Dar es Salaam. Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wameungana kutoa elimu na huduma ya upatikanaji wa viambatanisho kwa waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Shughuli hiyo inafanyika katika mikoa mbalimbali ikiwamo Mbeya, Dar es Salaam, Kagera, Kilimanjaro, Tabora na Zanzibar (Unguja na Pemba), ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia wanafunzi na wadau kupata taarifa sahihi kuhusu mchakato wa maombi ya mikopo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Meneja wa HESLB Kanda ya Ziwa, Usama Choka amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha waombaji wote wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.
“Tunawakaribisha wanafunzi, wazazi na wadau wote kujitokeza katika vituo hivi ili kupata elimu sahihi kuhusu uombaji wa mikopo ya elimu ya juu na vyuo vya kati, kwani lengo letu ni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa taarifa muhimu,” amesema Choka.
Kwa upande mwingine, TASAF imesema ushiriki wake katika shughuli hiyo unatokana na mkataba wa maelewano uliopo kati yake na HESLB, unaolenga kusaidia watoto kutoka kaya maskini kupata fursa ya elimu ya juu kwa kuwapatia mikopo yenye ufadhili wa asilimia 100.
“Ushirikiano huu ni sehemu ya dhamira yetu ya kuhakikisha watoto wa kaya maskini wanaendelea kupata fursa ya elimu ya juu bila vikwazo vya kifedha, kupitia mfumo uliowekwa kwa ushirikiano na HESLB, kwa kuwa kupata elimu ya chuo kikuu ni moja ya njia za kuondokana na umaskini,” imeeleza TASAF.
Baadhi ya wanafunzi waliofika katika vituo hivyo wameeleza kufurahishwa na huduma hiyo, wakisema imewasaidia kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu hatua za maombi ya mikopo na vigezo vinavyotumika.
“Huduma hii imetusaidia kupata majibu ya maswali yetu kwa wakati na kutuondolea hofu kuhusu namna ya kuomba mikopo kwa usahihi na kwa wakati. Tunawasihi wanafunzi wenzetu wote wanaotarajia kuomba mikopo wafike kupata elimu hii ili kupunguza changamoto wakati wa maombi utakapofika,” amesema mmoja wa wanafunzi waliohudhuria kituoni hapo.
Mbali na Mwanza, HESLB imeandaa vituo vingine vya utoaji elimu katika mikoa ya Dodoma, Tabora, Mbeya, Arusha, Mtwara, Kilimanjaro, Kagera na Morogoro kwa lengo la kuwafikia waombaji wengi zaidi na kutoa elimu ya kina kuhusu utaratibu wa maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo ujao.
Ushirikiano wa TASAF na HESLB unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa watoto wa kaya maskini, huku taasisi hizo zikisisitiza kuwa elimu sahihi kwa waombaji ni msingi wa kuhakikisha wanufaika wanafikia huduma hiyo kwa usahihi, kwa wakati na kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.















