Na John Bukuku, Dar es Salaam,
Juni 18, 2026 – Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wanawake, Raymond Mushumbusi Ishengoma, amesema waandaaji na watangazaji wa vipindi vya watoto nchini wanapaswa kuzingatia viwango vya kitaaluma, maadili ya uandishi wa habari na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuhakikisha watoto wanapata maudhui bora yanayochangia maendeleo yao.
Amesema hayo wakati wa semina ya mafunzo kwa waandaaji na watangazaji wa vipindi vya watoto inayofanyika kwa siku ya pili katika Ukumbi wa AFED jijini Dar es Salaam.
Ishengoma amesema vipindi vya watoto vinapaswa kuandaliwa kwa kuzingatia umri na hatua za ukuaji wa watoto ili viweze kukidhi mahitaji yao ya elimu na burudani.
Amesema watoto wa makundi tofauti ya umri wana mahitaji tofauti ya maudhui, hivyo ni muhimu kwa waandaaji kufanya utafiti wa kina kabla ya kuandaa vipindi ili kuhakikisha mada zinazowasilishwa zinaendana na uwezo wa watoto kuelewa na kujifunza.
Amesema vipindi vya watoto vinahitaji ubunifu mkubwa, matumizi ya lugha rahisi na maudhui yanayovutia watoto, huku elimu, michezo, nyimbo, hadithi na mafunzo ya maadili vikipewa nafasi muhimu katika vipindi hivyo.
Aidha, amesema ni muhimu kulinda haki za watoto katika vipindi na taarifa za habari kwa kuhakikisha watoto hawafichuliwi kwa namna inayoweza kuwaweka katika mazingira hatarishi au kuvunja faragha zao.
Ishengoma amesema waandishi wa habari wanapaswa kuhakikisha taarifa wanazozitoa kwa watoto ni sahihi, zenye ukweli na zisizo na maudhui ya ukatili, ubaguzi au yanayoweza kuathiri maendeleo yao.
Pia amesema ushirikishwaji wa watoto katika vipindi mbalimbali unaweza kusaidia kujenga kujiamini na kukuza vipaji vyao, huku akibainisha kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimefanikiwa kuwajengea watoto uwezo wa kujitokeza na kuendelea katika taaluma ya utangazaji.
Kuhusu changamoto zilizopo, amesema uhaba wa wataalamu waliobobea katika uandaaji wa vipindi vya watoto, gharama za uzalishaji wa maudhui bora na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ni baadhi ya masuala yanayohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Ishengoma amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya habari katika kutoa mafunzo kwa waandishi, watangazaji na waandaaji wa vipindi ili kuimarisha ubora wa maudhui yanayolenga watoto.
“Teknolojia hatuwezi kuikimbia, tunapaswa kuitumia kuongeza ubunifu na ubora wa vipindi vyetu huku tukizingatia maadili, tamaduni na sheria za nchi,” amesema.
Semina hiyo imewakutanisha waandaaji na watangazaji wa vipindi vya watoto kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kwa lengo la kujengeana uwezo kuhusu maadili ya taaluma, ubunifu wa maudhui na matumizi ya teknolojia za kisasa katika utayarishaji wa vipindi vya watoto.














