Dodoma
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeendelea kujivunia mafanikio ya matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kieletroniki kupitia mfumo Mfumo wa Ununuzi wa Umma wa Tanzania (NeST).
Mafanikio hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando alipotembelea banda la Mamlaka hiyo kwenye maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali, Jijini Dodoma.
Bw. Sando amesema kuwa moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa ilianzishwa ili kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinajitokeza kwenye utatuzi wa migogoro kwenye michakato ya ununuzi wa umma.
“Changamoto tulizoziondoa kwa wazabuni na taasisi nunuzi ni pamoja kuokoa muda, gharama, uwazi na uwajibikaji pamoja na kumbukumbu sahihi za malalamiko na rufaa zinazowasilishwa na wazabuni,” amesema Bw. Sando.
Bw. Sando amebainisha kuwa ili PPAA iweze kufanya maamuzi kuhusu shauri lililowasilishwa kwa Mamlaka hiyo ni lazima kuwa na kumbukumbu sahihi za shauri hilo, hivyo kupitia moduli PPAA imeweza kupata nyaraka mbalimbali zinazohitajika kwa wakati……. “moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa imeziunganisha taasisi nunuzi na PPAA, faida zote hizi zimeletwa na moduli hii,” ameongeza Bw. Sando
“Kwa Mwaka wa fedha 2025/26 hadi sasa malalamiko takribani 157 yamewasilishwa kupitia moduli hiyo kwa taasisi nunuzi, na kati ya malalamiko hayo mashauri 37 yamewasilishwa PPAA na kutolewa uamuzi, hivyo matumizi ya moduli yanaendelea vyema,” ameongeza Bw. Sando
PPAA inampango wa kuunganisha sekta ya utoaji haki katika ununuzi wa umma na mfumo wa utoaji haki wa Mahakama ya Tanzania kwa mwaka wa fedha ujao ili kuongeza uwazi na uwajibikaji zaidi.












