Dar es Salaam. Katika kile kinachotafsiriwa kama diplomasia inayotoka moyoni, Rais wa Namibia, Dk Netumbo Nandi-Ndaitwah, ameamsha furaha baada ya kutembelea eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam na kukumbuka nyumba aliyowahi kuishi miaka ya nyuma akipigania uhuru wa nchi yake kupitia Chama cha Swapo.
Ziara hiyo ya kipekee imevuta hisia za kihistoria, ikionyesha kwa vitendo mshikamano wa damu uliopo kati ya Tanzania na Namibia tangu enzi za harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika.
Rais Nandi-Ndaitwah alilakiwa kwa shangwe, vigelegele na nyimbo na wakazi wa Magomeni waliomfahamu fika kabla ya kuwa kiongozi mkubwa wa kitaifa.
Miongoni mwa walioguswa na ujio huo ni wenyeji wake wa zamani, wakiwamo Mama Salehe pamoja na mtoto wa marehemu Mama Salama, ambao walimtambua vyema kiongozi huyo tangu akiwa kijana mwanaharakati na mwakilishi wa Swapo nchini Tanzania.
Akizungumza kwa hisia na wakazi hao waliokusanyika, Rais wa Namibia hakuacha kutoa pongezi na shukurani za dhati kwa Serikali ya Tanzania na wananchi wake kwa moyo wa kipekee wa ukarimu waliouonyesha wakati wa miaka ya dhiki.
“Magomeni ni sehemu ya maisha yangu na ni sehemu ya msingi ya historia ya taifa langu la Namibia. Tanzania haikutupa tu hifadhi, bali ilitupa upendo wa kweli na jukwaa salama la kupigania uhuru wetu.
“Ziara yangu hapa leo ni ushahidi usiofutika wa urafiki wa dhati na mshikamano wa kweli wa Kiafrika,” alisisitiza Rais Nandi-Ndaitwah.
Baada ya kusalimiana na kubadilishana maneno ya faraja na majirani hao, kiongozi huyo alitembea na kuingia ndani ya nyumba hiyo aliyokuwa akiishi zamani.
Alipata fursa ya kukagua vyumba na maeneo mbalimbali yaliyomkumbusha changamoto, mikakati na maisha ya kishujaa ya miaka hiyo ya mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi wa kigeni.
Majirani hao walieleza kufurahi kwao kuona mtoto wao wa zamani amerudi akiwa Rais wa nchi, lakini bado hajasahau asili na watu waliomstiri.

















