Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema Tanzania haina taarifa ya uwepo wa raia wake yeyote nchini Cambodia.
Kauli hiyo ya Balozi Kombo imetokana na taarifa ya Serikali ya Kifalme ya Cambodia iliyowataka raia wote wa mataifa ya Afrika wanaoishi nchini humo kuhakikisha kabla au ifikapo Mei 31, 2026 wawe wameondoka.
Taarifa hiyo imeyataja mataifa ya Ghana, Kenya, Cameroon, Uganda na mengineyo, ikisisitiza kuwa atakayekamatwa baada ya Mei 31 atatozwa faini ya Dola za Marekani 8,000 (zaidi ya Sh21 milioni), sambamba na kifungo cha miaka miwili jela.
Balozi Kombo ameeleza hayo leo, Ijumaa Mei 29, 2026, alipozungumza na Mwananchi kuhusu taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uhamiaji nchini Cambodia, Luteni Jenerali Som Sopheak.
Amesema Tanzania haina taarifa ya uwepo wa raia wake yeyote nchini Cambodia na bado Serikali haijapata taarifa rasmi ya kidiplomasia kuhusu tangazo hilo.
“Hatuna uhusiano wa karibu zaidi na Cambodia. Hata balozi anayewakilisha kule ni balozi wetu nchini Malaysia na Indonesia, wote bado hawajapata taarifa,” amesema.
Amesisitiza hata wao wameiona taarifa hiyo kupitia mitandao ya kijamii.
Alipoulizwa kuhusu panya waliowahi kupelekwa nchini humo, Balozi Kombo amesema walipelekwa kwa mradi wa majaribio uliokuwa chini ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).
Hata hivyo, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi kubwa, lakini yenye watu wachache zaidi wanaoishi nje yaani diaspora, kwa sababu wengi wanafurahishwa na kuishi ndani ya taifa lao.
“Diaspora wa nje wako wengi zaidi nchini Tanzania kuliko Watanzania walioko nje. Kwa mfano, Waitaliano hapa Tanzania wapo 4,800, lakini raia wa Tanzania waliopo Italia ni 500 tu,” amesema.
Ameeleza vivyo hivyo hata kwa raia wa mataifa mengine kama Marekani, wengi wapo nchini, lakini Watanzania waliopo huko ni wachache zaidi.
Katika taarifa yake, Luteni Jenerali Sopheak amewataka raia wote wa Afrika kutoka Ghana, Kenya, Cameroon, Uganda na mataifa mengine kuwa muda wa msamaha wa kusalia nchini humo waliokuwa wamepewa utaisha rasmi Mei 31, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, raia wote wa kigeni ambao tayari wamelipa faini zao wanapaswa kuondoka nchini Cambodia kabla au ifikapo Mei 31, 2026.
Serikali hiyo imeonya kuwa kuanzia Juni 1, 2026, mgeni yeyote atakayekutwa akiingia, kuendelea kuishi au kuwepo nchini Cambodia kinyume cha sheria atakamatwa katika uwanja wa ndege au eneo lolote atakalobainika.
Aidha, mtu atakayekamatwa atatumikia kifungo cha miaka miwili jela na kulipa faini ya dola 8,000 za Marekani (zaidi ya Sh21 milioni) kabla ya kuruhusiwa kuondoka nchini humo.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa Polisi wa Cambodia wataanza operesheni ya kuwakamata wageni wanaoishi mafichoni au waliokiuka sheria za uhamiaji kuanzia Juni 1, 2026, na kuwapeleka kwa mamlaka za uhamiaji kwa hatua zaidi za kisheria.
Serikali ya Cambodia imesisitiza kuwa haitavumilia ukiukwaji wowote wa sheria zake za uhamiaji na imewataka wote wanaohusika kuzingatia kikamilifu maelekezo yaliyotolewa.















