekeza ipangiwe angalau siku tatu za kujadili.
Mkalimoto amesema kama ingemfaa Spika wa Bunge, Mussa Zungu, aziunganishe Wizara za Mambo ya Nje na Mambo ya Ndani ili kwa pamoja wasome hotuba zao ili kuiongezea Wizara ya Ardhi siku moja ya majadiliano.
“Hii ardhi inagusa watu wengi, sasa kule kunahusu polisi, uhamiaji, magereza, zimamoto kwani hamuoni kuwa haigusi moja kwa moja maisha ya watu, watoe muda wa kutosha kwa Wizara ya Ardhi ili wabunge wawasemee wananchi wao,” amesema Mkalimoto.
Mmoja wa watumishi waliokuwa wakifanya kazi Wizara ya Ardhi, kabla ya kupelekwa taasisi nyingine, amesema kilio cha ardhi hakiwezi kwisha kama Serikali itashindwa kuweka mazingira ya kuwalazimisha watumishi wasizalishe migogoro na kwamba ikitokea mhusika awajibike.
Kiongozi huyo ameeleza kuwa ndani ya wizara kuna tamaa za baadhi ya watumishi, lakini kufanya kazi kwa maelekezo na kwa haraka ni chanzo kingine cha mgogoro, hivyo ameshauri Serikali iruhusu ardhi yote ya Tanzania ipimwe ili wao wakusanye kodi tu.














