TULINDE AMANI, TUIMARISHE MAENDELEO NA TUENDELEE KUISIMAMIA SERIKALI – Habari Mpya

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amewataka wananchi wa mkoa wa Iringa kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano huku wakijiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi. Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, Kihongosi alisema maendeleo yanayoonekana…

admin Avatar

by

3 minutes

Read Time

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amewataka wananchi wa mkoa wa Iringa kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano huku wakijiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, Kihongosi alisema maendeleo yanayoonekana katika sekta mbalimbali yamewezekana kutokana na uwepo wa amani na utulivu nchini, hivyo wananchi wana wajibu wa kuvilinda vitu hivyo muhimu kwa mustakabali wa taifa.

Alisema Iringa ina nafasi ya kipekee katika maisha yake ya kisiasa kwani ndiyo mkoa uliomlea na kumpa nafasi zake za kwanza za uongozi, jambo lililomfanya kurejea kwa unyenyekevu mkubwa kuwashukuru wananchi wa mkoa huo kwa mchango wao katika safari yake ya kisiasa.

“Daima nitabaki kuwa kiongozi msikivu, mwenye kuheshimu watu wote na mwenye kuthamini mchango wa wananchi. Iringa ni sehemu muhimu sana katika maisha yangu,” alisema.

Kihongosi alisema ziara yake mkoani Iringa ilikuwa na malengo matatu makuu ambayo ni kukagua uhai wa chama, kutembelea miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.

Alieleza kuwa baada ya kutembelea mashina mbalimbali ya CCM katika Wilaya za Kilolo na Iringa Mjini, ameridhishwa na uimara wa chama hicho katika mkoa huo na kuwapongeza mabalozi na viongozi wa chama kwa kazi wanayoifanya.

Kuhusu miradi ya maendeleo, alisema CCM ina jukumu la kuisimamia serikali yake ili kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alitaja baadhi ya miradi aliyotembelea kuwa ni pamoja na Chuo cha VETA Kilolo chenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.6, skimu ya umwagiliaji ya Ruaha Mbuyuni yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 23 pamoja na miradi mbalimbali ya elimu, afya na miundombinu iliyotekelezwa katika Mkoa wa Iringa.

“Tumeshuhudia utekelezaji wa Ilani ya CCM ukiendelea kwa vitendo. Miradi mingi imekamilika na wananchi wanaendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali,” alisema.

Katika hotuba yake, Kihongosi alisisitiza umuhimu wa kulinda amani na kuonya dhidi ya vitendo vya vurugu, uchochezi na uharibifu wa mali za umma.

Alisema uharibifu wa shule, vituo vya afya, vituo vya polisi na miundombinu mingine ya umma huathiri moja kwa moja wananchi wanaotegemea huduma hizo, huku akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana katika mazingira ya machafuko.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama akisema vina mchango mkubwa katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuwepo nchini.

Kihongosi pia alitumia nafasi hiyo kuelezea mafanikio mbalimbali ya serikali ya CCM, akitaja upanuzi wa huduma za umeme vijijini, ujenzi wa barabara za lami, miradi mikubwa ya kimkakati pamoja na maendeleo katika sekta za afya, elimu na usafiri.

Alisema kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Mwalimu Julius Nyerere pamoja na maendeleo ya reli ya kisasa ya SGR ni miongoni mwa mafanikio makubwa yanayoonyesha dhamira ya serikali ya kuharakisha maendeleo ya nchi.

Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, Kihongosi alisema CCM itaendelea kuomba ridhaa ya wananchi kwa kuzingatia utekelezaji wa ilani yake na rekodi ya utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi.

Aliwahimiza wananchi kuendelea kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya kiuchumi badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na ustawi wa jamii.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali pamoja na mamia ya wananchi kutoka maeneo tofauti ya Mkoa wa Iringa waliofika kusikiliza maelezo kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikilizwa kero zao.

About the Author

About the Author

Easy WordPress Websites Builder: Versatile Demos for Blogs, News, eCommerce and More – One-Click Import, No Coding! 1000+ Ready-made Templates for Stunning Newspaper, Magazine, Blog, and Publishing Websites.

BlockSpare — News, Magazine and Blog Addons for (Gutenberg) Block Editor

Search the Archives

Access over the years of investigative journalism and breaking reports