Dar es Salaam. Mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Marekani na Iran kusitisha mapigano yametiwa saini na marais Donald Trump wa Marekani na Masoud Pezeshkian wa Iran, hatua iliyofungua matumaini ya kumalizika kwa vita hivyo.
Makubaliano hayo yalitiwa saini Jumatano, Juni 17, 2026, huku mazungumzo zaidi yakitarajiwa kufanyika Ijumaa Juni 19, 2026. Hata hivyo, yameshindikana kufanyika baada ya Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, kuahirisha safari yake ya kwenda Uswisi kukutana na wajumbe wa Iran, jambo lililoongeza wasiwasi kuhusu utekelezaji wa makubaliano hayo.
Makubaliano hayo yanaweka msingi wa kufikiwa kwa makubaliano ya mwisho ndani ya siku 60, yakiweka vipengele 14 vikiwemo, kufunguliwa kwa Mlango wa Hormuz kwa usafiri wa kimataifa, kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Tehran, Iran kutojihusisha na mpango wake wa nyuklia na kuanzishwa kwa mfuko wa ujenzi upya na maendeleo ya uchumi wa Iran.
Iran imekubali kutopanua shughuli zake za nyuklia katika kipindi cha mazungumzo na kutofuatilia utengenezaji wa silaha za nyuklia, huku Marekani ikitakiwa kutoongeza vikwazo vipya wala uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo.
Hata hivyo, kabla hata wino wa makubaliano hayo haujakauka, pande hizo zimeanza kutupiana vijembe na kutoa kauli zinazoashiria kuwa safari ya amani ya kudumu bado ni ndefu.
Changamoto ya kwanza ni kuendelea kwa mashambulizi ya Israel nchini Lebanon kinyume cha makubaliano. Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, mmoja wa wapatanishi wakuu, amesema pande hizo zilikubaliana kusitisha mara moja operesheni za kijeshi katika maeneo yote ya mapigano, ikiwamo Lebanon.
Lakini, siku chache baadaye, ndege za kivita za Israel ziliripotiwa kushambulia Nabatieh Foqa na Kafr Tibnit kusini mwa Lebanon huku Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, akisema majeshi ya nchi yake yataendelea kubaki katika maeneo ya usalama nchini Lebanon kwa muda usiojulikana na kuonya kuwa iwapo Iran itaishambulia Israel kwa sababu ya Lebanon, itajibu kwa nguvu.
Mwanasayansi wa siasa wa Taasisi ya Royal United Services (RUSI), H.A. Hellyer, ameripotiwa akisema kuwa, “Ujasiri wa kijeshi wa Israel, iwe dhidi ya Iran au kupitia kuendelea kwa uharibifu nchini Lebanon, ndio tishio kubwa zaidi kwa maendeleo ya kidiplomasia.”
Jambo la pili ni akiba ya urani iliyorutubishwa ya Iran. Tehran inasisitiza mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani pekee na imeahidi kutotengeneza silaha za nyuklia, lakini suala hilo limeahirishwa hadi mazungumzo ya mwisho.
Trump ameonya kuwa makubaliano hayo si ya mwisho na yakishindikana Marekani inaweza kuanza tena mashambulizi ya mabomu, huku Spika wa Bunge la Ushauri la Kiislamu la Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, akitoa kauli tata.
“Adui ameelewa kwamba tunapozungumza kuhusu mazungumzo, upanga wetu pia uko tayari,” ameripotiwa Spika huyo na vyombo vya habari nchini Iran, kauli inayoongeza mashaka juu ya mwafaka wa amani uliofikiwa.
Changamoto ya tatu ni mustakabali wa Mlango wa Hormuz, njia inayopitisha karibu asilimia 20 ya nishati ya gesi duniani. Makubaliano yanalenga kuufungua ndani ya siku 30 na kuruhusu meli kupita bila ushuru katika siku 60 za mwanzo.
Hata hivyo, Iran imeashiria kutaka nafasi kubwa zaidi katika usimamizi wake, huku Marekani ikipinga wazo hilo. Wakati nchi saba zenye uchumi mkubwa duniani (G7) na Umoja wa Mataifa wakizitaka pande zote kuendelea na mazungumzo kumaliza mzozo huo.
Pamoja na hatua muhimu zilizofikiwa, kauli za vitisho na kutokuaminiana kati ya Washington na Tehran zinaonesha kuwa makubaliano hayo bado ni mfumo wa mazungumzo, si suluhisho la mwisho. Kama alivyoonya Hellyer, akisema “Kazi ngumu bado haijaanza hata kidogo.”

















