Dar es Salaam. Serikali imesema imejizatiti kulinda soko la ajira nchini na kuhakikisha Watanzania wananufaika na ongezeko la uwekezaji wa kigeni, huku ikiendelea kuimarisha ulinzi wa haki za wafanyakazi na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuongeza fursa za ajira nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Deus Sangu amesema hatua hiyo inaendana na juhudi za Serikali za kuhakikisha uwekezaji unaoingia nchini unachangia utoaji wa ajira halisi na zenye staha kwa Watanzania, hususan vijana.
Kauli hiyo inakuja wakati zaidi ya makampuni 100 ya Kichina yakitoa zaidi ya nafasi 1,000 za ajira kupitia Maonesho ya Tano ya Ajira ya Tanzania na China.
Maonesho hayo yameandaliwa na Ubalozi wa China nchini Tanzania kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara wa China Tanzania (China Enterprises Association in Tanzania) pamoja na Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akizungumza kabla ya ufunguzi wa maonesho hayo yanayofanyika jana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sangu alisema tukio hilo linaonyesha kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China na kutoa jukwaa muhimu la kuwaunganisha vijana wa Kitanzania na waajiri kutoka sekta mbalimbali za uchumi.
“Serikali, kupitia maonesho haya ya tano ya ajira ya Tanzania na China, imejidhatiti kuhakikisha soko la ajira nchini linalindwa huku uwekezaji unaokua kutoka nje ukileta ajira halisi na zenye staha kwa Watanzania, hususan vijana,” alisema.
Aliongeza: “Kwa vijana wote wanaotafuta ajira, huu ni wakati wenu. Kuweni makini, jiwekeni tayari na amini uwezo wenu.”
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisema Maonesho ya Ajira ya Tanzania na China ni ishara ya uhusiano wa muda mrefu wa urafiki na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, pamoja na kuwa jukwaa la kuwaunganisha moja kwa moja vijana wa Kitanzania na waajiri.
Alisema mpango huo unaonyesha dhamira ya China kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Tanzania, hususan katika kuongeza ajira kwa vijana na kuimarisha ubadilishanaji wa ujuzi katika sekta muhimu za uchumi.
“Ushirikiano huu unachangia ukuaji wa pamoja na manufaa kwa pande zote mbili,” alisema.
Katibu wa Chama cha Wafanyabiashara wa China Tanzania, Juma Sharobaro, alisema maonesho hayo yanaonyesha ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi za Tanzania na China katika kukuza ajira na maendeleo ya rasilimali watu.
Alisema kampuni zinazoshiriki zinatoka katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi na uhandisi, madini, teknolojia, usafirishaji na ugavi wa mizigo, vyombo vya habari na utamaduni, viwanda, nishati pamoja na mawasiliano.
Kwa mujibu wake, maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kuwa makubwa zaidi tangu kuanzishwa kwake, yakileta pamoja zaidi ya makampuni 100 ya Kichina yanayofanya biashara nchini Tanzania na kutoa zaidi ya nafasi 1,000 za ajira kwa vijana wa Kitanzania.
Sharobaro alisema mbali na kutoa ajira, maonesho hayo yanawapa vijana fursa ya kupata uzoefu wa mazingira ya kazi ya kimataifa na kuimarisha ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Maonesho hayo ya kila mwaka yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza ajira, uhamishaji wa ujuzi na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China, huku waandaaji wakitarajia mwitikio mkubwa wa watafuta ajira kutoka maeneo mbalimbali nchini.















