Malezi ya watoto kwenye nyumba za kupanga

Dar es Salaam. Katika miji mingi nchini, maisha ya nyumba za kupanga yamekuwa sehemu ya kawaida ya familia nyingi. Hata hivyo, ukuaji wa miji, changamoto za kiuchumi na mabadiliko ya maisha, vimefanya watoto wengi wakue katika mazingira ya ujirani wa karibu, ambapo familia nyingi huishi pamoja ndani ya nyumba moja au eneo moja. Katika mazingira…

admin Avatar

by

4 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Katika miji mingi nchini, maisha ya nyumba za kupanga yamekuwa sehemu ya kawaida ya familia nyingi.

Hata hivyo, ukuaji wa miji, changamoto za kiuchumi na mabadiliko ya maisha, vimefanya watoto wengi wakue katika mazingira ya ujirani wa karibu, ambapo familia nyingi huishi pamoja ndani ya nyumba moja au eneo moja.

Katika mazingira haya, mtoto hulelewa si tu na wazazi wake, bali pia huathiriwa kwa kiwango kikubwa na watu wanaomzunguka kila siku.

Wataalamu wa saikolojia ya maendeleo ya mtoto wanasema mazingira ya mtaa na ujirani, yana mchango mkubwa katika kujenga tabia, maadili, lugha, mitazamo na hata malengo ya maisha ya mtoto.

Nasema hivyo kwa sababu mtoto hujikuta akijifunza kwa kuangalia, kusikiliza na kuiga yale anayoyaona kwa watu wazima na watoto wengine wanaomzunguka.

Mfano, katika nyumba za kupanga, watoto mara nyingi hukutana na watu wenye asili, tamaduni, tabia na mitazamo tofauti. Hali hii inaweza kuwa na manufaa makubwa ikiwa mazingira yanajengwa katika msingi wa heshima, ushirikiano na maadili.

Hapa mtoto anaweza kujifunza umuhimu wa kuishi na watu wa aina mbalimbali, kusaidiana, kuheshimu tofauti za wengine na kujenga uhusiano mzuri na majirani.

Hata hivyo, mazingira hayo hayo yanaweza kuwa chanzo cha changamoto endapo mtoto atakutana na mienendo isiyofaa.

Lugha chafu, ugomvi wa mara kwa mara, matumizi ya pombe na dawa za kulevya, vitendo vya ukatili au tabia za utovu wa nidhamu vinaweza kuathiri namna mtoto anavyofikiri na kutenda.

Mzazi unapaswa kukumbuka kwamba watoto wana uwezo mkubwa wa kuiga wanachokiona kuliko kusikiliza wanachoambiwa. Ndiyo maana mara nyingi tabia wanazoziona kila siku, hujengeka ndani yao kwa haraka zaidi.

Changamoto nyingine inayojitokeza katika maeneo mengi ya upangaji ni kupungua kwa muda wa wazazi kuwa karibu na watoto wao kutokana na majukumu ya kutafuta kipato. Wakati mwingine mtoto hutumia muda mwingi akiwa na marafiki au majirani kuliko akiwa na wazazi wake.

Hali hii inaweza kuongeza uwezekano wa kuathiriwa na shinikizo la rika na maadili yasiyoendana na yale anayofundishwa na wazazi wake ndani ya nyumba yao.

Lakini pamoja na changamoto hizo, wataalamu wanasisitiza kuwa mazingira pekee hayaamui hatima ya mtoto. Mchango wa mzazi bado ndio nguzo kuu katika malezi. Kile mzazi anachokifanya nyumbani kina uwezo mkubwa wa kupunguza au kuongeza athari za mazingira ya nje.

Kwanza, mzazi anapaswa kujenga mawasiliano ya karibu na mtoto. Watoto wanaopata nafasi ya kuzungumza kwa uhuru na wazazi wao huwa na uwezekano mkubwa wa kueleza changamoto wanazokutana nazo na kupata mwongozo sahihi.

Mazungumzo ya mara kwa mara huwasaidia pia wazazi kufahamu marafiki wa watoto wao, shughuli wanazoshiriki na mambo yanayowasumbua kutoka kwa majirani zake anaoishi nao kwenye nyumba hiyo ya kupanga.

Lakini pia ni muhimu kwa mzazi kuweka msingi imara wa maadili ndani ya familia. Heshima, ukweli, uwajibikaji, huruma na nidhamu vinapaswa kufundishwa kwa vitendo na si kwa maneno pekee.

Nasema hivyo kwa sababu watoto hujifunza zaidi kupitia mfano wa wazazi wao. Mzazi anayeheshimu watu wengine, anayetimiza wajibu wake na kuzungumza kwa staha huwa anatoa somo kubwa kwa mtoto kuliko maelekezo mengi ya maneno.

Lakini kitu kingine, wazazi wanashauriwa kufuatilia kwa karibu mazingira ya kijamii yanayomzunguka mtoto. Hii haimaanishi kumzuia mtoto kushirikiana na wengine, bali kujua anacheza na nani, anatumia muda wake wapi na ni shughuli zipi zinazomjenga au kumharibu. Uangalizi huu unapaswa kwenda sambamba na kujenga imani kati ya mzazi na mtoto.

Wataalamu wanahimiza wazazi kushirikiana na majirani katika kulinda ustawi wa watoto. Ujirani mwema unaweza kuwa rasilimali muhimu katika malezi. Wazazi wanapofahamiana na kushirikiana, huwa rahisi kubaini changamoto zinazoweza kuwaathiri watoto na kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja.

Aidha, ni muhimu pia kuwajengea watoto uwezo wa kufanya uamuzi sahihi hata wanapokuwa mbali na wazazi wao.

Badala ya kutegemea uangalizi wa muda wote, watoto wafundishwe kutambua mema na mabaya, kukataa ushawishi hasi na kuwajibika kwa matendo yao.

Kwa ujumla, maisha katika nyumba za kupanga si hukumu ya kupata au kukosa malezi bora kwa watoto. Kinachobeba uzito zaidi ni namna familia inavyojenga msingi wa maadili na uhusiano wa karibu na watoto.

Ingawa mtaa na ujirani vinaweza kuwa na ushawishi mkubwa katika tabia za mtoto, mzazi mwenye uangalizi, mawasiliano mazuri na mfano mwema, ana nafasi kubwa ya kumlea mtoto mwenye maadili na uwezo wa kufanya uchaguzi sahihi katika mazingira yoyote anayokulia.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports