Wajane wahimizwa kujiimarisha kiuchumi | Mwananchi

Morogoro. Mwenyekiti wa Chama cha Wajane Mkoa wa Morogoro (CCWT), Dorothy Mwamsiku, amewataka wajane kujishughulisha na shughuli halali za kiuchumi ili kumudu maisha yao na kuwalea watoto walioachiwa na waume zao. Ameyasema hayo mkoani Morogoro leo Ijumaa Juni 19, 2026, wakati wa kongamano la wajane lililofanyika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani Juni 23…

admin Avatar

by

2 minutes

Read Time

Morogoro. Mwenyekiti wa Chama cha Wajane Mkoa wa Morogoro (CCWT), Dorothy Mwamsiku, amewataka wajane kujishughulisha na shughuli halali za kiuchumi ili kumudu maisha yao na kuwalea watoto walioachiwa na waume zao.

Ameyasema hayo mkoani Morogoro leo Ijumaa Juni 19, 2026, wakati wa kongamano la wajane lililofanyika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani Juni 23 mwaka huu.

Amesema kufiwa na mwenza si laana wala mkosi, bali ni sehemu ya maisha, hivyo wanawake waliobaki na jukumu la kulea watoto wanapaswa kuwa imara na kutokata tamaa.

“Mwanamke kufiwa na mume si laana wala mkosi. Mama aliyeachiwa watoto anatakiwa kutambua kuwa sasa ndiye mlezi mkuu wa familia. Ni muhimu kupambana kwa kufanya shughuli halali za kujipatia kipato ili kuwahudumia na kuwalea watoto vizuri,” amesema.

Dorothy, amesisitiza si vyema kwa wajane kukimbilia kuwaachia ndugu jukumu la kulea watoto wao bila sababu za msingi, akieleza kuwa mama ndiye mwenye nafasi kubwa ya kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na kukua katika maadili mema.

“Mama akiteleza katika majukumu yake, watoto nao wanaweza kuyumba na kuingia katika vitendo visivyofaa kama matumizi ya dawa za kulevya, ulevi au uhalifu. Hivyo ni muhimu wajane kusimama imara na kutimiza wajibu wao wa malezi,” amesema.

Pia, amewataka wajane kuepuka mikopo yenye masharti kandamizi maarufu kama ‘kausha damu’, akisema imekuwa chanzo cha matatizo kwa wanawake wengi.

Badala yake, amewashauri kutumia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Serikali imeweka mifumo mizuri ya kuwawezesha wanawake kiuchumi. Wajane wanapaswa kutumia fursa hizi rasmi badala ya kuingia kwenye mikopo inayoweza kuwaingiza kwenye matatizo zaidi,” amesema.

Dorothy, amewahamasisha wajane kujiunga na chama hicho ili kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi, kubadilishana uzoefu na kusaidiana katika changamoto za maisha.

Kwa upande wake, Katibu wa CCWT Wilaya ya Morogoro, Fatuma Thabiti, amewataka wajane kuwa makini na baadhi ya wanaume wanaowafuata kwa madai ya kutaka kuwaoa huku wakilenga kunufaika na mali walizoachiwa.

“Kuna wanaume ambao huvutiwa na mali za wajane na siyo upendo wa kweli. Ni muhimu wajane kuwa waangalifu ili wasiingizwe kwenye mahusiano yatakayowasababishia kupoteza mali zao,” amesema Fatuma.

Mmoja wa wajane waliohudhuria kongamano hilo, Anuni Jafari, amesema wajane wanapaswa kutambua wajibu wao wa kulea watoto na kuendeleza mali walizoachiwa badala ya kuziacha zipotee.

Amesema baada ya kufiwa na mumewe alijitahidi kulea watoto wake na kuanzisha biashara iliyomwezesha kujitegemea kiuchumi.

“Mume wangu alinichia nyumba, pia nilijituma na kuanzisha biashara yangu mwenyewe. Leo watoto wangu wamekua na ninaendelea na maisha yangu kwa kujitegemea,” amesema.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports