MTWARA: MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mtwara imesema, kumekuwa na muamko mkubwa kwa walipa kodi kulipa kodi kwa hiyari pasipo kulazimishwa.
Yamejiri hayo hayo Juni 20, 2026 wakati wa zoezi la usafi wa mazingira katika kuadhimisha miaka 30 ya TRA tangu kuanzisha kwake mwaka 1996 lililofanyika kwenye baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara ikiwemo eneo la soko kuu mtwara.
Akiwasilisha salamu za Kamishna Mkuu wa TRA, Meneja wa TRA Mkoa wa Mtwara Maimuna Khatib amesema mkoa huo umebadilika katika ukusanyaji wa mapato tofauti na miaka ya nyuma.
“TRA imekuwa ikitambua wajibu wake wa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi na mazingira wanayoishi”amesema Maimuna
Pia amezitaka taasisi zingine kuwa na utaratibu wa kufanya zoezi la usafi wa mazingira ili kuongeza umoja na ushirikiano baina yao na wananchi.
Naye Mkurugenzi Manispaa hiyo Hassan Nyange ameipongeza TRA kwa zoezi la kufanya usafi na kutoa wito kwa wananchi kuwa na utaratibu wa kufanya usafi pasipo kusubiri baadhi ya taasisi kujitoa.
Meneja wa Chemba ya Taifa ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TNCC) Juma Napinda amesema kumekuwa na ushirikiano mzuri baina yao ya wafanyabiashara mkoani humo pamoja na mamlaka hiyo na ndio mana wamejumuika katika zoezi hilo la kufanya usafi.
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake Mkoa wa Mtwara, Mwajuma Ankon amesema wameshiriki zoezi hilo kama sehemu ya muendelezo wa mahusiano mazuri katika ukusanyaji wa kodi na TRA .












