Dar es Salaam. Wakati waumini wa Kiislamu Tanzania wakijiandaa kuungana na wengine duniani kuadhimisha Sikukuu ya Eid al-Adha Mei 27, 2026, bei ya mbuzi katika maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam imepanda kutokana na ongezeko la mahitaji ya mfugo huo.
Bei hiyo ya mbuzi imeongezeka kwa kiwango kinachotofautiana kulingana na ukubwa, huku wafanyabiashara wakieleza kuwa ongezeko hilo ni la kawaida kila msimu wa sikukuu hiyo unapokaribia.
Licha ya sikukuu hiyo unaweza kuchinja mnyama yoyote akiwamo ng’ombe au kondoo, mbuzi ndiye anaonekana kuwa kimbilio la wengi kutokana na gharama yake kuwa chini.
Katika baadhi ya maeneo, mbuzi waliokuwa wakiuzwa kati ya Sh90, 000 hadi Sh100,000 wiki kadhaa zilizopita sasa wanauzwa kwa kati ya Sh120,000 hadi zaidi ya Sh150,000 kutegemea ubora wa mnyama husika.
Wafanyabiashara wa mifugo hiyo wanasema ongezeko hilo linachangiwa na wateja wanaotafuta mbuzi wa kuchinja kwa ajili ya kutimiza ibada ya Eid al-Adha.
Akizungumza na Mwananchi, leo Jumapili, Mei 24, 2026 mfanyabiashara wa mbuzi, katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam Khafidhi Ramadhani amesema kadiri sikukuu inavyokaribia ndivyo wateja wanavyoongezeka na kusababisha bei kubadilika haraka.
“Kwa kawaida bei hupanda siku za mwisho kwa sababu watu wengi huja kununua kwa wakati mmoja. Wiki mbili zilizopita tulikuwa tunauza kwa bei ya chini kidogo lakini sasa mahitaji ni makubwa, ndiyo maana hata bei zimepanda,” amesema Hassan.
Amesema licha ya ongezeko hilo, bado baadhi ya wateja wanaendelea kununua kwa sababu wanaona ni sehemu ya ibada muhimu kwa familia zao.
Naye Hamisi Ali anayejishughulisha na uuzaji wa mbuzi Vingunguti amesema pamoja na bei ya wanyama hao kuwa juu kwa sasa, haijapanda sana kama ilivyokuwa mwaka jana katika kipindi cha maandalizi ya sikukuu hiyo.
“Mwaka jana katika kipindi kama hiki mbuzi alianzia kuuzwa kati ya Sh150,000 hadi Sh180,000 hivyo kwa Eid ya mwaka huu bei haijapanda sana,” amesema.
Kwa upande wake, mmoja wa wanunuzi, Salum Mohamed mkazi wa Temeke amesema ongezeko la bei limeongeza mzigo wa gharama, lakini kwa waumini wengi suala la kuchinja bado linaendelea kuwa la kipaumbele.
“Ukweli bei zimepanda tofauti na tulivyotarajia. Lakini kwa kuwa ni ibada, watu wanajitahidi kutafuta namna ya kumudu,” amesema.
Naye Ashura Juma, mkazi wa Kinondoni amesema licha ya kupanda kwa bei, bado wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia uhalisia wa maisha ya wananchi.
“Tunafahamu ni biashara na wanatafuta faida, lakini pia waangalie uwezo wa watu. Wengine wanatamani kushiriki ibada lakini wanakwama kutokana na gharama kuwa kubwa,” amesema.
Kwa upande mwingine, wasafirishaji wa mifugo wameeleza kuwa ongezeko la bei ya mafuta kulikochangia kupanda kwa gharama za usafirishaji pamoja na ongezeko la uhitaji wa pia vinachangia kupaa kwa bei katika kipindi hiki.
Tino Msuya anayejishulisha na kusafirisha wanyama kutoka mikoa mbalimbali amesema mbuzi wengi wanaosafirishwa kutoka mikoani kwenda Dar es Salaam huingia sokoni kwa gharama zaidi kutokana na ongezeko la bei ya mafuta linaloathiri bei ya mwisho kwa mnunuzi.
Licha ya changamoto hiyo, baadhi ya wananchi wameendelea kueleza matumaini yao kuwa baada ya sikukuu bei za mifugo zitarejea katika hali ya kawaida, huku wakitoa rai kwa wafanyabiashara kuweka bei zinazozingatia hali ya uchumi wa wananchi katika kipindi hiki cha maandalizi ya Eid al-Adha.















