Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa amesema bado anaendelea kufanya tathmini ya kina kabla ya kutoa uamuzi kuhusu majibu yaliyowasilishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufuatia tuhuma zilizotolewa dhidi yao.
CCM na Chadema vinadaiwa, kwa nyakati tofauti, kutoa kauli kupitia viongozi wao ambazo zinatafsiriwa za kuchochea chuki na mgawanyiko katika jamii na kuvunja Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 na kanuni zake.
Hali hiyo ilisababisha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuviandikia barua ya kutaka maelezo na kuvitaka kuwasilisha majibu ndani ya muda uliopangwa huku kwa Chadema msajili alikieleza kwa nini asisimamishe usajili kwake kwa tuhuma hizo.
Mei 19, 2026, Chadema iliwasilisha majibu yake kwa barua ya msajili yenye kumbukumbu namba HA.322/362/16A/22 ya Mei 7, 2026. Katika majibu hayo yaliyobeba hoja 50, chama hicho kilikana tuhuma zote kilizoelekezwa nacho.
Pia, Chadema ilieleza hata kama kungekuwa na ukiukwaji wa Katiba, madai hayo yanayohusu makosa ya jinai yanaweza kuamuliwa na Mahakama pekee iwapo yamethibitishwa au la na si Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Chama chetu hakijakiuka Sheria ya Vyama vya Siasa kama inavyodaiwa. Kilichofanyika ni utekelezaji wa haki za kisiasa na Kikatiba zilizoainishwa katika Katiba ya nchi,” ilieleza sehemu ya barua hiyo ya Chadema kwenda kwa msajili.
Kwa upande wa CCM, Mei 21, 2026, chama hicho kiliwasilisha maelezo yake kujibu barua ya msajili iliyotaka ufafanuzi kuhusu kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Mary Chatanda.
Kauli hiyo ilizua mjadala mkubwa baada ya Chatanda kudai kama angepewa mamlaka ya kuiongoza nchi hata kwa dakika moja, asingependa kuwaona watu aliowataja kuwa wanatumiwa kutoka nje ya nchi wakiendelea kuwepo.
“Nasema, kama ningekabidhiwa nchi hii hata kwa dakika moja tu! Mama Samia, sijui kama wale watu wangekuwepo. Wamemkuta ndugu yetu mpendwa, Dk Samia, akiwa mpole, mnyenyekevu na msikivu,” alisema Chatanda Mei 18, 2026 akiwa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge, Isimani mkoani Iringa.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Mei 24, 2026, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, amesema ofisi hiyo imepokea na kupitia majibu yote kutoka CCM na Chadema na kwamba yanaendelea kufanyiwa tathmini kabla ya kufikiwa uamuzi.
“Tumepokea barua zote za CCM na Chadema, tumezisoma na tunaendelea kuzifanyia kazi. Hatuna haraka ya kutoa majibu kwa sasa kwa sababu mchakato wa tathmini bado unaendelea kabla ya kufikia uamuzi,” amesema Nyahoza.
Amesema ofisi hiyo haiwezi kutaja muda maalumu wa kutoa majibu, kwa kuwa bado inahitaji muda wa kuchunguza kwa kina hoja na tuhuma zilizowasilishwa.
“Tunaweza kuamua kuwaita tena kwa ajili ya mazungumzo au usikilizaji zaidi, kulingana na namna tutakavyoendelea kuzifanyia kazi taarifa hizi. Ofisi ya Msajili ina mamlaka ya kuita wahusika iwapo itaona kuna haja ya kupata ufafanuzi wa kina zaidi,” amesema.
Nyahoza amesema iwapo maelezo yaliyowasilishwa na vyama hivyo yataonekana kujibu kwa kina hoja zote zilizotolewa, Ofisi ya Msajili itatoa msimamo wake rasmi kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Akizungumza kuhusia na ofisi ya Msajili kuhusu suala hilo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo (CEGODETA), Thomas Ngawaiya amesema msajili wa vyama vya siasa anapaswa kutoa majibu au maoni yake kwa kuzingatia sheria ya vyama vya siasa.
“Endapo madai hayo yatathibitika kuwa ya kweli, katika majibu yake asiwe na upendeleo wowote, bali afuate sheria zinazovibana vyama vyote kwa usawa, ikiwemo CCM, Chadema na vyama vingine vyote vilivyosajiliwa,” amesema.
Ngawaiya amesema uamuzi wa msajili utakuwa na maana ikiwa utazingatia sheria ya vyama vya siasa bila kuegemea upande wowote, kwani kufanya tofauti na hapo kunaweza kusababisha minong’ono mikubwa katika jamii.















