DAR ES SALAAM: SERIKALI imepeleka na kusimika maabara mbili jongezi zenye uwezo wa kupima sampuli za ugonjwa wa Ebola katika mikoa ya Kagera na Kigoma ili kuimarisha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo.
Waziri wa Afya, Mohamed Omary Mchengerwa amesema hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za uchunguzi karibu na wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopakana na nchi zilizoathirika na mlipuko wa ugonjwa wa ugonjwa huo.
“Tumepeleka na kusimika maabara mbili jongezi katika mikoa ya Kagera na Kigoma ili kuhakikisha sampuli za wahisiwa zinapimwa kwa haraka na hatua stahiki zinachukuliwa kwa wakati,” amesema Mchengerwa.
Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza uwezo wa taifa katika kugundua na kudhibiti milipuko ya magonjwa ya kuambukiza.
Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa wataalam wa maabara, kusambaza vifaa muhimu vya uchunguzi pamoja na kuimarisha uratibu wa huduma za dharura katika maeneo yenye hatari kubwa ya kuingiza maambukizi kutoka nje ya nchi.
“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna ucheleweshaji wa uchunguzi wa sampuli na kwamba wananchi wanapata huduma kwa wakati huku tukihakikisha usalama wa afya ya Taifa letu,” alisisitiza Waziri Mchengerwa.
Hatua hiyo imekuja sambamba na juhudi nyingine zinazotekelezwa na Serikali za kuimarisha uchunguzi katika mipaka, viwanja vya ndege na bandari ili kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini.













