IRINGA: KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi amewataka Watanzania kutowasikiliza wanasiasa wanaotumia majukwaa ya siasa kubeza na kupunguza thamani ya maendeleo yaliyofanya ya serikali.
Kihongosi amesema hayo Juni 20,2026 alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa mkoani Iringa.
“Msisikilize wanaopita kwenye majukwaa wakisema hakuna maendeleo yaliyofanyika, maendeleo yapo na yanaonekana. Shule ,vituo vya afya vimejengwa, huduma za maji zinaendelea kuboreshwa na miradi mingi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi,” alisema Kihongosi.

Alisema inashangaza baadhi ya viongozi wa kisisasa kufika mkoani humo kupitia ndege ya Air Tanzania kisha kutua katika uwanja wa ndege Nduli ambao serikali ya Rais Samia imetoa Sh bilioni 68 kuujenga, alafu kusema hakuna kilichofanyika.
Alisema wapo wanaosema barabara siyo maendeleo jambo ambalo siyo sahihi kwani barabara zimechochea kasi ya maendeleo na uchumi wa wananchi katika maeneo
mbalimbali nchini.
Aliongeza wazee ndiyo wenye kufahamu hali iliyokuwa awali na sasa, akifafanua kuwa sehemu kubwa ya barabara zilizopo nchini zinapitika, hivyo anayesema uongo anapaswa kukosolewa.

“Wananchi wanaona wenyewe maendeleo yaliyopo katika maeneo yao, kazi yetu ni kuendelea kutatua changamoto zilizobaki huku tukilinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana,” alisema.













