Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Nyenzo za Utekelezaji wa Dira 2050 Juni 29, 2026 jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais- Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango Dkt Tausi Kida wakati akitoa elimu kwa wananchi mbalimbali juu ya utekelezaji wa Dira 2050 katika maonesho ya wiki ya utumishi wa umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park-Jijini Dodoma.
Akiwa katika viwanja hivyo kwenye Banda la Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Kida aliwaambia waandishi wa Habari kuwa Tume hiyo imekamilisha nyenzo za utekelezajiwa wa Dira 2050 sambamba na Mfumo wa kitaifa wa kusimamia mipango na miradi ya maendeleo unaojulikana kama e-Delivery.
“Tumekamilisha nyenzo zote za utekekezaji wa Dira 2050, ikiwa ni pamoja na Mipango ya utekelezaji, Miongozo na Mifumo ya Usimamizi na Ufuatiliaji na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atazindua Nyenzo hizo tarehe 29 Juni, 2026” amesema Dkt. Kida.
Aidha, amefafanua kuwa nyenzo zitakazozindualiwa ni pamoja na Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/27-2050/51, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2026/27-2030/31 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2026/27 pamoja na Mfumo wa kitaifa wa kusimamia mipango na miradi ya maendeleo unaojulikana kama e-Delivery.

















