Kahama. Watu sita wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa baada ya basi la abiria mali ya Kampuni ya OG Classic lililokuwa likitokea Kahama kwenda Geita kugonga lori kwa nyuma na kupinduka katika eneo la Wendele, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi, Juni 20, 2026 majira ya saa 12 asubuhi, ikihusisha basi hilo na lori lililokuwa likielekea Masumbwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea ajali hiyo na kusema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo ni mwendokasi wa dereva wa basi ambaye alijaribu kulipita lori bila kuchukua tahadhari.
Amesema wakati dereva huyo akijaribu kulipita lori, basi liligonga ukingo wa barabara na kisha kurudi kugonga tela la lori kabla ya kupinduka, hali iliyosababisha vifo na majeruhi.
“Dereva wa basi alipofika eneo la Wendele alilikuta lori ambalo nalo lilikuwa likielekea Masumbwe. Alijaribu kulipita bila kuchukua tahadhari huku akiwa katika mwendokasi, ndipo alipogonga ngema na kurudi kuligonga tela la lori kisha kupinduka,” amesema Kamanda Magomi.
Amesema waliofariki katika ajali hiyo ni wanaume wanne na wanawake wawili ambao bado hawajatambuliwa, huku miili yao ikihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama.
Aidha, amesema majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Kamanda Magomi amesema dereva wa basi, anayefahamika kwa jina la Chacha Bosco (35), alitoroka baada ya ajali hiyo na Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Amewataka madereva wa mabasi ya abiria kuzingatia sheria za usalama barabarani, akisema Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa wale watakaobainika kukiuka sheria na kuhatarisha maisha ya wananchi.
Baadhi ya majeruhi walieleza kuwa walikuwa wamemuonya dereva kuhusu mwendokasi kabla ya ajali kutokea.
Seni Bundala, mmoja wa majeruhi, amesema walikuwa wakilalamikia kasi ya dereva lakini hakuwasikiliza.
“Gari letu lilikuwa mwendokasi na abiria walikuwa wakilalamika kwa dereva lakini hakutaka kutusikiliza,” amesema.
Mwasi Duti, ambaye ni miongoni mwa majeruhi, amesema ajali hiyo imemsababishia majeraha makubwa ikiwemo kuvunjika mkono na kushonwa kichwani.
“Mwendokasi umesababisha nimekuwa mlemavu. Serikali ichukue hatua dhidi ya madereva wa aina hii ili wengine wajifunze, maana wamepoteza maisha ya watu wasiokuwa na hatia,” amesema.

















