
Unguja. Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikiwa imetoa Rasimu ya Bajeti ya Mwaka 2026/27, wadau wa sekta binafsi wameonesha ubora na upungufu wa rasimu hiyo.
Kutokana na rasimu hiyo, mapato na matumizi ya SMZ kwa mwaka 2026/27 yanakadiriwa kufikia Sh8.217 trilioni ikiwa ni ongezeko la Sh1.2 trilioni ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2025/26 ya Sh6.9 trilioni.
Kati ya fedha hizo, Sh5.294 trilioni zimekadiriwa kutumika kwa utekelezaji wa mpango wa maendeleo sawa na asilimia 64.42 ya bajeti yote.
Wakizungumza katika mjadala wa sekta binafsi ulioandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kijamii, Kiuchumi na Uchambuzi wa Sera Zanzibar (ZRCP) kwa kushirikiana na Chemba ya Biashara Zanzibar (ZNCC), Mei 23, 2026 wamesema katika mipango ya maendeleo Serikali haina budi kushirikisha sekta binafsi.
Akiwasilisha mada katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa ZRCP, Dk Twahir Mohamed Khalfan amesema wanaangalia maeneo muhimu ya bajeti na mwelekeo wa kiuwekezaji wa Serikali na uamuzi wake wa kifedha yanavyoathiri katika jamii na biashara.
“Matarajio ambayo yamo kwenye rasimu hayastajabishi, kwani ni mwendelezo ambao Serikali imeufanya takribani miaka minne kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati, kwa hiyo hapa sekta binafsi inaweza kushiriki kufanya biashara na Serikali na kuleta tija kwenye miradi,” amesema Dk Twahir.
Hata hivyo, amesema uchumi wa Zanzibar unategemea zaidi utalii lakini mnyororo wa thamani ni mdogo kwa sababu hakuna sekta nyingi zinazochangia utalii, hivyo kuna hali ya kutokuwapo kwa muunganiko mzuri.
“Mathalani, bidhaa zinazouzwa kwenye utalii zinatoka nje hazizalishwi hapa, hivyo huu ni uvujaji wa fedha unaonufaisha uchumi wa nchi nyingine,” amesema.
Pia, amesema mchango wa uvuvi ni chini ya asilimia 20, kilimo kimepungua kuwa sekta muhimu kiuchumi, kuna ajira nyingi katika uvuvi na mwani lakini sio ajira bora.
Hata hivyo, amesema kuna mafanikio makubwa katika sekta ya ujenzi na ndiyo sekta inayovutia zaidi au yenye faida zaidi katika uchumi wa Zanzibar.
“Lakini bila shaka, hata katika ujenzi, malighafi nyingi zinaagizwa kutoka nje. Na Zanzibar, bila shaka, hatuwezi kuwa na viwanda vikubwa, lakini tunatakiwa kuwa na viwanda vidogo,” amesema.
Hivyo, amesema inahitaji kuzingatia katika ujenzi wa viwanda, kwani sekta hiyo inashuka na inapata uangalifu mdogo kadri muda unavyopita, huku akisema katika soko la mitaji la ndani linahitaji kupata njia ya watu wadogo, hasa wazawa kuwekeza kipato chao kidogo katika fursa za kujenga uchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Zanlink, Sanjay Raja amesema kuweka kodi ya matumizi maalumu ya silimia 17 ya intaneti ni kuifanya ionekane haramu wakati kila kitu kwa sasa kunahitajika huduma hiyo.
Amesema Serikali imetunga sera mbili zinazokinzana, sera ya kusambaza mabadiliko ya kidijitali na sera inayoweka kodi ya matumizi maalumu ya intaneti.
“Hizi ni sera mbili zinapingana, wakati wakitaka kusambaza mabadiliko ya kidijitali. Hiyo ni sera. Na kisha kuna sera inayosema tunaweka kodi ya matumizi maalumu ya asilimia 17. Haziwezi kwenda pamoja,” amesema Sanjay.
Amesema katika dunia ya sasa hakuna sekta isiyohitaji intaneti; iwe sekta binafsi, ya umma au mtu mmoja mmoja.
Mkurugenzi wa Utafiti na Uchambuzi wa Sera kutoka ZRCP, Dk Muhsin Masoud amesema kwa sasa kuna suala la mgogoro unaoikabili dunia na kusababisha bei za mafuta kupanda, jambo linalochangia bidhaa nyingine kupanda, hivyo kuna haja ya kuangalia suala hilo kwa mapana.
Amesema kila mwaka kunakuwa na baadhi ya kodi, kama Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kodi za bidhaa maalumu na nyingine zinazohusiana na bei za bidhaa.
“Ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba, sasa hivi ni wakati wa kuzidisha umakini tusitekeleze kodi hizi kulingana na gharama au bei ili kuleta unafuu,” amesema mtaalamu huyo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Hamad Omar Bakar amesema ni jambo muhimu waliofanya kujadili mwelekeo wa bajeti ya Serikali na kutoa maoni katika maeneo ya kuboresha.
Amesema kila mwaka Serikali imekuwa na vipaumbele vinavyolenga zaidi kwenye maendeleo ya umma, katika miradi ya kimkakati kwa mustakabali wa jamii nzima, wakiwamo wafanyabiashara.
Amesema miongoni mwa mambo ambayo bajeti hiyo itajikita ni kuandaa mazingira wezeshi kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na kuleta tija.
“Kila mwaka tunaendelea kuwa na maboresho ndani yake, yajikite katika mustakabali wa maendeleo kwa jumla. Lengo ni kuhakikisha tunaanda mazingira ambayo hayatakuwa na vikwazo na vizuizi,” amesema Dk Hamad.
Mkurugenzi Mtendaji wa ZNCC, Hamad Hamad amesema wanafanya mjadala huo kupitia rasimu ya bajeti ya Serikali kufahamisha umma vipaumbele na kodi zinazokwenda kubadilika na sera.
“Sekta binafsi tumezoea kuona michango barazani na wataalamu wengine bila kupata maoni na wafanyabiashara, hatujapata ushiriki mpana wa sekta binafsi, hii itakuwa ni mwendelezo kuona vipi kodi mpya zinaathiri biashara ili kuingilia mapema kabla ya athari hazijatokea,” amesema.















