Maswa. Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vincent Naano amesema mafanikio ya kutokomeza malaria hayawezi kupatikana kwa juhudi za sekta ya afya pekee, bali yanahitaji ushiriki wa moja kwa moja wa wananchi katika kutunza mazingira na kuzuia mazalia ya mbu wanaosambaza ugonjwa huo.
Dk Naano ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Juni 21, 2026 wakati wa uzinduzi wa kunyunyizia viuatilifu vya kibaiolojia katika mabwawa, madimbwi na maeneo mengine yanayotumika kama mazalia ya mbu katika Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu.
Amesema pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kudhibiti malaria, mafanikio ya kudumu yatapatikana ikiwa wananchi wataendelea kushiriki kikamilifu kwa kuhakikisha mazingira yao yanakuwa safi, kuondoa maji yaliyotuama na kutumia vyandarua vyenye dawa kila wanapolala.
Amesema malaria bado ni miongoni mwa magonjwa yanayoathiri afya na maendeleo ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt Vicent Naano akizungumza kabla ya kuanza kaa zoezi la kupulizia dawa ya viuadudu vya kibailojia vya mbu wanaoneza ugonjwa wa.malaria. Picha na Samwel Mwanga
“Ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake wa kutunza mazingira na kutumia chandarua, tunaweza kufikia lengo la kuwa na wagonjwa wa malaria. Vita hii haiwezi kuachiwa sekta ya afya pekee, ni jukumu la kila mwananchi,” amesema Dk Naano.
Amesisitiza kuwa, kampeni ya kunyunyizia viuatilifu vya kibaiolojia inalenga kuharibu mazalia ya mbu kabla hawajafikia hatua ya kuzaliana na kuendelea kusambaza ugonjwa huo kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, amewataka watendaji wa afya na viongozi wa Serikali za mitaa kuhakikisha dawa zilizotolewa na Serikali zinawafikia wananchi katika maeneo yote yaliyokusudiwa na kutumika kwa malengo yaliyopangwa.
“Dawa hizi zisibaki maghalani. Ni lazima ziwafikie wananchi kwa wakati na zitumike katika maeneo yote yanayotambulika kuwa mazalia ya mbu ili kufanikisha lengo la kupunguza maambukizi ya malaria,” amesema.
Aidha, amewasisitiza wananchi, hawapaswi kutozwa fedha yoyote katika utekelezaji wake kwa kuwa Serikali tayari imegharamia dawa hizo kama sehemu ya mkakati wa kulinda afya za wananchi.
“Serikali imewekeza rasilimali kubwa kuhakikisha dawa hizi zinapatikana. Hivyo, hakuna mwananchi anayepaswa kulipia huduma hii kwa namna yoyote ile,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa amesema licha ya maboresho ya huduma za afya yaliyofanyika katika wilaya hiyo, malaria bado inaendelea kuwa tishio kwa makundi yenye hatari kubwa zaidi, hususan wanawake wajawazito na watoto walio chini ya miaka mitano.
Amesema kutokana na hali hiyo, halmashauri imeamua kuongeza nguvu katika kuangamiza mazalia ya mbu sambamba na kuendelea kutoa elimu ya kinga kwa wananchi.
Mratibu wa Malaria Wilaya ya Maswa, Naomi Nyangindu amesema juhudi za Serikali na wadau wa afya zimeanza kuonesha matokeo chanya baada ya kiwango cha maambukizi ya malaria kupungua kutoka asilimia 21 hadi asilimia 3 katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu.
Amesema mafanikio hayo yametokana na mikakati mbalimbali ikiwamo matumizi ya vyandarua vyenye dawa, utoaji wa elimu ya afya kwa wananchi na kuangamiza mazalia ya mbu kwa kutumia viuatilifu vya kibaiolojia.
Mratibu wa Malaria Wilaya ya Maswa, Naomi Nyangindu (aliye kati) akisoma taarifa ya kiwango cha ugonjwa wa malaria katika wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga
Kwa mujibu wake, wilaya hiyo imepokea lita 900 za dawa za kunyunyizia mazalia ya mbu zenye thamani ya Sh10 milioni zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza kampeni hiyo.
“Dawa hizi zitatumika katika maeneo yote yenye mabwawa na madimbwi. Hazina madhara kwa binadamu wala wanyama kwani zinalenga kuharibu vijidudu vinavyowezesha mbu wa malaria kuzaliana,” amesema Nyangindu.
Hatua hiyo imepokewa kwa matumaini makubwa na wananchi wa Maswa ambao wanaamini itasaidia kupunguza maambukizi ya malaria na gharama za matibabu kwa familia nyingi.
Lucy John, mkazi wa Kitongoji cha Mnadani, amesema kampeni hiyo imekuja wakati muafaka kutokana na ongezeko la mbu katika kipindi cha mvua.
Naye Lydia Mathias amesema mafanikio ya kampeni hiyo yatategemea pia ushiriki wa wananchi katika kutunza mazingira yao.
“Dawa peke yake haitoshi. Sisi wananchi tunapaswa kuondoa maji yaliyotuama na kuhakikisha mazingira yanakuwa safi ili kuzuia mbu kuzaliana,” amesema.















