Vyuo vikuu nchini vinapaswa kuifanya agenda ya umataifishaji kuwa sehemu ya mikakati yake ya msingi kwa kuijumuisha katika ufundishaji, utafiti, ubunifu na huduma kwa jamii ili kuongeza ushindani wa kimataifa, kupanua fursa za elimu na ajira kwa vijana pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Prof. Maulilio Kipanyula wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa wa Kuimarisha Mikakati ya Umataifishaji wa Elimu ya Juu Juni 19, 2026 katika kampasi ya NM-AIST jijini Arusha, ukiwakutanisha wataalamu wa sekta ya elimu kutoka ndani na nje ya Tanzania kujadili mustakabali wa elimu ya juu nchini.
Prof. Kipanyula ameeleza kuw umataifishaji wa elimu ya juu una mchango mkubwa katika kuongeza ubora wa elimu na tafiti, kuvutia wanafunzi na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuwaandaa wahitimu wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira la dunia.
Aidha, aliipongeza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuandaa mkutano huo na kutambua mchango wa Mradi wa TANZIE katika kuimarisha uwezo wa taasisi za elimu ya juu kupitia ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya Tanzania na Ulaya.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amesema mkutano huo unatoa jukwaa muhimu la kujadili masuala ya sera, rasilimali fedha na ushirikiano wa kimataifa, huku ukitarajiwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha utekelezaji wa agenda ya umataifishaji nchini.
Mkutano huo umeandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kupitia Mradi wa TANZIE unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuongeza uwezo wa taasisi za elimu ya juu nchini.














