Michelle anavyomzungumzia Obama kama kiongozi, baba wa familia

Dar es Salaam. Maneno ya Michelle Obama aliyoyatoa katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Kumbukumbu za urais wa Barack Obama, si tu kumbukumbu ya kihistoria ya mapenzi ya kifamilia, bali pia ni kioo kinachoakisi nafasi ya baba katika familia, jamii na taifa. Katika hotuba hiyo iliyojaa hisia, Michelle amemuelezea mume wake, Barack Obama, kama…

admin Avatar

by

6 minutes

Read Time

Dar es Salaam. Maneno ya Michelle Obama aliyoyatoa katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Kumbukumbu za urais wa Barack Obama, si tu kumbukumbu ya kihistoria ya mapenzi ya kifamilia, bali pia ni kioo kinachoakisi nafasi ya baba katika familia, jamii na taifa.

Katika hotuba hiyo iliyojaa hisia, Michelle amemuelezea mume wake, Barack Obama, kama kiongozi aliyepitia misukosuko mikubwa ya kisiasa na kijamii, lakini akabaki imara bila kupoteza utu wake, dira wala maadili.

Maneno haya mazito ya Michelle yanakuja kipindi ambacho dunia inaadhimisha Siku ya Baba Duniani, ujumbe wa mama huyu si tu unagusa siasa na hadhi ya urais, bali unaleta swali muhimu, je, baba ni nani katika familia ya sasa?

Michelle anasisitiza kwamba Barack Obama hakuwahi kusahau mizizi yake mama mlezi aliyehangaika, babu na bibi waliomlea kwa upendo licha ya hali duni, pamoja na jamii ya Chicago iliyomjenga kupitia elimu, uanaharakati na maadili ya kazi.

Huu ni msingi wa baba bora anayejua alikotoka na anayejua anakoelekea.

Katika hotuba hiyo, Michelle anabainisha pia changamoto za kuwa “wa kwanza” kama rais mweusi wa Marekani ambapo mashinikizo, lawama na mashaka vilikuwa sehemu ya kila hatua.

Akizungumzia kipindi cha urais, Michelle ameeleza jinsi mume wake alivyokabiliana na changamoto kubwa za kisiasa na kijamii bila kuyumba.

Hata hivyo, badala ya kukata tamaa au kukasirika, Obama anaelezwa kama mtu aliyebaki mtulivu, mwenye subira na anayefikiri kwa mtazamo wa mbali.

“Miaka minane katika moto mkali wa majaribio, na hata mara moja hukuyeyuka kutokana na joto lake, wala hukuruhusu likakufanya uwe mgumu na usiye na hisia. Ulikuwa mtulivu katika kila hatua, kila mara umekusudia, kila mara umetulia, kila mara ukiangalia mbali zaidi.”

Hukuwahi kufikiria kukata tamaa hata mara moja chini ya shinikizo, kulipuka kwa hasira kwa kuchukizwa, au kupoteza uvumilivu wako. Ulikuwa tayari kufanya chochote kuifanya familia yetu na taifa hili lote lijivunie.”

Amesema katika kipindi cha uongozi wake alikuwa tayari kufanya kazi ya watu, kuokoa uchumi, kupanua huduma za afya, kumaliza vita, kutoa amri ya uvamizi wa kumkamata Osama bin Laden, kuokoa sekta ya magari na kushinda Tuzo ya Amani.

“Na ulifanya yote hayo kwa neema, hadhi na utulivu kiasi kwamba ulifanya kazi ngumu zaidi duniani ionekane kama matembezi katika bustani nzuri”.

Ni picha inayowiana na wajibu wa baba katika familia ya leo kuwa nguzo ya utulivu hata wakati wa misukosuko, kutoongozwa na hasira, bali hekima na uvumilivu.

“Ulikuwa ukitupa kila mara kilicho bora zaidi ndani yako. Na kwa kufanya hivyo, ulitukumbusha sisi wengine kwamba tunaweza kufanya hivyo pia. Barack, hakuna maneno ya kutosha kueleza jinsi ninavyojivunia namna ulivyojitokeza na unavyoendelea kujitokeza kila siku.

“Imekuwa heshima kuwa kando yako… umetupa sisi sote mfano tunaopaswa kuiga. Na natumaini unajua kwamba hakuna wito wa juu zaidi kuliko huo.” amesema Michelle

Michelle pia amegusia mafanikio ya Obama katika uongozi wake kuimarisha uchumi, kupanua huduma za afya, kukabiliana na migogoro ya kimataifa na kusimamia maamuzi magumu ya kitaifa.

Lakini, zaidi ya mafanikio hayo ya kisiasa, ameeleza kuwa mumewe ni mfano wa uongozi uliojaa heshima, utu na unyenyekevu.

“Hukuwahi kuangukia kwenye mtego wa suluhisho la haraka au pesa za haraka. Hukubadilika kutoka yule kijana mwenye maono wa kazi ya mafunzo ya majira ya kiangazi ambaye alikuja siku ile ya mvua tulipokutana kwa mara ya kwanza, bila mwavuli” amesema Michelle huku akilengwa na machozi.

Katika muktadha wa Siku ya Baba Duniani, hili linaibua mjadala muhimu je, baba wa leo anapimwa kwa kipato au kwa maadili anayoyaacha kwa familia yake?

Michelle ametoa jibu kwa vitendo aliposema Obama ni mfano ambao wengine wanaweza kuuiga.

Siku ya Baba Duniani inapoadhimishwa, maneno ya Michelle yanabaki kama ujumbe kuwa baba si nafasi ya kawaida, bali ni wito wa kipekee unaohitaji uthabiti, upendo, uvumilivu na mfano wa kuigwa.

Obama Presidential Center ni mradi ulioanzishwa na Obama pamoja na Michelle kwa lengo la kuhifadhi kumbukumbu za urais wa Obama na kuwa kitovu cha elimu, uongozi na ushirikishwaji wa jamii.

Kituo hicho kipo katika eneo la Jackson Park kusini mwa jiji la Chicago, eneo ambalo pia ni karibu na mahali alipoanza safari yake ya kisiasa Barack Obama.

Mradi huo unajumuisha jengo la makumbusho linaloeleza historia ya maisha na urais wa Obama, maktaba na vituo vya kujifunzia, kumbi za mikutano na mafunzo ya uongozi kwa vijana, maeneo ya wazi kwa shughuli za jamii, bustani na sehemu za mapumziko kwa wananchi.

Tofauti na maktaba nyingi za marais wa Marekani, kituo hiki kimeundwa zaidi kama kituo cha jamii na elimu, badala ya kuwa sehemu ya kuhifadhi nyaraka pekee.

Kwa Obama mwenyewe, kituo hiki kinatarajiwa kuwa urithi wa kudumu unaolenga kuhamasisha kizazi kipya cha viongozi na kuendeleza ushiriki wa wananchi katika masuala ya kijamii na kisiasa.

Hafla ya uzinduzi wa kituo hicho ilihudhuriwa na maelfu ya Wamarekani wakiwemo marais wastaafu wa Taifa hilo walioambatana na wake zao. Alikuwepo Bill Clinton na mkewe Hilary Clinton, George W Bush na mkewe Laura Bush pamoja na Joe Biden na mkewe Jill Biden.

Kila Jumapili ya tatu ya mwezi Juni, mataifa mengi duniani huadhimisha Siku ya Baba, siku maalumu inayotumika kutambua mchango wa baba katika malezi ya watoto, ustawi wa familia na maendeleo ya jamii.

Ingawa leo imekuwa sehemu ya utamaduni wa kimataifa, historia ya siku hiyo inaanzia zaidi ya karne moja iliyopita nchini Marekani, ambako ilizaliwa kutokana na juhudi za binti mmoja aliyetamani kuona baba yake akipewa heshima sawa na ile ya akina mama.

Mwanzo wa wazo la kuadhimisha Siku ya Baba ulitokea mwaka 1908 katika jimbo la West Virginia, Marekani, baada ya kufanyika ibada maalumu ya kuwaenzi wanaume na akina baba 361 waliopoteza maisha katika ajali ya mlipuko wa mgodi wa makaa ya mawe.

Hatua kubwa zaidi ilikuja mwaka 1910 kupitia juhudi za Sonora Smart Dodd wa mjini Spokane, Washington. Dodd alihamasishwa na maadhimisho ya Siku ya Akina Mama na akaona kuna umuhimu wa kuwepo siku maalumu ya kuwatambua akina baba.

Chanzo cha msukumo wake kilikuwa maisha ya baba yake, William Jackson Smart, mwanajeshi mstaafu aliyebeba jukumu la kuwalea watoto sita peke yake baada ya kufiwa na mke wake. Dodd aliamini kuwa kujitolea kwa baba yake kulistahili kutambuliwa na kuheshimiwa na jamii.

Kutokana na juhudi zake, Juni 19, 1910, maadhimisho ya kwanza rasmi ya Siku ya Baba yalifanyika mjini Spokane, yakifungua ukurasa mpya wa kutambua mchango wa wanaume katika familia.

Hata hivyo, ilichukua zaidi ya miongo sita kabla ya siku hiyo kupata hadhi rasmi ya kitaifa nchini Marekani. Mwaka 1972, Rais wa wakati huo, Richard Nixon, alisaini sheria iliyotambua rasmi Siku ya Baba kuwa maadhimisho ya kitaifa yanayofanyika kila Jumapili ya tatu ya mwezi Juni.

Tangu wakati huo, maadhimisho hayo yameendelea kuenea katika nchi mbalimbali duniani, yakibeba ujumbe wa kuthamini upendo, uongozi, ulinzi na malezi yanayotolewa na baba na walezi wengine wa kiume.

Leo, Siku ya Baba imekuwa zaidi ya tukio la kalenda. Ni fursa ya familia kukutana, kutoa zawadi, kuandika jumbe za shukrani na kutafakari mchango wa baba katika maisha ya watoto na jamii kwa ujumla.

Katika dunia inayobadilika kwa kasi, maadhimisho haya yanaendelea kukumbusha umuhimu wa nafasi ya baba kama nguzo ya familia, mlezi, mshauri na mfano wa kuigwa kwa vizazi vinavyokua.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports