
Dodoma. Serikali ya Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo ili kuongeza tija, kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia shughuli za kilimo.
Hayo yameelezwa leo, Ijumaa Juni 19, 2026 na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, wakati wa mazungumzo na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Bekir Gezer.
Chongolo, amesema makubaliano hayo yataweka mkazo katika usimamizi wa mazao baada ya mavuno ili kupunguza upotevu unaowakabili wakulima na kuongeza thamani ya mazao yao.
Amesema ushirikiano huo utahusisha matumizi ya mashine za kisasa, ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao katika mazingira ya baridi na utoaji wa msaada wa kiufundi ili kuboresha mifumo ya uhifadhi na usindikaji wa mazao.
“Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na Uturuki unalenga kuimarisha ushirikiano wa kilimo kwa manufaa ya wakulima na uchumi wa Taifa kwa ujumla.”
“Pia, utafungua fursa mpya za biashara na kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika soko la kimataifa,” amesema Chongolo.
Ameeleza ushirikiano huo utaisaidia Tanzania kutekeleza kwa ufanisi Dira ya Kilimo ya 2050 na Ajenda ya 10/30, inayolenga kukuza sekta ya kilimo kwa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030.
Chongolo, amesema makubaliano hayo pia yatafungua fursa zaidi za uwekezaji katika uchakataji wa mazao na biashara ya kilimo, hatua itakayoongeza thamani ya mazao na mapato kwa wakulima.
Kwa upande wake, Bekir Gezer, ameishauri Tanzania kuhakikisha miradi inayotekelezwa na Wakala wa Ushirikiano na Maendeleo wa Uturuki (Tika) inanufaisha moja kwa moja wakulima kwa kuboresha mazingira ya uzalishaji na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Amesema matumizi sahihi ya miradi hiyo yatasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wakulima, kuongeza uzalishaji na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujikita katika shughuli za kilimo.
Gezer, ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi kati ya mataifa hayo mawili, akisema hatua hiyo itafungua fursa mpya za uwekezaji kutoka Uturuki katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, uvuvi, nishati na biashara.















