Wamerudi Nyumbani | Mwananchi

Dar es Salaam. Kurejea kwa Mchungaji Peter Msigwa na Joseph Selasini ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumezua jambo, makada na wafuasi wa chama hicho, wakigawanyika kimitazamo kuhusu mapokezi ya wanasiasa hao. Baadhi ya wafuasi wanasema hawakupaswa kupokewa hasa kutokana na matendo yao, walipoondoka ndani ya Chadema, waliisema vibaya na hata kuitusi katika…

admin Avatar

by

6 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Kurejea kwa Mchungaji Peter Msigwa na Joseph Selasini ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumezua jambo, makada na wafuasi wa chama hicho, wakigawanyika kimitazamo kuhusu mapokezi ya wanasiasa hao.

Baadhi ya wafuasi wanasema hawakupaswa kupokewa hasa kutokana na matendo yao, walipoondoka ndani ya Chadema, waliisema vibaya na hata kuitusi katika majukwaa ya kisiasa.

Makada wengine wanasema, licha ya matendo yao walipokuwa nje ya chama hicho, kama wamejitafakari na kuona umuhimu wa kurudi wasifungiwe milango, wakisisitiza umuhimu wa Chadema kuimarisha intelejensia yake ili kubaini dhamira zao.

Wakati wafuasi wakiwa na mitazamo hiyo, Chadema yenyewe inasema sio wafuasi tu, hata wanachama na viongozi wa chama hicho, wana haki ya kuwa na wasiwasi kuhusu kurejea kwa wanachama hao, kutokana na maneno yao walipoondoka.

Mchungaji Msigwa ambaye ni mbunge wa zamani wa Iringa Mjini na Selasini, aliyewahi kuwa mbunge wa Rombo walikihama chama hicho kwa nyakati tofauti, Selasini mwaka 2020 kwenda NCCR Mageuzi na Mchungaji Msigwa Juni 30, 2024 kwenda Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mei mwaka huu wote wametangaza kurejea Chadema. Akiwa nje ya Chadema, Mchungaji Msigwa alikikosoa chama hicho katika kampeni na ziara za CCM na kuonesha jinsi ambavyo Watanzania hawapaswi kukimaini.

Katika kundi moja sogosi la WhatsApp, mfuasi wa Chadema amesema kupokewa kwa mwanasiasa aliyewahi kuhama kwenda CCM ni makosa kwa kuwa kunadhoofisha msimamo wa chama dhidi ya ufisadi na ukiukwaji wa sheria.

Amesema wanaohama kwa tamaa au masilahi binafsi na kurejea, hawapaswi kupokewa kirahisi.

Hata hivyo, wengine wamepinga hoja hiyo wakisema walioondoka na kutambua walikosea wanapaswa kuruhusiwa kurejea.

Wamesema Chadema inaweza kutumia mbinu za kiintelejensia kubaini dhamira zao, huku wakisisitiza kuwa, Katiba inaruhusu uhuru wa kisiasa na kujiunga na chama chochote.

Alipoulizwa kuhusu mashaka ya baadhi ya wafuasi wao, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa, ameeleza sio wafuasi tu, hata wanachama na viongozi wana haki ya kujiuliza maswali na kuwa na wasiwasi.

Amesema ni haki ya wanachama wote kuwaambia wanasiasa hao kwamba maneno mabaya waliyoyasema kwa chama hicho walipoondoka bado hayajasahaulika.

Pamoja na hayo, amesema ukweli unabaki kuwa, watu wana haki ya kwenda kwenye chama chochote ambacho moyo wao unakiamini, hasa wanapoona waliko kumeyumba.

“Wale waliorudi pengine kwa sababu hawakuridhishwa na kule walikokuwepo, kwa kufuata utaratibu tunawarejesha tu. Watakwenda kwenye tawi watapokewa na kuonesha kwamba wamekubali kuendana na itikadi za chama,” amesema.

Golugwa, amesema hiyo haitazuia wanachama na viongozi kuuliza ili kupata uhakika kwamba ilikuaje walisema vibaya wakati wameondoka.

“Sasa suala la kumuamini inategemea na muda na matendo yake kwa kadiri siku unavyokwenda akiwa mwanachama. Tutaendelea kuwa macho kuangalia mienendo yao,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu hayo, Mchungaji Msigwa ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa amesema yeye ni mwanademokrasia, anapenda kukosoa na kujenga hoja, hivyo atafanya makosa asipowaruhusu wengine kujenga hoja dhidi yake.

Uamuzi wake wa kurejea Chadema, amesema aliufanya akiwa na matarajio ya mapokezi ya aina tofauti ya watakaofurahia, watakaokuwa na shaka, watakaochukia, watakaochukua muda kumpokea na wengine ambao hawatampokea kabisa.

“Wakati natangaza kurudi, nilikuwa na matarajio ya makundi matatu. Kundi la watakaofurahi, watakaokuwa na shaka, watakaochukia na wapo ambao itawachukua muda kunipokea na wengine hawatanipokea kabisa,” amesema Msigwa ambaye tayari amepokewa ndani ya chama hicho na kupewa kadi mpya ya uanachama, Kata ya Mkimbizi, Iringa Mjini.

Pamoja na yote hayo, Mchungaji Msigwa amesema wanachama wenzake wanapaswa wampe muda ili anayoyasema na kuyasimamia ayathibitishe kwa vitendo.

Katika andiko lake la kuhamia tena Chadema, Mchungaji Msigwa amedai amefikia uamuzi huo baada ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, dhuluma na ukosefu wa utu yaliyotokea Oktoba 29, 2025.

Amesema matukio mbalimbali yaliyoshuhudiwa nchini yalimfanya aanze kutafakari upya kuhusu nafasi yake kisiasa na wajibu wake kwa jamii na kuwa haki, utu na demokrasia ni misingi ambayo haipaswi kupuuzwa katika taifa lolote.

Akizungumzia hilo, Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Richard Kasesela, amemjibu Mchungaji Msigwa kwa kuandika siasa zinahitaji msimamo, uaminifu na huduma kwa wananchi badala ya mihemko.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Kasesela aliyewahi kuwa mkuu wa Wilaya ya Iringa ameandika kuwa,  kuingia au kutoka kwa mwanasiasa mmoja hakubadilishi uimara wa CCM kwa kuwa chama hicho kina mizizi imara kwa wananchi kuanzia ngazi ya mashina hadi Taifa.

‎”Kutumia matukio hayo kama msingi wa kuondoka CCM ni sehemu ya mkakati wa kisiasa unaolenga kujitafutia uhalali wa kurejea Chadema,” ameandika Kasesela.

Ameandika kuwa, mwanasiasa anayebadilika kulingana na upepo wa kisiasa hupoteza sifa ya msingi ya uongozi ambayo ni uaminifu na uthabiti wa uamuzi na wananchi wanahitaji viongozi wenye dira na misimamo inayotabirika.

Amesisitiza CCM itaendelea kusimamia misingi ya umoja, mshikamano na maendeleo ya Watanzania bila kuyumbishwa na uamuzi wa mtu mmoja mmoja na kuwa nguvu ya chama hicho ipo kwa wanachama wake wa kawaida.

‘Watapitia nyakati ngumu’

Mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Profesa Ali Makame Ussi amesema wanasiasa wanaohama vyama na kurejea hukabiliwa na changamoto ya kurejesha uaminifu na ushawishi wao wa kisiasa.

Amesema mara nyingi huonekana wanatanguliza masilahi binafsi kuliko itikadi za vyama, akitolea mfano Bernard Membe, Edward Lowassa na Wilbrod Slaa ambao ushawishi wao ulipungua baada ya kuhama CCM na kurejea.

“Katika matukio mengi, mwanasiasa anapoondoka ndani ya chama, hata akirejea baadaye, kiwango cha uaminifu na nguvu yake ya kisiasa inapungua. Mara nyingi huonekana kama watu wanaoweka mbele masilahi yao binafsi kuliko masilahi ya chama,” amesema.

Kwa upande wa mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Salbinus David amesema matukio hayo yanaendelea kuonesha  Chadema bado ina mvuto wa kisiasa, ndiyo maana inafuatwa.

Amesema sio kina Msigwa tu,  kuna uwezekano wa wanachama wengine wa zamani wa Chadema kurejea ndani ya chama hicho, hasa baada ya chama hicho kurejea kwenye shughuli za wazi za kisiasa na kuonekana bado kina ushawishi na mvuto kwa wafuasi.

“Kuna uwezekano wanachama wengi zaidi wa Chadema wakarejea, kwa kuwa chama kimeanza tena shughuli zake za kisiasa na kinaendelea kuvutia umma, baadhi ya wanasiasa wanaweza kuhisi kuwa mazingira ya kisiasa yamebadilika tena,” amesema.

Jana, chama hicho kilizindua Operehseni Katiba Mpya Kanda ya Kati, katika mkutano wa hadhara uliofanyikia Uwanja wa Mtekelezo, Dodoma Mjini na kuhutubiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu, John Mnyika.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasi, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amesema kilio cha viongozi wa Chadema si kutaka ubunge bali kuwe na haki ya kufanya uchaguzi huru, haki na wa amani huku akiwaonya viongozi wasiotekeleza wajibu wao ipasavyo.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu Bon Yai amedai watenda haki wanaishia jela lakini mafisadi wanadunda mtaani.

Kwa upande wake, Mnyika amesema hali ya mwenyekiti wao, Tundu Lissu aliyeko gerezani zaidi ya mwaka sasa, “hali yake ya afya inaendelea vizuri na licha ya hali yake inaendelea vizuri, siku anatoka nje tutampeleka hospitali kupima.” Akidai lengo ni kujua utimamu wa afya yake.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports