Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi(VVU) na upatikanaji wa huduma kwa wanaoishi na virusi hivyo, Taasisi ya GGML Kilimanjaro Challenge Against HIV/AIDS Trust imetangaza uzinduzi wa kampeni mpya ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya Ukimwi nchini.
Uzinduzi huo utafanyika Mei 30, 2026 jijini Dar es Salaam kupitia matembezi ya kujiandaa ya GGML Kili Challenge 2026, yatakayowakutanisha wananchi, kampuni binafsi, taasisi mbalimbali na wadau wa maendeleo katika harakati za kuhamasisha mchango wa jamii kwenye vita dhidi ya VVU.
Mpango wa Kili Challenge, unaoratibiwa na GGML kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), umetajwa kuwa miongoni mwa miradi ya muda mrefu zaidi ya sekta binafsi nchini inayochangisha fedha kwa ajili ya mapambano ya VVU.
Kwa zaidi ya miaka 24 sasa, mpango huo umeendelea kusaidia juhudi za kitaifa kupitia ufadhili wa programu za kinga, matibabu, elimu na huduma kwa watu wanaoishi na VVU.
Akizungumza jana Jumamosi, Mei 23, 2026, jijini Dar es Salaam, Meneja wa Trust wa GGML Kilimanjaro Challenge Against HIV/AIDS Trust, Stephen Mhando, amesema kampeni ya mwaka huu inalenga kuhamasisha ushiriki mpana zaidi wa wananchi katika kusaidia mwitikio wa Taifa dhidi ya Ukimwi.
“Mara zote Kili Challenge imekuwepo kwa ajili ya kuhamasisha watu na rasilimali kwa ajili ya jambo linalotuhitaji sote. Matembezi haya yanafungua rasmi msimu wa 2026 na kuwaalika watu wote kuwa sehemu ya mapambano haya.”
Amesema fedha zitakazokusanywa zitaelekezwa kusaidia programu zinazowafikia Watanzania wanaoishi na VVU katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika miaka ya karibuni, wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa jamii na sekta binafsi katika mapambano dhidi ya VVU, wakieleza kuwa changamoto ya maambukizi mapya bado ipo hususan kwa vijana na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.
Kupitia kampeni hiyo, washiriki watapata nafasi ya kushiriki matembezi au mbio za kilomita tano na 10 katika maeneo ya Masaki na Oysterbay, huku wakihamasishwa kutoa michango ya fedha kabla au wakati wa tukio.
Kaulimbiu ya mwaka huu ya: “Ni Jukumu Letu Sote,” imelenga kuwakumbusha Watanzania kuwa mapambano dhidi ya VVU hayawezi kuachiwa Serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa jamii nzima.
Mbali na uchangishaji fedha, kampeni hiyo pia inalenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kupima VVU kwa hiari, kupunguza unyanyapaa na kusaidia watu wanaoishi na virusi hivyo kupata huduma stahiki.
Kama ilivyo ada ya Kili Challenge, msimu wa mwaka huu utahitimishwa kwa washiriki kupanda Mlima Kilimanjaro na wengine kuendesha baiskeli kuzunguka maeneo ya chini ya mlima huo ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kimataifa ya kuongeza uelewa na kuchangisha fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi.














