IRINGA: KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Taifa, Kenani Kihongosi amewataka wazazi na walezi kuvitambua na kuviendeleza vipaji vya watoto wao tangu wakiwa wadogo, ili wapate mwongozo sahihi wa kufikia ndogo zao.
Kihongosi ameeleza hayo leo Juni 20,2026 aliposhiriki kikao katika shina Namba 10 Kata ya Kihesa mkoani Iringa ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika mkoa huo.

Akizungumza hayo Kihongosi amesema wazazi wanapaswa kuzingatia viashiria vya uongozi na vipaji vinavyojitokeza kwa watoto wao badala ya kuvipuuzia, kwani viongozi na wataalamu wengi huanza kuonesha uwezo wao mapema lakini hukosa watu wa kuwaongoza kufikia ndoto zao.

“Wazazi na walezi mna wajibu wa kuwatambua watoto wenu wana vipaji gani na kuwasaidia kuvikuza. Wapo watoto wenye uwezo mkubwa lakini wanahitaji mtu wa kuwaongoza na kuwapa moyo ili wafikie malengo yao,” amesema Kihongosi.
Ameongeza kuwa historia yake ya uongozi ilianzia katika Kata ya Kihesa alikokulia na kusoma shule ya msingi, ambapo aliwahi kuwa kiongozi wa darasa kabla ya kuendelea na majukumu mbalimbali ya uongozi yaliyomfikisha katika nafasi aliyonayo sasa.

“Mtoto anaporudi nyumbani akisema ni monita wa darasa, usione ni jambo dogo, huenda hicho ndicho kiashiria cha kipaji na uwezo ambao Mungu amemjalia, wajibu wa kukilea na kukiendeleza kipaji cha mtoto ni wa mzazi na mlezi,” amesisitiza.













