Dar es Salaam. Rais wa Namibia, Dk Natumbo Nandi Ndaitwah amesema umefika wakati kwa mataifa ya Afrika kuingia katika hatua mpya ya kujitegemea kiuchumi kwa kuimarisha uzalishaji wa ndani, viwanda na biashara ya kikanda badala ya kutegemea masoko ya nje.
Rais Nandi Ndaitwah yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu iliyoanza jana Juni 19 hadi 21, 2026, kufuatia mwaliko rasmi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Ziara hii inafanyika katika kipindi muafaka ambacho Tanzania na Namibia zinajenga mustakabali mpya juu ya misingi yao imara ya kihistoria.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Namibia, Dk Netumbo Nandi-Ndaitwah wakati wakishuhudia utiaji saini wa Hati nne za Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta za biashara, maendeleo ya biashara ndogo na za kati; Ulinzi, pamoja na Ushirikiano wa miji kati ya Manispaa ya Mji wa Zanzibar na Manispaa ya Swakopmund kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Uhusiano wa nchi hizi ulizaliwa tangu zama za harakati za ukombozi wa Afrika, ukaimarika kupitia urafiki wa muda mrefu na sasa unaendelea kushamiri katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Juni 20, 2026, katika jukwaa la biashara kati ya Tanzania na Namibia lililoandaliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Tiseza), Rais huyo amesema wakati umefika wa Afrika kuacha mfumo wa kusafirisha malighafi nje na kununua bidhaa zilizoongezwa thamani, akisisitiza kuwa mabadiliko hayo ndiyo njia ya kuleta ajira na maendeleo ya kweli.
Amesema Afrika ina rasilimali watu, soko kubwa na ubunifu wa kutosha kujenga uchumi imara, lakini bado haijatumia kikamilifu fursa hizo.
Alibainisha kuwa hata alipokuwa akisafiri kutoka uwanja wa ndege aliona shughuli nyingi za kiuchumi mitaani, akisema hiyo ni ishara ya soko kubwa la ndani linalohitaji kuendelezwa.
“Mustakabali wa Afrika lazima uongozwe na bidhaa za ndani, viwanda vya Afrika na matumizi ya masoko ya Afrika yenyewe. Utegemezi wa masoko ya nje umedhoofisha ukuaji wa viwanda na kupunguza kasi ya ajira kwa vijana,” amesema.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Namibia, Dk Netumbo Nandi-Ndaitwah wakati wakishuhudia utiaji saini wa Hati nne za Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta za biashara, maendeleo ya biashara ndogo na za kati; Ulinzi, pamoja na Ushirikiano wa miji kati ya Manispaa ya Mji wa Zanzibar na Manispaa ya Swakopmund kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Amesema Mkataba wa Biashara Huria wa Afrika (AfCFTA) na Ajenda 2063 vinatoa fursa ya kihistoria ya kuunganisha bara kuwa soko moja lenye nguvu, akisisitiza kuwa fursa hiyo itafikiwa tu endapo nchi za Afrika zitawekeza katika uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa.
Akizungumzia Tanzania na Namibia, amesema nchi hizo zina nafasi kubwa ya kushirikiana katika sekta za kilimo, madini, viwanda, utalii, nishati na usafirishaji. Alisema Tanzania ina soko kubwa na miundombinu inayokua, huku Namibia ikiwa na rasilimali na fursa za viwanda vya kuongeza thamani.
Amesema upo umuhimu wa kuunganisha bandari za Dar es Salaam na ile ya Walvis Bay ili kuimarisha biashara kati ya Afrika Mashariki na Kusini, akisema usafirishaji ni mhimili wa ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda.
“Dunia inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia na kuibuka kwa viwanda vipya, hivyo Afrika haina muda wa kusubiri bali inapaswa kuchukua hatua sasa ili kuepuka kubaki nyuma,” alisisitiza.
Alisema mafanikio ya ushirikiano wa kiuchumi hayatapimwa kwa takwimu pekee, bali kwa ajira zitakazoundwa, ujuzi utakaohamishwa na maisha ya wananchi yatakayoboreshwa.
Alisisitiza kuwa vizazi vijavyo vinapaswa kuikuta Afrika ikiwa imejenga uchumi wa uzalishaji badala ya utegemezi, na ushirikiano badala ya migogoro.
Alisema historia haitawahukumu viongozi wa Afrika kwa mikutano au matamko, bali kwa viwanda vitakavyojengwa na fursa zitakazofunguliwa kwa wananchi.
Rais huyo alihitimisha kwa kusisitiza kuwa mustakabali wa Afrika upo mikononi mwa Waafrika wenyewe, akitoa wito wa mshikamano wa kiuchumi na imani mpya ya kujenga uchumi wa bara hilo.
Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan amesema licha ya uhusiano mzuri wa kisiasa na kidiplomasia, ushirikiano wa kiuchumi uliopo kati ya Tanzania na Namibia bado haujaendana na kiwango cha mahusiano ya kihistoria, huku akisisitiza haja ya kuongeza kasi ya biashara na uwekezaji ili kunufaika na fursa zilizopo pande zote mbili.
Amesema Tanzania inaendelea kufanya maboresho ya mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia taasisi kama Tiseza, hatua ambayo imewezesha usajili wa kampuni kufanyika ndani ya muda mfupi wa hadi saa 24.
Samia aliitaja sekta ya bandari na usafirishaji kuwa nguzo muhimu ya ushirikiano wa kikanda, akieleza kuwa Tanzania ni lango la biashara kwa nchi sita zisizo na bandari na kwamba upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na miradi ya Bagamoyo na Mangapwani unafungua fursa kubwa za uwekezaji katika huduma za meli, usafirishaji na viwanda vinavyohusiana na logistiki.
“Katika sekta ya kilimo, Tanzania ina ardhi kubwa inayofaa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali,” amesema, akibainisha kuwa kuna fursa ya kuimarisha biashara ya chakula kati ya Tanzania na Namibia, ambapo Tanzania inaweza kusafirisha ziada ya mazao kama mpunga na mahindi kutokana na uwezo wake wa kuwa ghala la chakula katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Rais Samia pia alieleza kuwa sekta za mifugo na uvuvi zina nafasi kubwa ya ushirikiano, akibainisha kuwa Tanzania ina moja ya mifugo mingi zaidi barani Afrika, huku Namibia ikiwa imepiga hatua katika uzalishaji wa nyama na uvuvi, hivyo kuwepo kwa nafasi ya kubadilishana ujuzi, teknolojia na uwekezaji.
Katika sekta ya madini, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika rasilimali kama dhahabu, almasi, uranium na madini mengine ya kimkakati, akisema ushirikiano huo utaongeza thamani na tija kwa uchumi wa mataifa yote mawili kupitia uhamishaji wa ujuzi na uwekezaji wa pamoja.
Katika sekta ya nishati mbadala, amesema pia ina nafasi kubwa ya uwekezaji kutokana na uwepo wa rasilimali za jua, upepo na gesi, akisisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na wawekezaji katika kuharakisha mpito wa nishati safi.
“Kwenye utalii, Tanzania na Namibia ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa vivutio vya safari barani Afrika, hivyo kuna fursa ya kushirikiana katika uuzaji na utangazaji wa pamoja wa vivutio hivyo, ikiwemo kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja za anga kati ya nchi hizo mbili,” amesema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kukuza lugha ya Kiswahili kama daraja la mawasiliano ya kiuchumi na kijamii, akikipongeza Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na taasisi za Namibia ambazo tayari zimeanza kufundisha lugha hiyo, akisema inaweza kuwa nyenzo ya kuimarisha biashara ndogo na za kati.
“Sisi kama Serikali tumejipanga kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili yawe ya uhakika, ya kutabirika na rafiki kwa wawekezaji wa muda mrefu,” amesema.
Mataifa hayo yamesaini hati nne za makubaliano ya ushirikiano katika sekta za biashara, ulinzi na ukuzaji wa miji ya Zanzibar kwa upande wa Tanzania na Swakopmund nchini Namibia.
Pia, imesainiwa hati ya makubaliano ya ushirikiano katika maendeleo ya biashara ndogo na za kati kati ya Serikali za Tanzania na Namibia.
Hati nyingine ya makubaliano iliyosainiwa ni kuhusu ushirikiano katika sekta ya ulinzi kati ya Tanzania na Namibia na mkataba wa ushirikiano wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar na Manispaa ya Swakopmund nchini Namibia.














