John Bukuku, Dar es Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake imepata mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, ambapo makusanyo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 538 kwa mwaka hadi kufikia shilingi trilioni 32.3 katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Kauli hiyo amesema Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusuf Mwenda, wakati akizungumza katika Kongamano la Pili la Kodi la TRA (TRA Tax Symposium 2026) linalofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam Juni 19, 2026, likiambatana na maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996.
Amesema TRA imeendelea kufanya mageuzi makubwa ya kiutendaji kwa lengo la kuboresha huduma kwa walipa kodi, kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kujenga mfumo unaochochea ulipaji kodi kwa hiari.
CPA Mwenda amesema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano mkubwa kati ya TRA, walipa kodi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali ambao wamekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya mfumo wa kodi nchini.
Amesema ukuaji wa mapato kutoka shilingi bilioni 538 mwaka 1996 hadi kufikia shilingi trilioni 32.3 katika mwaka wa fedha 2025/2026 unaonyesha mafanikio ya kujenga uelewa na uhiari wa wananchi katika kutimiza wajibu wa kulipa kodi.
Ameongeza kuwa TRA imeendelea kukua kutoka kuwa na watumishi chini ya 500 ilipoanzishwa hadi kufikia zaidi ya watumishi 8,800 kwa sasa, jambo lililosaidia kuongeza uwezo wa kutoa huduma bora kwa walipa kodi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Nsubili Joshua, aliyemwakilisha Waziri wa Fedha, amesema walipa kodi na wakusanyaji wa kodi ndio msingi muhimu wa mafanikio ambayo Serikali imeendelea kuyapata katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema serikali yoyote duniani hutegemea kodi ili kujiendesha na kutekeleza majukumu yake, hivyo walipa kodi hawapaswi kujiona watu wa kawaida bali ni washirika wakuu wa maendeleo ya taifa.
Amesema mafanikio ya Serikali katika utekelezaji wa mipango yake yanategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa walipa kodi na taasisi zinazokusanya mapato, hivyo amewapongeza wadau hao kwa mchango wao katika maendeleo ya Tanzania.
Awali, Mkuu wa Chuo cha Kodi, Profesa Isaya Jairo, amesema Kongamano la Pili la Kodi la TRA ni fursa ya kutathmini safari ya miaka 30 ya mamlaka hiyo, kujadili mafanikio yaliyopatikana na kuweka mikakati ya kuimarisha usimamizi wa kodi kwa miaka 30 ijayo.
Amesema mazingira ya usimamizi wa kodi yanaendelea kubadilika kutokana na maendeleo ya teknolojia, mifumo ya kidijitali, utandawazi na mabadiliko ya namna biashara zinavyofanyika duniani, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuboresha mifumo ya kodi.
Kongamano hilo linalofanyika limebeba kaulimbiu isemayo “Miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania: Mafanikio na Matarajio kwa Miaka 30 Ijayo,” likiwakutanisha watunga sera, wataalamu wa kodi, sekta binafsi, taasisi za elimu, washirika wa maendeleo na walipa kodi.
Lengo la kongamano hilo ni kujadili namna bora ya kuimarisha usimamizi wa kodi, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali na kujenga mfumo endelevu wa kodi unaochangia maendeleo ya taifa.
















