Dar es Salaam. Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) umedai kuwa,Sh227 milioni za fidia katika Msikiti wa Rahman uliopo Mtaa wa Jangwani jijini Dar es Salaam zililipwa kwa watu wasio sahihi ili kupisha mradi wa uendelezaji bonde la Mto Msimbazi
Hayo yamesemwa jana Jumamosi, Mei 23, 2026 na mratibu wa mradi huo kutoka Tarura, Humphrey Kanyenye alipozungumza na Mwananchi baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa waumini wa msikiti huo.
Mradi huo unaofadhiliwa na benki ya dunia, zilitengwa Sh52 bilioni kwa ajili ya ulipaji fidia ambapo nyumba 2500 ziliweza kufidiwa.
Malengo ya kufanyika kwa mradi huo uliopo chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ni kukabiliana na mafuriko na kuboresha matumizi ya ardhi katika eneo la chini la bonde.
Hata hivyo, wakati nyumba nyingi zikiwa zimeshabomolewa msikiti huo wa Rahman bado upo ukichochewa na mgogoro huo wa waumini wake.
Kanyenye ameiambia Mwananchi kuwa wamebaini fedha zililipwa kwa watu wasio sahihi na wanajiandaa kuzikutanisha pande hizo mbili.
Amesema waliozichua watapaswa kuzirejesha la sivyo itabidi sheria ifuate mkondo wake kwa kuwa huo ni utapeli kama utapeli mwingine.
“Tayari suala hili tunalishughulikia baada ya kubaini kuwepo kwa changamoto katika kulitekeleza, hivi karibuni kwa kukutanisha pande zote mbili,” amesema Kanyenye.
Hata hivyo, amesema pamoja na kutolewa wa fedha hizo, mpango ulioamuliwa ni kujengwa kwa msikiti mwingine.
“Hapa Jangwani mbali na kuwepo kwa makazi ya watu, kutakuwa na masoko mawili ikiwamo soko la wamachinga na lile la Kigogo Sambusa, hivyo kuna uhitaji wa msikiti ili watu waweze kwenda kuswali,” amesema Kanyenye.
Alichosema Imamu wa Msikiti
Akielezea ilivyokuwa, Imamu wa msikiti huo, Sheikh Hassan amesema upande wa pili wa masheikh wenzao baada ya kusikia kuna hela italipwa ya fidia walikwenda kufungua akaunti nyingine bila kuushirikisha msikiti na kutuma nyaraka Tarura ambao ndio wasimamizi wa mradi huo wamelipa Sh227 milioni.
Amesema wamefanya hivyo wakati msimamo wa waumini hawakutaka kulipwa fedha bali walitaka kujengewa msikiti mbadala katika eneo hilohilo, lakini kwa bahati mbaya wenzao walizunguka mlango wa nyuma kuweza kupokea hela hizo.
“Sisi tulihitaji kujengewa msikiti eneo hilihili la mradi kwa kuwa kama ni waumini bado wapo, hata soko la kisasa la wamachinga likijengwa hapa, makazi ya watu, ni wazi watahitaji eneo la kuswalia, lakini wenzetu haya yote hawakuayaona wakataka hela tena ambayo wameichukua kinyume na utaratibu,” amesema Hassan.
Masheikh wanaotuhumiwa kuchukua fedha hizo ambao katika kundi lao wapo saba wamekiri kuzichukua na kueleza akaunti walioifungua ni ya msikiti pia baada ya wenzao kutotaka kuwapa ushirikiano.
Kiongozi wa masheikh hao, Khatib Mtali amesema fedha hizo zipo salama na wanatarajia kujenga msikiti maeneo ya Kivule.
Alipoulizwa kwa nini wanajenga mbali na ulipo msikiti, Mtali amesema ni kutokana na hapo Jangwani wakazi wote wameshaondolewa hivyo hakuna muumini wa kwenda kuswali hapo.
Kuhusu kutowashirikisha wenzao, Mtali amesema ilikuwa ni ngumu kwa kuwa walishawatisha hata katika msikiti huo wasiende kuswali.
Waumini wakiwa wanaingia katika Msikiti wa Rahman ambao masheikh wanadaiwa kuchukua fidia yake kinyume cha sheria.
Pia, walipoitwa mara kadhaa kwa ajili ya kusuluhishwa katika ofisi ya Sheikh wa Wilaya aliyekuwa akisimamia kusuluhisha mgogoro huo hawakutokea kwa kile walichodai hawana imani naye na kutaka suala hili liende kwa Sheikh wa Mkoa.
Sheikh wa Wilaya, Adam Mwinyimbingu amekiri kufahamu mgogoro huo na kueleza alifanya kila njia ya kukutanisha pande mbili bila mafanikio.
Hata hivyo, Sheikh Mwinyimbingu amesisitiza fedha zilizolipwa zipo salama na kueleza atahakikisha anazisimamia kuhakikisha zinafanyiwa lile lililokusudiwa.
Naye Sheikh wa Mkoa, Sheikh Walid Alhad Omari, alipotafuta kuhusiana na suala hilo, amesema analijua ila walimuachia sheikh wa wilaya kulishughulikia.














