NA DENIS MLOWE,IRINGA
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, amesema serikali imejipanga kuhakikisha michezo na sanaa zinaendelea kupewa nafasi kubwa katika mfumo wa elimu nchini, akisisitiza kuwa shughuli hizo hazitaondolewa tena shuleni kwa kuwa ni sehemu muhimu ya kukuza vipaji, afya, ajira na ushindani wa kimataifa.
Waziri Mkenda alitoa kauli hiyo wakati akifungua rasmi Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) 2026 yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Lugalo mkoani Iringa.
Katika hotuba yake, Waziri Mkenda aliushukuru Mkoa wa Iringa kwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, akisema mkoa huo umeendelea kuwa kivutio kutokana na mazingira yake mazuri na ukarimu wa wananchi wake.
“Tunafurahi sana kuja Iringa tunawashukuru viongozi na wananchi wote wa Iringa kwa kutupokea na kuwa wenyeji wa mashindano haya muhimu kwa maendeleo ya michezo nchini,” alisema.
Aidha, aliwapongeza wanafunzi, walimu na viongozi wa michezo waliofanikiwa kufika katika hatua ya taifa baada ya kushinda katika ngazi mbalimbali kuanzia shule, kata, wilaya na mikoa.
Waziri Mkenda alitoa pongezi kwa sekretarieti ya mashindano pamoja na wizara na taasisi zilizoshiriki katika maandalizi ya UMISSETA, akitaja Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Akizungumzia nafasi ya michezo katika maendeleo ya taifa, Mkenda alisema michezo ni zaidi ya burudani kwani ni chanzo cha afya bora, mshikamano wa jamii, ajira na fursa za biashara.
Alisema shule zinapaswa kuendelea kuwa viwanda vya kuzalisha na kukuza vipaji vya wanafunzi katika michezo na sanaa, huku akisisitiza kuwa sera ya elimu inatambua rasmi umuhimu wa kubaini na kuendeleza vipaji mbalimbali mapema.
“Kupitia sera ya elimu, serikali imeweka wazi kuwa itaendelea kubaini na kuendeleza wanafunzi wenye vipaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo michezo, sanaa, sayansi na teknolojia,” alisema.
Mkenda alieleza kuwa michezo na sanaa za maonyesho zimeingizwa rasmi katika mafunzo ya amali, sambamba na sekta nyingine kama kilimo, uvuvi na ufundi, hatua inayolenga kuwajengea wanafunzi ujuzi na uwezo wa kujitegemea.
Akihamasisha wanafunzi kushiriki kwa bidii katika mashindano hayo, Waziri Mkenda alisema kaulimbiu ya UMISSETA 2026 inayosema “Michezo na Sanaa, Shule ni Daraja la Ajira, Afya na Ushindani wa Kimataifa” inapaswa kuwapa hamasa ya kuangalia mbali zaidi ya mashindano ya ndani.
Alisema Tanzania ina kila sababu ya kuamini kuwa siku zijazo inaweza kufuzu na kushiriki Kombe la Dunia kupitia uwekezaji unaoendelea kufanyika katika michezo ya shule na maendeleo ya vipaji vya vijana.
“Ninaamini baadhi ya watakaocheza Kombe la Dunia katika miaka ijayo wanaweza kuwa miongoni mwa wanafunzi waliopo hapa leo. Hivyo mshiriki mashindano haya kwa bidii, nidhamu na kujituma,” alisema.
Aliwataka washiriki wote kuzingatia usalama, maadili na uadilifu wakati wote wa mashindano, akisisitiza kuwa mafanikio ya michezo yanategemea nidhamu na kuheshimu sheria na taratibu.
Kwa upande mwingine, aliipongeza hatua ya kuwapa wanafunzi nafasi ya kusimamia michezo kama waamuzi, akisema jambo hilo linasaidia kujenga kizazi cha wataalamu wa michezo wenye weledi na uwezo wa kusimamia mashindano kwa haki.
Mashindano ya UMISSETA 2026 yamewakutanisha wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo na sanaa vinavyoweza kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kikanda na kimataifa.












