Kigoma. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma imeridhia maombi ya walalamikaji katika kesi ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini, uliompa ushindi mbunge wa jimbo hilo, Clayton Chipando, maarufu Baba Levo kuongezewa muda wa kuwasilisha mahakamani maelezo ya maandishi ya mashahidi wao.
Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa jana Juni 18, 2026 jioni na Jaji Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo iliridhia maombi ya walalamikaji hao baada ya kukubaliana na hoja za wakili wao, huku ikitupilia mbali hoja za mawakili wa Baba Levo walioyapinga vikali.
“Hivyo maombi haya yanakubaliwa na waombaji wanapaswa kuwasilisha maelezo ya maandishi ya mashahidi kama sheria inavyoelekeza. Sitoi amri kuhusu gharama, kwa hiyo kila upande utabeba gharama zake wenyewe,” alisema Jaji Nongwa akihitimisha uamuzi huo baada ya kuchambua na kujadili hoja za pande zote.
Kesi hiyo imefunguliwa na wananchi wanne, Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Kigoma Mjini, mbunge wa jimbo hilo, Baba Levo mwenyewe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Walalamikaji hao wanapinga ubunge wa mbunge wa jimbo hilo, Baba Levo (CCM), aliyetangazwa kushinda kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimzidi mpinzani wake kutoka Chama cha ACT-Wazalendo, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Zitto Kabwe.
Wanadai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na kasoro za ukiukwaji wa taratibu, kanuni na Sheria za Uchaguzi, pamoja na mambo mengine wakidai kuwa kulikuwa na vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.
Kesi hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa ushahidi wa walalamikaji jana Juni 18, 2026.
Hata hivyo walalamikaji hawakuweza kuwasilisha mahakamani maelezo ya maandishi ya mashahidi kwa wakati kama walivyoamuriwa, kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Wabunge na Rais za Mwaka 2025.
Hivyo Juni 17, walifungua maombi madogo wakiomba kuongezewa muda wa kuwasilisha maelezo hayo ya mashahidi ambayo yalisikilizwa jana Juni 18, 2026 kabla ya kusikiliza kesi ya msingi kwa kuwa usikilizwaji wa kesi ya msingi ulitegemea uamuzi wa maombi hayo.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo jana, Juni 18, 2026, wakili wa walalamikaji hao, John Seka aliieleza mahakama kuwa walalamikaji wameshindwa kuwasilisha maelezo hayo ya mashahidi ndani ya muda uliowekwa kutokana na ufinyu wa muda.
Alidai kuwa kulingana na kanuni hizo, maelezo hayo yalipaswa kuwasilishwa kwa Msajili ndani ya saa 48 kabla ya saa ya usikilizaji.
Hata hivyo alidai kuwa muda wa mwisho wa kuwasilisha maelezo hayo ulikuwa ni kabla ya saa 6:00 mchana, Juni 16, 2026.
Alidai kuwa kwa kuwa usikilizwaji wa awali ulichelewa kukamilika ambao uliisha saa 12 basi kutoka Juni 15, 2026 saa 12 mpaka Juni 16 kabla ya saa 6 mchana ni saa 18 tu, zikiwemo saa 12 zisizo za kazi (usiku).
Hivyo alidai kuwa muda waliobakia nao kutekeleza amri hiyo ulikuwa ni saa sita tu, yaani kuwatafuta mashahidi 20, kuwahoji kuandaa nyaraka zikiwemo za kurasa 180 na za kielektroniki yaani picha jongefu (video) zaidi ya 60.
Wakili Seka alidai kuwa kwa mazingira hayo jambo hilo halikuwezekana na ndio maana wanaomba kuongezewa muda.
Alidai kuwa walalamikaji wameweza kukidhi vigezo vya kisheria vilivyokwishawekwa na mahakama katika uamuzi wa mashauri mbalimbali ambavyo ni pamoja na kuonesha sababu za kuchelewa, kutokuchelewa kwa muda mrefu na kwamba hawakuzembea kutafuta haki yao hiyo.
Hata hivyo mawakili wa Baba Levo (mjibu maombi wa pili), Daniel Rumenyela na Thomas Msasa walipinga vikali maombi hayo wakiwasilisha hoja mbalimbali kuishawishi mahakama iyatupilie mbali maombi hayo.
Walidai kuwa walalamikaji wamefanya uzembe na kupuuza amri ya mahakama kwa kuwa walikuwa na muda wa kutosha wa saa 48 ambazo zilikuwa zinaishia Juni 17, 2026 saa 12 jioni.
Walidai kuwa hata kama mashahidi wengine wapo nje ya Kigoma, wangeweza kuwasilisha maelezo ya mashahidi wanaoweza kupatikana kisha ambao wangeshindwa kuwapata kwa wakati kisha wangeiomba mahakama waruhusiwe kutoa ushahidi kwa mdomo.
“Hata hivyo hawakuwasilisha hata maelezo ya shahidi hata mmoja na hata ya walalamikaji ambao wanapatikana,” alidai Wakili Rumenyela.
Pia alidai kuwa wakili wa walalamikaji hajasema kuwa wanaomba kuongezewa muda kwenye shauri gani, wala muda gani wanaouomba kuongezewa na kwamba katika kiapo cha kuunga mkono hawakubainisha sababu za kuridhisha.
Vilevile alidai kuwa kiapo kinachounga mkono maombi hayo kina kasoro kutokana na kutaja muda wa kukithibitisha ambao haupo, kwani muda uliotajwa Desemba 24, 2025 ulishapita na kasoro hiyo haiwezi kurekebishika.
Wakili Msasa kwa upande wake alidai kuwa kwa kasoro hiyo kiapo hicho ni batili na kinapaswa kufutwa pamoja na kesi ya msingi kwani haitakuwa na miguu ya kusimamia mahakamani.
Akijibu hoja za mawakili wa Baba Levo, wakili Seka alisisitiza hoja yake ya ufinyu wa muda na maombi ya kuongezewa muda hayana ukomo wa muda kisheria na kwamba wameeleza sababu za msingi.
Alifafanua kuwa maombi hayo kama kichwa cha habari kinavyojieleza ni ya nyongeza ya muda kwenye shauri la msingi ambalo limetajwa (kesi ya uchaguzi).
Kuhusu hoja ya kasoro ya kiapo, wakili Seka alieleza kuwa wao wenyewe ndio wameigundua kasoro hiyo na kama maofisa wa mahakama wao ndio wameieleza na kubainisha kuwa inatibika.
Akitoa uamuzi wake, Jaji Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo alisema kuwa baada ya kuchambua hoja za pande zote anakubaliana na wakili wa waombaji, Seka, kuwa alitakiwa kukutana na mashahidi wote na kuwaandaa kabla ya kuwasilisha mahakamani maelezo yao.
Alisema kuwa asingeweza kuwaandaa kabla ya kukamilika kwa hatua ya usikilizwaji wa awali na kwamba baada ya kukamilika usikilizwaji wa awali ndipo ilijulikana kuwa ni mambo gani ya msingi wanayopaswa kuyathibitisha.
Jaji Nongwa aliongeza kuwa hata kama angeweza kukutana na mashahidi wachache asingeweza kuwasilisha mahakamani maelezo yao, kwani kwa kufanya hivyo basi angelazimika kuwatumia mashahidi hao wachache tu.
Jaji Nongwa alibainisha kuwa kuwasilishwa kwa haraka kwa maombi hayo bila kuchelewa, kueleza sababu na kutokuonesha uzembe na iwapo kuna hoja ya msingi ni miongoni mwa masharti ya mahakama kuongeza muda kwa waombaji.
Pia alisema kuwa mawakili wa Baba Levo hawaoneshi ni namna gani mjibu maombi huyo ataathirika kama waombaji wataongezewa muda huo.
Kuhusu kasoro za kiapo cha waombaji zilizoelezwa na mawakili wa Baba Levo, Jaji Nongwa akirejea uamuzi wa mashauri mbalimbali alisema kuwa hiyo inarekebishika.
“Kueleza kuwa ni muda gani waombaji wanaomba kuongezewa haijawahi kuwa takwa la kisheria,” alisema Jaji Nongwa.
Kuhusu hoja ya mawakili wa Baba Levo kuwa wakili wa waombaji hakutaja shauri waliloombea nyongeza ya muda kwenye kiapo, bali alilitaja kuwa ni katika kesi ya uchaguzi wakati akitoa hoja mahakamani, Jaji Nongwa alisema kuwa ni jambo lililo wazi kuwa maombi hayo yanahusu shauri gani.
Jaji Nongwa alisema kuwa wakili wa waombaji ameeleza kuwa mashahidi anaokusudia kuwaita wapo ndani na nje ya Kigoma na isingekuwa rahisi kuwapata na kuwaandaa wote kwa wakati.
Alisema kuwa waombaji wamefafanua kuwa kuchelewa kwao kuwasilisha maelezo ya mashahidi si kwa uzembe na wameeleza sababu za msingi.
Amesisitiza kuwa kama alivyoeleza, waombaji hao wamewasilisha maombi haya kwa haraka ndani ya siku mbili tangu usikilizwaji wa awali ulipofanyika na wameeleza kikamilifu sababu za kuchelewa kuwasilisha maelezo ya mashahidi.
Hivyo nimejiridhisha kuwa maombi hayo yana msingi na waombaji wanastahili nyongeza ya muda wa kuwasilisha maelezo ya mashahidi,” alisema Jaji Nongwa.
Baada ya uamuzi huo, Jaji amepanga kuendelea na usikilizaji wa kesi ya msingi ( ya kupinga ubunge wa Baba Levo) kuanzia Julai 6, 2026.

















